Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

AIBU KUBWA MREMBO ADAKWA KWA WIZI HOSPITALI!

 
MREMBO mmoja aliyejulikana kwa jina la Mariam Moshi (23), mkazi wa Mwananyamala Ujiji, aliponea chupuchupu kuuawa na wagonjwa wenye hasira kali waliolazwa katika Hospitali ya Mwananyamala jijini Dar baada ya kudaiwa kuiba nguo. 
Mariam Moshi akihamaki baada ya kukamatwa na nguo anazodaiwa kuiba katika wodi ya wazazi Hospitalini Mwananyamala.
Walinzi wa hospitali hiyo walimuokoa mrembo huyo kwa kumnasua mikononi mwa wagonjwa hasa wajawazito walioenda kujifungua, waliodai kwamba Mariam aliingia katika wodi yao na kuwaibia.Tukio hilo lilitokea Machi 27, mwaka huu saa tisa alasiri, ambapo mama mmoja ndiye alishtuka kwa kuona amechukuliwa kitenge chake kipya.
Mama huyo alipobaini ameibiwa, alitoka nje na kuangaza macho huku na kule akiangalia alipoelekea Mariam aliyekuwa wodini kwao, ndipo alipomuona akiwa anatoka nje kulielekea geti ambapo aliwapigia kelele walinzi ili wamzuie.
 
Mariam akiwa mikononi mwa mlinzi wa hospitali hiyo.
“Walinzi walimsimamisha na kumuuliza kama aliiba kitu chochote wodini akirudishe, lakini alikataa katakata kuhusika ma wizi huo,” kilisema chanzo.
Hata hivyo, walinzi walipompekua, aligundulika kuwa na vitu alivyovifunga na kufunika kwa dera (gauni kubwa, refu alilokuwa amevaa).Askari wa kike walipomfunua gauni hilo, walimkuta akiwa na taulo ambalo alikuwa amelifunga kiunoni pamoja na kitenge alichokuwa akituhumiwa kukiiba wodini.
Baada ya wagonjwa kuona mali alizoiba mrembo huyo, ndipo akina mama wengine wakiwa na watoto wao walitoka wodini na kuanza kupiga makelele kwa hasira wakitaka apewe mkong’oto.
 
Walinzi hao wakitoa baadhi ya vitu alivyoiba.
Hata hivyo, walinzi wa hospitali hiyo walipoona Mariam amezongwa, ilibidi watumie nguvu kumuokoa na kumweka chini ya ulinzi wakisubiri namna ya kumpeleka polisi.Mariam alipohojiwa na waandishi wetu juu ya kitu kilichompeleka hospitalini hapo, alisema alikwenda kuwaona wagonjwa ambao hata hivyo alishindwa kuwataja. Alisema yeye ni mwenyeji wa Dodoma anayeishi Dar kwa kujitegemea.
Aliomba msamaha kwa kitendo alichokifanya, akisema kinatokana na maisha magumu na katika hali ya kushangaza zaidi, alipoulizwa kuhusu taulo alilokuwa amejifunga ndani ya dera alilovaa, alisema halikuwa la hospitalini hapo, bali aliliiba katika gesti aliyokuwa amelala siku hiyo.
 
...Wakimuhoji.
Wauguzi wa hospitali hiyo walidai malalamiko ya wagonjwa kuibiwa mali zao hospitalini hapo ni jambo la kawaida, hivyo siku hiyo ilikuwa ni ‘40’ ya Mariam.
KWAKO Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima. Pole sana kwa masaibu yaliyokupata na bila shaka, Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, atakujaalia afya njema hivi karibuni.
Binafsi mimi mwananchi wa kawaida  nisiyekuwa na cheo chochote cha dini wala siasa, ni mzima wa afya na ninaendelea na shughuli zangu za kila siku likiwemo hili la kukuandikia wewe barua.
Kama ulikuwa hufahamu, kupitia hii barua yangu huwa nawakumbuka watu mbalimbali wenye majina katika jamii yetu. Leo nimekukumbuka wewe, japo naamini hatujawahi kuonana ana kwa ana lakini nautambua mchango wako kama kiongozi wa dini mwenye heshima kubwa kwa waumini wengi walio nyuma yako.
Wengi hawategemei kukuona katika jambo lolote ambalo litakuwa kinyume na matakwa ya Mungu. Mungu ni mpole na mnyenyekevu. Kwenye amri zake ametuzuia kufanya matendo maovu likiwemo la matusi.
Hapo ndipo kwenye msingi wa barua yangu. Kama msikilizaji mwingine, nilipata kusikia sauti yako ikimdhihaki kiongozi wa Kanisa Katoliki, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo kwa maneno machafu yasiyo na staha hata kidogo kutamkwa na kiongozi mkubwa wa dini kama wewe.
Nilijiuliza uliuweka uchungaji pembeni ulipokuwa unazungumza lugha kali kama ile? Maneno mazito kama yale hayakupaswa kuzungumzwa na mtu kama wewe, hata kama uliyekuwa unamtuhumu ametenda kosa kiasi gani, haikuwa busara hata kidogo kutamka maneno machafu yasiyo na hekima.
Maneno uliyoyatamka katika kinywa chako, yangetamkwa na mhuni wa mtaani wala nisingeshtuka. Nisingeona jambo hilo ni la ajabu kwani maneno kama hayo na mazito, yanatamkwa sana uswahilini kwetu.
Nimeshtuka sababu wewe ni mchunga kondoo wa Bwana. Wewe una dhamana ya kufundisha mema, ni kiongozi. Tena huongozi kikundi cha siasa, unaongoza kanisa lenye waumini wengi.Mbaya zaidi, kiongozi uliyemtusi naye ni kiongozi mkubwa wa dini. Ana dhamana kubwa ya kuwaongoza waumini kama wako au pengine zaidi yako.
Kimsingi busara zilipaswa kukuongoza kufikisha ujumbe uliokuwa umekusudia.
Kama uliona amekosea kutofautiana na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT) na Jumuiya ya Kikristo (CCT) katika suala la Katiba Inayopendekezwa, ungetumia lugha nzuri kumueleza kwa hoja.

WAUMINI WA GWAJIMA WAFUNGA SIKU 40

WAKATI mambo yakiwa bado tete juu ya afya ya kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima la jijini Dar es Salaam, Mchungaji Josephat Gwajima, wafuasi wake wametangaza kufunga kwa muda wa siku 40 kuanzia juzi Jumatatu ili kuomba.
Mchungaji Josephat Gwajima akiwa hospitali.
Chanzo kilicho ndani ya kanisa hilo ambalo kwa sasa makao makuu yake yapo Kawe, kililiambia gazeti hili kuwa wafuasi hao wameamua kuliacha suala hilo mikononi mwa Mungu, hivyo wameona ni vyema kufunga kwa muda huo ili kumuombea kiongozi wao apate afya njema, lakini pia misukosuko inayomuandama imalizike.
“Jamaa wameona hali sasa inakuwa ngumu, wanafunga kwa vikundi, kila mmoja anamuombea apate afya njema baada ya kuzidiwa wakati akihojiwa, lakini pia wanataka haya mambo yamalizike, kwa hiyo wameona ni bora kumuachia Mwenyezi Mungu ili ayamalize,” kilisema chanzo hicho.

Waumini.
Mchungaji Gwajima alianguka ghafla wakati akihojiwa na maofisa wa Polisi wa Kanda Maalum ya Polisi Dar es Salaam, kufuatia maneno yake ya kashfa dhidi ya Askofu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarb Kardinali Pengo.
Baada ya kuanguka, mchungaji huyo amekuwa akitibiwa katika Hospitali ya TMJ iliyopo Mikocheni ambako hali yake imeelezwa kuwa bado tete, huku kukiwa na taarifa za kukamatwa kwa watu 15 wanaodaiwa kupanga mipango ya kumtorosha kiongozi huyo wa kiroho kutoka mikononi mwa polisi wanaomlinda.

Migomo yaendelea kutikisa kila kona nchini Tanzania ambapo Tabora wafanya biashara nao wagoma.

Wananchi manispaa ya Tabora wamekuwa katika wakati mgumu wa kununua bidhaa mbali mbali baada ya wafanyabiashara  wa maduka yote ya maeneo ya soko kuu mjini humo,  kufanya mgomo wa kushitukiza wakiishinikiza serikali kwa mambo matatu, ya kumpa dhamana mwenyekiti wao kitaifa,Bw.Johnson Minja,kuongezeka kwa kodi asilimia mia moja,na matumizi ya mashine za EFDS.
Wakiongea na ITV katika  sehemu za maduka hayo akiwemo Mwenyekiti wa wafanyabiashara hao wamesema kuwa, hali ambayo imewafanya kugoma ni kutokana na malalamiko yao kutosikilizwa kwa mda mrefu, pamoja na juhudi ambazo zimekuwa zikifanywa na viongozi wao jambo ambalo limekuwa ni kitendawili huku wakiongezewa kodi. 
 
Akizungumza na wafanyabiashara hao mwenyekiti wa kamati ya ukusanyaji wa kodi wilaya hiyo ya Tabora mjini, ambaye pia ni mkuu wa wilaya hiyo Bw.Suleimani Kumchaya,amewataka kutokuwa na maamuzi yanayoathiri jamii bali kufanya makubaliano yanayoleta maendeleo katika jamii,kuliko kuchukua hatua za maamuzi na za haraka.

Matusi na ngumi zatawala baraza la wawakilishi Zanzibar.

Wajumbe wa baraza la wawakilishi wameweka tofauti za seriklai ya kitaifa pembeni na kuanza kutupiana matusi na  kutishia kupigana hadharani ndani ya baraza baada ya mabishano kuhusu hoja ya vitambulisho vya Zanzibar.
Hali hiyo ambayo haijawahi kutokezea  ndani ya baraza hilo ilianza wakati wajumbe walipokuwa wakianza  kuchangia hoja hiyo binafsi ya mwakilshi wa CUF Mh. Hamad Masoud ambapo mwakishi wa CUF jimbo la magogoni Mh. Abdillahi Jihad ambaye pia ni waziri alipaonza kumshambulia wazir wa nchi tawala za mikoa na idara maalum  Mh. Haji Omar Kheir
 
Hapo ndipo sakata hilolilipoanza  ambapo  naibu  waziri amabye ni CCM Mh. Haji Gavu alipaona kukwaruzana kwamaneno na matusi dhidi ya mwakilishi wa CUF na kutaka kugeuza ukumbi huo kuwa wa masumbwi.
 
Pamoja na jitihada za spika Mh. Pandu Ameir Kificho kutaka kuwepo kwa amani na utaratibu hakiusaidii  lolote na fujo hizo zikageuka kwa wawakilishi wa CCM Mh. Hamza Hassan Juma na mwakilishi wa CUF Mh. Salum Nassor ambao mnao wataka kuzipiga na kutishiana kwenda nje.
 
Hili ni tukio la pili kutokea ndani ya mkutano huu wa baraza ambao wawakilishi wa CUF na CCM kuvutana na kubishana kwa maneno ya matusi na kejeli.

Mwanamuziki Suma Lee Akata Shauri Aamua Kuacha Mziki, Aagiza Nyimbo zake zifutwe na Redio Wasizipige Tena

Hit maker wa ‘Hakunaga’, Suma Lee amesema kuwa hatafanya tena muziki kwasababu ameachana kabisa na maisha hayo na ameamua kusomea dini ya kiislam

Suma ambaye alitengeneza pesa nyingi kupitia hit yake ya ‘Hakunaga’, amesema kuwa hana mpango wa kuzitoa nyimbo zake zilizoko studio ambazo hazijatoka.

“sifanyi tena muziki na nimeachana kabisa na maisha hayo, na nyimbo zote zilizobaki studio nimezisimamisha zisitoke baada ya kuzilipia, “ Alisema Suma.

“kuna wimbo mmoja nimefanya na Cp ambao ndio ulikuwa wa kurudisha kundi la Parklane, pia nimeuzuia, labda Cp auchukue yeye.Kilichobaki ni kuwaombea wazazi wetu waliotutangulia, wengine walikuwa hawataki tufanye kazi hizi, kwa kuwa hawapo na hakuna wakutukataza tena, bora tukae na kuwaombea.”

Baada ya Mahojiano, Gwajima Aachiwa kwa Dhamana, Kwenye Hii Kesi Nani Mlalamikaji ?

Taarifa zimeenea kuwa baada ya Kutoka hospitalini Gwajima alikwenda moja kwa moja Kituo cha polisi Ostabey kwa ajili ya kumaliza mahojiano yake na Polisi kuhusu kumtukana Askofu Pengo...Baada ya mahojiano Askofu Gwajima Ameachiwa Huru kwa Dhamana....

Najiuliza kwa Sauti:
Katika Hili Sakata ni Nani Mlalamikaji ? Wakati kila mkubwa akijidai hausiki kwenye sakata hili
Je Pengo Amemshitaki ?

Nguvu na Ushawishi wa Lowassa Waongezeka Maradufu

*Tafiti Mpya Za Kitaalamu Zadhihirisha Uhalali wake Kisiasa

*Kauli ya Jk yaongezewa nguvu na Tafiti Mpya za PTT

*Kauli ya mjumbe kamati kuu Jerry Slaa Yampa majibu nape na January "Chama chetu lazima kipeleke bidhaa inayohitajika sokoni, inayouzika na inayokidhi haja ya mnunuaji"

*Tafiti zabainisha nguvu ya Wapinzani Wa Lowassa Pinda na Membe, washindwa kutumia System kumzima Lowassa Zaweka wazi ushawishi wa Lowassa Kwa Umma.

Taasisi isiyo ya kiserikali ya Positive Thinkers Tanzania imetoa ripoti yake ya utafiti kuhusu mwanasiasa anayekubalika zaidi na wananchi katika nafasi ya Rais ajaye, Lowassa aongoza na nafasi ya 2 imeenda kwa Dr. Wilbroad Slaa huku Mwigulu Nchemba aking'ara kama kijana aliyeongoza kwa kukubalika kwa kukamata namba 3.
Ifuatayo ni orodha ya wanasiasa waliongia 10 bora na asilimia ya kura walizopata.

1. Edward Lowassa 22.8%
2. Wilbroad Slaa 19.5%
3. Mwigulu Nchemba 10.6%
4. Ibrahim Lipumba 8.9%
5. John Magufuli 6.8
6. Zitto Kabwe 6.7 %
7. Bernard Membe 5.9%
8. Mizengo Pinda 3.2%
9. January Makamba 1.6%
10. Mark Mwandosya 1.2%

Tafiti hizi zimedhirisha nguvu na ushawishi aliyonayo Edward Ngoyayi Lowassa Kama Kiongozi Kwa Jamii na Umma Wa Tanzania kwa Kiwango Cha Asilimia Alichopata Lowassa Ni dhahiri Shahiri Uchaguzi Ukifanyika leo basi ana nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi huo.

Hii ni Tofauti na Wagombea wengine ndani ya CCM ambao kama watapitishwa na chama, chama kitalazimika kutumia nguvu kubwa mno ili kupata ushindi na ushindi ambao unaweza ukawa wa asilimia moja tena baada ya uchaguzi kurudiwa ikiwa ni sehemu ya marudio baada ya round ya kwanza kuonekana kutofikia asilimia.
  Tafiti hizi zinaipa kauli ya Mh mwenyekiti na Rais wa tanzania Amiri jeshi mkuu nguvu kwani alisema " ikitokea kuna mtu ananguvu ya kutosha na mnamuona anafaa kuwa Rais basi msisite kumshauri agombee, eeh mshawishini tuuh" kwa muda wa week sasa makundi mbali mbali kada na rika mbali mbali kutoka katika kila kona ya tanzania yamekuwa yakijitokeza kwenda kumuomba Lowassa agombee urais.

Kwa Tafiti hizi watu watapata majibu ni nani anafaa na kwa nini mamia ya watanzania wanajitokeza kumshawishi Edward Lowassa Agombee,Alisema hivi karibuni mjumbe wa kamati kuu ndugu jerry silaaa Yakwamba " chama lazima kipeleke mgombea anayekubalika anayeuzika na anayeweza kukipa chama ushindi" kauli hii ilikuwa mwiba na jibu kwa nape aliyewahi kutoa kauli isiyo ya kiungwana kwa kusema chama hakiwezi kumpitisha mgombea asiyesafishika hata kwa dodoki.

Kauli hii inapingwa na takwimu za tafiti za kitaalamu kwamba Lowassa Ni sawa na kiatu kilichokwisha pakwa kiwi ni kazi ya chama kukibrush tuu" pia kauli hii ni jibu linalomjibu January makamba yakwamba Lowassa Alishapita umri wa kufanya siasa ya maigizo tafiti hizi zinaonyesha namna january anatakiwa kukuza siasa yake watanzania Wamfahamu zaidi na apate uhalali wa kisiasa.
 Alisema mama Sophia simba mjumbe wa kamati kuu Kumjibu januaru " kama unaona wenzio wanaigiza kwa kutoa pesa ili watu wawashawishi nawe toa pesa tuone kama kuna mtu atakuja kukushawishi"Pamoja na nguvu kubwa ya kibobezi inayotumiwa na wabobezi hawa wawili pinada na membe bado siasa yao imeonekana kukosa uhalali kwa watanzania tafiti za za kitaalamu mara kwa mara zimekuwa sio rafiki kwa pinda na membe kwa takwimu za tafiti kwa chama cha ccm kumpitisha membe au pinda ni sawa na kupeleka KOFIA YA POLICE DUKANI UKAIUZE Nguvu ya Mwigulu Lamerck Nchemba Imeonekana kuwa Kubwa Kuliko Hata Wabobezi hawa wawili wanaotumia ubobezi wao kupitia system ya serekali na dola kushinikiza makundi mbali mbali kuwaunga mkono.

Hivi karibuni kumekuwa na tabiya ya makundi mbali mbali yanayopewa na kupokea vitisho kutoka kwa wabobezi hawa wawili kwa kosa la kutumia uhuru wao na Dhamira yao njema ya kumshawishi edward atangaze nia na agombee urais.

UKIUWA KWA UPANGA NAWE UTAULIEA KWA UPANGA, TAFITI HIZI ZINAONYESHA SI RAHISI KUZUIYA MKUKI KWA SHUKA

PAUL MAKONDA, DK SLAA WAMJULIA HALI ASKOFU GWAJIMA

 
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilibroad Silaa (kushoto), akimjulia hali Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda akimjulia hali Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima aliyelazwa Hospitali ya TMJ kwa ajili ya matibabu baada ya kupata mshituko katika mahojiano na polisi akituhumiwa kutoa lugha isiyofaa kwa Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo.
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilibroad Silaa (kushoto), akiteta jambo na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda walipokutana Hospitali ya TMJ walipofika kumjulia hali Askofu Gwajima.

Baada ya Kuhamia Nyumba Mpya, Diamond na Zari Roho Mkononi, Yabainiki Kwake ulinzi ni Sifuri, Mwenyewe Akiri Kuishi kwa Hofu

TAHADHARI ichukuliwe! Habari zikufikie kuwa, baada ya staa mkubwa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz‘ na mpenzi wake, Zarinah Hassani ‘Zari’, kuhamia kwenye mjengo wake mpya uliopo Madale jijini Dar, imebainika kuwa familia hiyo inaishi roho mkononi kufuatia ulinzi sifuri, jambo linalowafanya kuishi kwa hofu tupu

Kikizungumza kwa hofu juu ya familia hiyo, chanzo chetu makini kilipasha kwamba, pamoja na Diamond kutumia mamilioni ya fedha kujenga nyumba hiyo ya gharama kubwa, sasa changamoto imehamia kwenye ulinzi na usalama wao

“Jamani watu wanampongeza Diamond kwa kuhamia nyumba mpya lakini wale jamaa aisee wanapaswa kuombewa kila kukicha.

“Pamoja na kushusha mjengo wa maana bado changamoto ni juu ya ulinzi wao.

“Huwezi kuamini Diamond bado anaishi kizamani sana na sijui kwa nini anajiamini kiasi hicho wakati anajua wazi kuwa yeye ni staa wa Afrika na hapaswi kuishi kwa ulinzi hafifu.

MAENEO HATARISHI?

“Nasema hivi kwa sababu hata maeneo anayoishi ni hatari sana kwake hivyo anatakiwa kuwa na ulinzi mkali ili tu siku moja asije akafanyiwa kitu ambacho taifa likaingia kwenye hasara ya kumpoteza nyota mkubwa kama yeye.

“Nina uhakika asilimia mia moja Diamond hadi leo hajaanza hata kufanya process (taratibu) za kuchukua silaha (bastola).

“Mimi naijua vizuri Madale ni sehemu ambayo watu huwa wanavamiwa mara kwa mara na wanaishi kwa hofu kama Diamond anavyoishi.

HIKI NDICHO KINACHOMPONZA

“Kitu kingine kinachomponza Diamond ni ishu ya kuweka kila kitu kilichopo ndani kwake mitandaoni. Usione kila mtu anasifia lakini kuna wengine wanavitolea macho.

“Kwa mfano katupia picha za toilet (choo) ambacho kimepakwa dhahabu na kusema kimegharimu shilingi milioni 70.

“Hajakaa sawa akatupia picha za jikoni kwake kuna vitu vingi vya thamani kubwa kila mahali mpaka kwenye korido kuna flat screen (runinga). Huko si ni kuwakejeli watoto wa mbwa? Ni vizuri akaacha kufanya hivyo kwa sababu anawapa watu tamaa,” kilitiririka chanzo hicho.

ANA ULINZI GANI?

Juu ya ulinzi wa nyumbani kwa Diamond, chanzo hicho kilidai kwamba, mbali na baunsa anayewalinda aitwaye Mwarabu hakuna askari wa silaha anayelinda nyumbani hapo hivyo jamaa anatakiwa kufanya haraka kuajiri walinzi wenye silaha.


Baada ya habari hizo na uchunguzi wa kutosha, Ijumaa Wikienda lilimsaka Diamond a.k.a Dangote au Chibu ili kujua namna anavyoishi na jinsi anavyoimarisha ulinzi wake na familia kwa jumla.

Diamond, mbali na kukiri kuwa na hofu, alikuwa na haya ya kusema: “Suala la ulinzi wangu nalijua mwenyewe lakini zaidi watu wanatakiwa kujua mimi nipo na mlinzi na ninaendelea kuimarisha ulinzi wa nyumbani kwangu.

“Sidhani pia kama ni suala zuri sana kwa watu kujua siri za ulinzi wangu ila mambo mengi ya kujilinda niko kwenye michakato ya mwisho kukamilisha na soon (haraka) mambo yote yatakaa levo maana huwezi ukafanya kila jambo kwa wakati mmoja,” alisema Diamond huku akikubaliana na ushauri wa gazeti hili juu ya kuongeza ulinzi alionao wa baunsa.

ILIWAHI KUMTOKEA SUGU

Huko nyuma iliwahi kumtokea Mwanamuziki Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema) ambapo alikuwa amerejea kutoka nchini Uingereza.

Akiwa amepanga nyumba nzima maeneo ya Tegeta, Dar, Sugu alifanyiwa makala ya runingani na kuonesha vitu vya thamani vya nyumbani kwake.

Siku chache baada ya kipindi hicho kuruka runingani, jamaa huyo alivamiwa na kuporwa kila kitu lakini yeye hakudhurika.

Emmanuel Mbasha Afunguka sakata la Gwajima katika Twitter, Asema Hayuko Tayari Kurudiana na Mkewe

Katika Sakata linaloendelea sasa la Gwajima Kumtukana Askofu Pengo na la Kuzidiwa na Kukimbizwa Hospitalini akiwa mikononi mwa Polisi , Emmanuel Mbasha ambae inasemakana yeye na mkewe kuachana kuna mkono wa Gwajima ametoa maoni yake kuhusu Sakata la Askofu Huyo..
Jisomee Hapa Chini:

TAMKO LA MAASKOFU NA WACHUNGAJI KUTOKA MADHEHEBU MBALIMBALI JUU YA TUKIO LA ASKOFU GWAJIMA.

Sisi maaskofu na wachungaji kutoka makanisa mbalimbali tumeshtushwa na kusikitishwa kwa taarifa ya ugonjwa wa Askofu na mtumishi mwenzetu Josephat Gwajima ambaye tarehe 27/03/2015 alifika kituo cha polisi cha kati kuitikia wito wa polisi uliomtaka kwenda kujibu shutuma za kutumia lugha ya matusi kwa kardinali Pengo.
Maswali yetu makuu ni kitu gani kimempata mwenzetu? Tunajiuliza, je vyombo vya usalama vimekua sio sehemu salama kama zamani?
Tukiwa bado tunatafakari hill, tumeshtushwa tena baada ya kupata taarifa ya kuwa Wachungaji Wasaidizi wa Askofu Gwajima pamoja na walinzi wake waliokuwepo hospitalini hapo kwa ajili ya kumuuguza nao pia wamekamatwa kwa tuhuma za. kutaka kumtorosha Askofu Gwajima. 
Jambo hili linashangaza zaidi maana wachungaji wale wale waliokuwa naye akiwa mzima wa afya wakati anaelekea polisi ndio wale wale wanatuhumiwa kutaka kumtorosha akiwa mgonjwa.
Ni jambo la kushangaza na lisiloingia akilini kuwa wasaidizi hao wa Gwajima walitaka kumtorosha wakati Gwajima kama angekua na nia hiyo angekwisha fanya hivyo mana alikuwa na uwezo wa kutoroka alipokua Arusha kwenye kikao cha Maaskofu wakuu wa makanisa ya Kipentekoste ambao alipata taarifa za kuitwa Polisi.
Isitoshe Gwajima aliitija wito na kwenda polisi mwenyewe kwa miguu yake bila kushurutishwa, wala hakufikishwa polisi kwa nguvu.
Swali: Kama alikua anaona ugumu wa kutoroka wakati hakuna polisi anayemlinda na huku akiwa mwenye afya tele, itakuaje rahisi kutoroshwa leo akiwa mahututi na akiwa kwenye ulinzi mkali wa polisi?
Mbona hii inastaajabisha?
Jambo jingine linalotupa shida ni kuhusu mlalamikaji wa kesi hii inayomkabili Askofu Gwajima. Tumeelezwa na wasaidizi wa Askofu Gwajima kuwa pale polisi walielezwa kuwa aliyefungua kesi hii sio Pengo ila mtu mmoja aitwaye Aboubakar.
Kwa ufahamu wetu juu ya sheria unatutuma kuamini kuwa Aboubakar sio MTU sahihi wa kufungua kesi hiyo sababu hawezi kutuonyesha ameumizwa kiasi gani na matamshi ya Askofu Gwajima.
Isitoshe, Kardinali Pengo mwenyewe ametamka katika Ibada yake ya Jumapili hii ya tarehe 29/03/2015 kuwa amemsamehe Gwajima, yupi tena mwenye uchungu wa kumzidi Kardinali Pengo?
 RAI YETU:
Rai yetu ni kwamba, ni vizuri serikali pamoja na vyombo vyake vya usalama vikatumia weledi katika kushughulikia mambo ya kidini na viongozi wake kwani yanaweza kusababisha chuki dhidi ya serikali na pia kupelekea mpasuko mkubwa wa kidini katika jamii yetu iliyo na historia nzuri ya umoja na mshikamano na ushirikiano katika matukio yote ya kimaisha.
Tunaomba serikali isaidie kuondoa mkanganyiko huu na busara kubwa itumike ili kuepusha uvunjifu wa Amani katika jamii.
MAAMUZI YETU:
Jambo hili linazungumzika, maana hata hivyo tumeshaazimia kukutana na IGP ili kupata suluhisho juu ya jambo hili.
Kwa niaba ya maaskofu na wachungaji:
Mwenyekiti: Askofu Dr. Mgullu Kilimba
Katibu: Askofu Dr. Dramas Mukassa
Na mwandishi
F.A.K
30/03/2015

Gwajima Afunguka......Asema Aliagiza Bastola yake ili Ajihami Baada ya Taarifa Kuzagaa Mitandaoni kuwa Amefariki Dunia

Hii  ni  Picha  iliyosambazwa  katika  mitandao  ya  kijamii  ikidai  kuwa  Gwajima  kafariki  dunia  na  yuko  Mochwari.Taarifa  hizi  zilimpa  hofu  Gwajima  na  kumfanya  Aagize  Bastola  yake  kwa  ajili  ya  kujihami.
**********

Utata umeibuka kuhusu bastola waliyodaiwa kukamatwa nayo wafuasi wa Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima baada ya kiongozi huyo kusema anaimiliki kihalali kinyume na maelezo ya polisi.
  

Gwajima aliyetolewa kwenye chumba cha uangalizi maalumu cha Hospitali ya TMJ jana, amelitaka Jeshi la Polisi kurudisha bastola hiyo, akisema ni mali yake na aliiagiza ipelekwe hospitalini kwa sababu ya kujilinda.
 
Akizungumza na waandishi wa habari hospitalini hapo alipolazwa baada ya kuishiwa nguvu na kupoteza fahamu akiwa katika mahojiano na polisi, Gwajima alisema anashangaa kukamatwa kwa wachungaji wake waliokuwapo kwa ajili ya kumlinda.
 
Hata hivyo, katika kwa upande mwingine, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema bunduki hiyo haina umiliki halali wa Gwajima wala wa wachungaji 15 waliokamatwa lakini baadaye jioni baada ya maelezo ya Gwajima, alitoa taarifa akisema bastola hiyo ni mali halali ya askofu huyo. Pia alisema kuhusu risasi 17 za bunduki aina ya Shortgun, Gwajima anamiliki bunduki ya aina hiyo lakini akasema uchunguzi kuhusu watu hao 15 unaendelea.

Kauli ya Gwajima
Akizungumza kwa shida akiwa amejishika tumbo, Gwajima alisemaalipopata taarifa za uvumi kwenye mitandao ya kijamii kuwa amefariki dunia, aliagiza wachungaji waende hospitalini kwa ajili ya kumlinda, lakini wakaishia mikononi mwa polisi wakidaiwa kutaka kumtorosha.
 
Alisema alihofia kuwapo kwa watu wabaya ambao wangeweza kumdhuru halafu wakasingizia kitendo hicho kufanywa na polisi kwa kuwa alipata tatizo akiwa mikononi mwao.
 
“Usiku wasiwasi ulizidi, huku kila mmoja akiwa hafahamu kwa nini ujumbe wa namna ile unasambazwa kwenye mitandao, msambazaji ni nani, ana nia gani, nikaamua kuwaagiza waniletee silaha yangu iliyokuwa kwenye begi ili likitokea lolote niweze kujilinda,” alisema Gwajima.
 
Alisema alishangaa kukamatwa wachungaji wake na kuchukua silaha iliyokuwa ndani ya begi na hadi jana hakuwa ameulizwa chochote kuhusu umiliki wa silaha hiyo.
 
“Kabla sijazungumza na waandishi kueleza ukweli wa kinachodaiwa kuwa nilitaka kutoroshwa na wachungaji wangu, nilitaka kuzungumza na ZCO (Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu), lakini hajaja, kadi ya ile silaha ninayo,” alisema Gwajima.
 
Alisema madai kuwa alitaka kutoroka ilihali polisi alikwenda mwenyewe akitokea Arusha baada ya kusoma katika vyombo vya habari kuwa anatafutwa.
 
Alifafanua kuwa hata alipofika polisi kwa ajili ya mahojiano hakuwa na shaka hata kidogo, lakini alishangaa kuona anaishiwa nguvu kila baada ya muda na alipoona kichwa kinamuuma, akawaomba wampeleke hospitali ili mambo mengine yafuate baadaye, kitu ambacho hakikufanyika kwa wakati.
 
Wasiwasi kwa polisi
Alisema alijaribu kuomba apelekwe hospitali mara kadhaa, lakini hakuna aliyekubaliana naye hadi alipopoteza fahamu na kupelekwa hospitali ya Polisi Kurasini.
 
“Hivi hata kama ni chombo cha usalama, nimepata matatizo nipo mikononi mwao, halafu nikubali kutibiwa katika hospitali yao, sikulitaka hilo na hata waliposema nikatibiwe Muhimbili pia sikutaka, ndiyo maana nilikuja hapa, sisemi moja kwa moja kama Polisi wanahusika lakini kuna vitu vinanitia shaka,” alisema Gwajima.
 
Alieleza kuwa anatilia shaka Jeshi la Polisi kutokana na kuwapo vitu vingi vinavyoashiria wana kitu kingine wanatafuta, kwani jana tulikuwa na hofu ya kuvamiwa, waliokuja kutuvamia ni wao, sikugombana na Pengo, nilikuwa namkemea kama kiongozi mwenzangu wa kiroho wao, wameligeuza ni kesi.
 
“Sijawahi kulitilia shaka Jeshi la Polisi lakini katika hili napata wasiwasi mwingi, sina ugomvi na Kardinali Pengo, nampenda, hajanilaumu, wala kunishtaki, nilikuwa namkemea katika masuala yetu ya mabaraza ya dini na siyo vinginevyo,” alisema Gwajima.
 
Gwajima pia alionyesha wasiwasi wake kwa kile kilichokuwa kinang’ang’aniwa na polisi kwenda kupekua nyumbani kwake kuwa hakikuwa kitu kizuri.
 
Kova alipinga
Wakati Gwajima akisema hayo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema bastola waliyokutwa nayo wafuasi wa Gwajima haimilikiwi kihalali.
 
“Tumegundua kuwa katika wale watu waliokuwa pale akiwamo Gwajima mwenyewe, (bastola) haikuwa  katika umiliki wao halali, kwa hiyo hapa kuna kesi ya kupatikana na silaha bila kibali.”
 
Akizungumzia tuhuma kwamba polisi walimpekua mke wa Gwajima, Kova alisema hakuna polisi waliofika nyumbani kwake kufanya upekuzi wowote na kama wakitaka kufanya hivyo watafuata taratibu maalumu za upekuzi.
 
Akijibu swali kuhusu mahali Gwajima alipotakiwa kutoroshewa, Kova alisema uchunguzi huo bado unaendelea na utakapomalizika wahusika watafikishwa mahakamani.
 
Pia alipoulizwa kama Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amemsamehe Gwajima, kwani polisi imng’ang’anie, Kova alisema;“amesema anamsamehe lakini haingilii mambo ya sheria.”
 
Kuhusu sababu za Gwajima kuzimia wakati akihojiwa, Kova alisema anayepaswa kuulizwa kwa nini alianguka wakati akihojiwa na polisi ni Gwajima mwenyewe.
 
“Siri za mahojiano huwa hazitolewi kabla ya ushahidi mahakamani, sababu ya kupata shock (mshtuko) atajua mwenyewe, kwa kuwa ukifanyiwa jambo ukafurahi au ukachukia wewe ndiyo unajua ilikuwaje, chochote kitakachotokea ukicheka, ukinuna, ukizimia, wewe ndiyo tukuulize ilikuwaje mpaka ukazimia kwa sababu hisia unazipata wewe,”alisema Kova.

Makonda amtembelea
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda ambaye alikuwa amemwandikia Gwajima barua akimwita ofisi kwake, jana mchana alimtembelea hospitalini hapo kwa ajili ya kumjulia hali kiongozi huyo lakini akasisitiza kuwa nia yake bado ipo palepale.
“Nilimtaka leo aripoti ofisini kwangu lakini kwa bahati mbaya anaugua na amelazwa. Nitakwenda kumuona ili nijue hali yake ikoje,” alisema Makonda kabla ya kufunga safari kwenda hospitali alikolazwa.
 
Alisema pia atataka kiongozi huyo wa kiroho amweleze anavyoelewa maana ya uhuru wa kuabudu unaoelezwa katika Katiba, usajili wa taasisi yake na katiba ya taasisi hiyo. 
  
“Mimi ni mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kinondoni. Niliagiza polisi wamkamate na baadaye wakimaliza kumhoji aje kwangu pia atahojiwa na jopo la watu 20,” alisema Makonda.

WATANO WANUSURIKA KIFO BAADA YA KUFUKIWA NA KIFUSI JIJINI MWANZA

Rashid Mkumba Hamis ambaye ni mmoja wa majeruhi aliyevunjika mguu.
Majeruhi katika tukio hilo wakihojiwa na wanahabari (hawapo pichani).
Vikosi vya uokoaji vikitoa msaada eneo la tukio.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Baraka Kunisaga akiongea na wanahabari baada ya ajali hiyo.
Eneo la msingi uliokuwa unajengwa na kuangukiwa na ukuta.
Wananchi wakishuhudia tukio hilo.
Vijana wakijaribu kuokoa baadhi ya mali zilizofukiwa na kifusi hicho.

Watu watano katika Wilaya ya Nyamagana jijini hapa wamenusurika kifo baada ya kuangukiwa na kifusi wakati wakiwa kwenye maandalizi ya kujenga jengo lililotegemewa kuwa na ghorofa saba, eneo la Nyerere Road, leo majira ya saa sita mchana.
Akizungumza na waandishi wa habari eneo la tukio, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Baraka Kunisaga amesema kuwa amesikitishwa na tukio hilo ambapo watu hao wameangukiwa na ukuta wakati wakijenga msingi wa jengo hilo na hii ni kutokana na kuwa na wakandarasi ambao hawajengi majengo kwa kiwango kinachotakiwa.
Katika hatua nyingine, Kunisaga amesema kuwa hali ya Watanzania kuwa wanapoteza uhai wao kila kukicha kutokana na kuangukiwa na vifusi, serikali haiwezi kukubaliana nayo hivyo amesitisha ujenzi wa jengo hilo.
Majeruhi waliokumbwa na tukio hilo wameongea na waandishi wa habari japo kwa taabu na kusema kuwa ukuta uliowaangukia ulikuwa umeunganishwa kama uzio hivyo wakati wakiendelea kuchimba msingi, uzio huo ulikuwa ukiendelea kutitia hivyo kusababisha kuporomoka na kuwaangukia.
Daktari wa zamu wodi ya dharura, Ernest Elisenguo amethibitisha kupokea majeruhi watano ambao wametokana na tukio la kuporomokewa na kifusi na kuwataja kuwa ni Ramadhan Hussein Nyarandu, Rashid Mkumba Hamis, Elias Bahati, Benson Agustino na Mtani ambapo watatu kati ya hao hali yao imeendelea vizuri na wameruhusiwa kwenda nyumbani ila wawili kati yao bado hali zao siyo nzuri na wataendelea kuwa chini ya uangalizi wa madaktari.
Majeruhi Rashid Mkumba Hamis, ameeleza kama ifuatavyo: "Mimi ni fundi na  nilikuwa natengeneza 'bezi' kwa ajili ya kushikilia nguzo za ghorofa wakati ninaendelea na kazi yangu nikaanza kusikia udongo ukiniangukia mgongoni, ghafla nikasikia matofali yananiangukia.

TIWA SAVAGE, FLAVOUR, DAVIDO WASHINDWA KUPIGA KURA NIGERIA

Tiwa Savage.
WAKATI wananchi wa Nigeria wakiwa katika zoezi la kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika juzi na jana, baadhi ya mastaa walishindwa kuhudhuria tukio hilo muhimu kutokana na majukumu mbalimbali.
 
Davido Adeleke.
Miongoni mwa mastaa hao ni mwanamuziki Davido Adeleke, aliyekuwa na shoo kwenye tamasha moja nchini Kenya hivyo hakuweza kupiga kura.
Flavour N'abania.
Mwanamuziki mwingine Flavour N'abania yeye alikuwa jijini London kwenye Tamasha la Dance Afrique. Huku mastaa wengine wakiwemo Tiwa Savage na P Square wakihudhuria tamasha hilo.
 
Toke Makinwa.
Mtangazaji Toke Makinwa yeye alikuwa nchini China wakati wa tukio hilo.
Mwanamuziki Wizkid ni staa mwingine ambaye hakupiga kura kutokana na shoo yake aliyokuwa nayo huko Dubai.
Wizkid.
Matokeo ya uchaguzi huo yanatarajiwa kutangazwa leo jioni ambapo Rais Goodluck Jonathan wa chama tawala cha PDP na Muhammud Buhari kutoka chama cha upinzani cha APC wanachuana vikali.

WATANGAZA NIA WAELEWE KUWA RAIS WA AWAMU YA TANO ATABEBA MIZIGO MIZITO

Rais Jakaya Mrisho Kikwete.
TUMSHUKURU Mungu kwa kutupa uhai, hatuna budi kumpongeza kwa kutupendelea kwani wengi kawachukua na sasa wametangulia mbele za haki.
Baada ya kusema hayo nianze mada ya leo kwa kusema kwamba  rais ajaye wa awamu ya tano hapa nchini atabeba mizigo mizito na kwa hali hiyo ni wazi kwamba atakuwa na wakati mgumu pengine kuliko watangulizi wake wanne.
Naamini kwamba wanasiasa wote waliotangaza nia ya kuwania ofisi hiyo kubwa kuliko zote nchini kiutendaji wanalitambua hilo, na wamejipima na kujiridhisha kuwa wako tayari kukabiliana na changamoto zinazotokana na jukumu hilo kubwa.
Mifano ni mingi ya jinsi atakavyokumbana na changamoto nyingi kama vile, itakuwa kazi ngumu kwake kuwafunga midomo Watanzania ambao kwa sasa wameelimika, wanajitambua pia wanafahamu haki zao, wanafahamu nini wanakitaka, nini wanakikosa na baadhi yao wanajua sheria za nchi.
Kiongozi ajaye, awe wa CCM au upinzani, hakuna shaka kazi yake ya kwanza itakuwa ni kuunda serikali,  jukumu ambalo pia siyo rahisi kama ilivyokuwa zamani pia atakuwa na jukumu la kutekeleza kazi zote zilizoanzishwa bila kukamilishwa na mtangulizi wake wa awamu ya nne, Rais Jakaya Kikwete.
Mbali ya ahadi za Kikwete, pia kuna masuala mengine mengi yamekuwa sugu na serikali yake imeshindwa kukabiliana nayo. Hayo ni pamoja na ujangili, rushwa, biashara ya dawa za kulevya, matumizi mabaya ya fedha za umma yaani ufisadi na mikataba mibovu inayoangamiza nchi.
Kuna matatizo mengi kama vile migogoro baina ya wakulima na wafugaji karibu maeneo mengi nchini na inasumbua wengi na kusababisha vifo katika baadhi ya sehemu kama yalivyoainishwa vizuri kwenye ripoti ya kamati teule ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyoongozwa na Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka.
Tatizo hili ni kubwa na zito linalohitaji ufumbuzi wa haraka. Ardhi, ni rasilimali kubwa, utajiri ambao nchi yetu imejaliwa kuwa nao, lakini imekuwa na mzozo hasa baada ya kuwaingiza wawekezaji ambao wanalalamikiwa na wananchi kutokana na kuingiza unyanyasaji.
Hapa nchini kwa sasa ardhi inauzwa hovyo wakati mwingine kwa kisingizio cha uwekezaji mkubwa au mdogo, dhuluma za kuwania viwanja au mashamba zinaongezeka, mijini na vijijini.
Ardhi, badala ya kuwa rasilimali, imegeuka chanzo, sababu kubwa ya ugomvi na maafa makubwa kwenye jamii zetu nyingi.
Matokeo ya maafa ya ardhi siyo madogo na haipo sababu ya kufumbiwa macho na kuachwa yapite, rais ajaye atakumbana na changamoto hii.
Mbali ya ardhi, kuna tatizo la mauaji ya Albino,wanawake kwa wanaume, hasa wenye umri mkubwa kutokana na ushirikina na  yamekuwa yakitokea Shinyanga, Mwanza au mikoa mingine ya kanda ya ziwa, hili ni tatizo ambalo rais ajaye lazima ahakikishe analimaliza.
Kuhusu watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), ni wengi, wanaendelea kuwindwa kama vile wao ni swala wanaowindwa kwa ajili ya kitoweo, kisa ni dhana potofu kwamba ngozi zao ni biashara nzuri, yenye kuleta utajiri. Upuuzi huu ni kama mfupa mgumu ambao serikali ya awamu ya nne imejaribu kuutafuna, lakini imeshindwa, sasa utahamishiwa kwa rais ajaye.
Pia, kuna tatizo la Katiba Mpya ambayo inasubiriwa kupigiwa kura ya maoni siku si nyingi, lakini mchakato huo ukikwama litakuwa ni jukumu jingine la rais ajaye.
Nchi yetu, ambayo imejitangaza kama kisiwa cha amani, utulivu na mshikamano katika miaka ya karibuni imeshuhudia pia matukio mengi ya mauaji na uhalifu unaongezeka, ujambazi na udini umeanza kushamiri. Ni jukumu la rais ajaye kuona tatizo hili linalotishia amani ya nchi yetu nzuri.
Ukabila pia una harufu yake, hivi sasa kuna ukanda, hili ni tatizo zito ambalo rais ajaye atatakiwa atoe kucha kuliangamiza.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.
USISITE KUTUACHIA UJUMBE WAKO HAPO CHINI

MFANYABIASHARA APIGWA...


MFANYABIASHARA wa Kisesa wilayani Magu, Mwanza, Nestory Andrew ameuawa kwa kupigwa risasi na majambazi usiku wa Februari 16, mwaka huu huku mke wake akishuhudia.
 
Mke wa mfanyabiashara huyo (kulia) akiwa na simanzi kubwa.
Imedaiwa kuwa kabla ya majambazi hao hawajafanya mauaji hayo, waliuteka Mtaa wa Kisesa kwani jirani na duka la mfanyabiashara huyo kulikuwa  na mafundi baiskeli ambao walizuiwa kupiga kelele na wauaji hao.
“Tukio hili lilitisha kwa sababu lilitokea mita kama 55 kutoka kituo cha polisi na hawakutoa msaada wowote,” alisema shuhuda mmoja.Akisumulia tukio hilo, mfanyakazi wa marehemu aitwaye Emmanuel Kulwa alisema bosi wake huyo alifika dukani saa mbili usiku ghafla wakati analifunga duka aliona mtu akiwa amevaa koti jeusi ambaye alipiga risasi kadhaa hewani, yeye akakimbia.
 
Nestory Andrew enzi za uhai wake.
“Baada ya hali kutulia nilirudi dukani nikakuta bosi wangu ameshauawa na mwili wake ukiwa umepelekwa Hospitali ya Mkoa  Sekeoture,” alisema.  Mke wa marehemu, Sara Limbu alisema alishuhudia tukio hilo la kuuawa mume wake baada ya kushuhudia risasi zikirindima eneo la tukio.
“Nilikimbia lakini nilirudi dukani baadaye na kumkuta mume wangu ameshafariki kwa kupigwa risasi mbili kifuani… ameniachia watoto sita. Mungu ailaze mahali pema peponi roho yake,” alisema mama huyo.
USISITE KUTUACHIA UJUMBE WAKO HAPO CHINI

MAITI YA MCHUNGAJI YAZUA TAFRANI

MAITI ya Mchungaji James Regnald Mhando  aliyefariki  Februari 18, mwaka huu imezua tafrani nzito kwa ndugu na jamaa baada ya kujulikana kuwa alikuwa na wake wawili ambapo mke mmoja alitaka mwili uagwe hospitali na upande wa pili ukitaka ukaagwe kwa mama yake marehemu.
 
Mchungaji James Regnald Mhando enzi za uhai wake.
Katika msiba huo ilibainika kuwa, mchungaji huyo (kanisa lake tunalihifadhi kwa sababu maalum), alikuwa na watoto sita kwa mama tofauti na wote walijitokeza katika mazishi ya baba yao.
Inadaiwa  kuwa Mchungaji Mhando alianza kuumwa Jumamosi ya Februari 14, mwaka huu lakini inadaiwa baadhi ya watoto na ndugu wengine hawakujulishwa hadi Jumanne ambapo inadaiwa alibebwa na gari la wagonjwa kutokea Morogoro hadi Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Jeneza la mchungaji James Regnald Mhando.
Habari zinasema ilipofika Jumatano saa tano usiku, mchungaji huyo aliaga dunia na mbali ya kuaga dunia, bado tukio hilo lilikuwa ni siri na ilidaiwa ilikuwa afanyiwe shughuli za mazishi kwa siri bila ya baadhi ya watoto wake wakubwa kujua.
Hata hivyo, habari za msiba huo zilizagaa haraka na kumfikia mke wa kwanza wa ndoa ambaye alikuwa nchini kwa ajili ya mapumziko kwani anafanya kazi nje ya nchi, hivyo ukoo ukaanza kutaarifiana.
Mchungaji Mhando alioa na kufunga ndoa Novemba 17,  1979  katika Kanisa la Anglikana la Mtakatifu Albano, jijini Dar es Salaam,  hata hivyo,  ilidaiwa kuwa mwaka 1985 mtumishi huyo wa Mungu aliamua kuondoka nyumbani alikokuwa akiishi na mkewe na kwenda kuishi na mwanamke mwingine ambaye inadaiwa kuwa alikuwa ni wa dhehebu lingine na wakafunga ndoa serikalini.
Habari zinadai kwamba mwanamke huyo alikuwa anaitwa Mwanaheri kabla ya kubadili dini na kuitwa Glory na wakafanikiwa kuzaa  watoto wawili, mmoja akapewa jina la Reginald Junior na mtoto mwingine anaitwa Sada au Doreen Mhando. Habari zinasema kabla ya kuondoka kwa mke wa kwanza, mchungaji huyo alizaa naye watoto wawili, wa kiume na wa kike....Askari akiwa eneo la tukio.
Hata hivyo, wakati wa msiba huo watoto wengine wawili walijitokeza nao wakidai kuwa ni baba yao, hali iliyozusha minong’ono kwa watu walioshangazwa na mwenendo wa marehemu.Akizungumza na Uwazi, mama mzazi wa mchungaji huyo aliyejitambulisha kwa jina la Dorofea Mhando (82) alisema kitendo kilichofanywa na mwanamke huyo ni kibaya kwani alimshawishi mwanaye kuisaliti familia yake.
“Mwanamke huyo mwingine alikuwa akiishi na mwanangu kwa siri kubwa  sana, kama vile marehemu hakuwa na familia na akawa anajifanya kuwa yeye ndiye mke wa kwanza, kitu ambacho ni cha uongo kwani marehemu alishaoa kanisani mwaka 1979.
“Marehemu baada ya kumpata mwanamke huyo alikuwa hashiriki shughuli nyingi za hapa nyumbani kwa kuhofia watu  watajua kuwa alikuwa na familia nyingine,  kitu ambacho kilinisikitisha,” alidai mama huyo.
Mwili wa marehemu ukiagwa.
Mama  huyo aliongeza  kuwa  maisha ya mchungaji huyo yalikuwa sehemu mbili, Morogoro na jijini Dar  es Salaam, alikuwa akifikia Mivinjeni kwenye ofisi ya shughuli zake.“Baada ya kupata taarifa ya msiba niliagiza mwili uletwe hapa Ukonga Majumba Sita ukitokea Muhimbili kwa ajili ya shughuli za kuagwa lakini mke mdogo akawa anapinga,” alidai mama huyo.
Hata hivyo, ilidaiwa kuwa mke mdogo alisisitiza kuwa baada ya kuandaa mwili wa marehemu uagwe Muhimbili, kisha  upelekwe katika Makabauri ya Kinondoni kwa mazishi.   Kulitokea mabishano ambapo mtoto mkubwa wa marehemu aliyefahamika kwa  jina Feda, alisema  baba yao hawezi  kuagwa kama mkimbizi kwani ana watoto, mke na mama yake mzazi, hivyo akaamuru mwili ukaagwe kwa bibi yake Ukonga Majumba Sita.
Habari zinadai kuwa mvutano huo ulifikishwa Polisi Kituo Kikuu ambapo lilifunguliwa jalada namba CD/ RB/ 2627/ 2015 ambao waliamuru shughuli za mazishi zisifanyike hadi muafaka upatikane.
Habari zinadai kikao kilifanyika polisi na muafaka ukapatikana kwamba mwili ukaagwe kwa mama yake mzazi Ukonga Majumba Sita.
Maofisa wa polisi walitoa askari wenye silaha chini ya kamanda wao aliyefahamika kwa jina moja la Manyama aliyeongozana na wana familia hao hadi Muhimbili kisha Ukonga, baadaye kwenye Makaburi ya Kinondoni ambapo mchungaji huyo alizikwa chini ya ulinzi.
USISITE KUTUACHIA UJUMBE WAKO HAPO CHINI

MAPIGANO TANGA, NGOMA BADO NZITO WALE MAGAIDI WATAJWA KUWA NI MAKOMANDO


YALE mapigano yaliyotikisa Mapango ya Amboni jijini Tanga kwa saa 48 kati ya watu wanaodaiwa na wananchi kuwa ni magaidi na majeshi ya ulinzi ya Tanzania bado ngoma nzito kufuatia baadhi ya wananchi kusema mengine mapya wanayoyajua kuhusu magaidi hao, Uwazi limechimba na kuchimbua.
Polisi wakipambana na magaidi hao.
Kwa mujibu wa baadhi ya wakazi wa Vijiji vya Mafuriko, Mikocheni, Majimoto, Kilomoni na Amboni yenyewe, wanaamini wahalifu hao ni makomandoo wazuri na waliishi kwenye mapango hayo wakijua siku wakivamiwa watapambana vikali.
KWA NINI MAKOMANDOO?
Mkazi mmoja wa Kijiji cha Majimoto alisema kwa jinsi watu hao walivyofanikiwa kutoweka katika mazingira tata huku wakiwa salama haingii akilini kwamba ni wapiganaji wenye mafunzo ya kawaida.
“Wakati risasi zinapigwa na serikali inatuambia tuchukue tahadhari kwa mtu tusiyemjua tumtolee taarifa tuliamini lazima watakamatwa hata kama si wote. Lakini tulipoambia hali imetulia lakini hajakamatwa hata mmoja tulishangaa sana,” alisema mkazi huyo akiomba asitaje jina lake.
KUMBE WAPO TANGU 2013!
Akizungumza na Uwazi, mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Amboni aliyejitambulisha kwa jina moja la Hassan alisema magaidi hao walipiga kambi kwenye mapango hayo tangu mwaka 2013.
“Sisi tulianza kuwaona mwaka 2013, sikumbuki mwezi. Lakini walionekana kama wachimba kokoto ndiyo maana walidumu kwa muda wote huo. Pale kuna sehemu watu wanachimba kokoto.”
ILIKUWA KAMA KWAO
“Naweza kusema walipatawala pale kwani ilikuwa kukicha, wengine walikuwa wakienda mjini wengine wanashinda palepale. Haikuwa rahisi kudhani ni magaidi,” alisema Hassan.
MAMBO MATATU YAIBUKA
Hata hivyo, wananchi hao ambao wanasema mpaka sasa hawana amani licha ya kuwepo kwa askari polisi kila kona kulinda, walisema kuna mambo matano ambayo polisi wamekaa kimya kuyatolea ufafanuzi.
Polisi wakiwa kwenye mapambano.
MOSI
“Sisi wakazi wa hapa palipotokea mapigano tunajiuliza, kwa nini polisi wameshindwa kutuambia ukweli wale ni akina nani badala ya kusema majambazi.
“Tangu lini majambazi wanapiga kambi mahali? Mimi ninavyojua, majambazi hufanya uhalifu na kurudi makwao. Tena naamini majambazi tunapanga nao nyumba tunazoishi au tunaishi nao mtaa mmoja au jirani,” alisema Almasi, mkazi wa Kijiji cha Kilomoni.
PILI
Wakazi hao walikwenda mbele zaidi na kusema kuwa, tangu Tanzania ipate uhuru haikuwahi kutokea majambazi wakapambana na polisi halafu polisi wakashindwa hadi kuita wanajeshi na wasikamatwe hata mmoja?
TATU
Wakazi hao waliendelea kudai kuwa, wamesikia tetesi zinazodai mwanajeshi aliyeuawa yalitokea makosa ya kiufundi kutoka kwa majeshi yetu lakini wanashangaa kimya cha polisi licha ya habari hizo kusambaa sana Amboni.
“Sisi tunasikia yule askari aliyeuawa ilitokana na makosa ya kiufundi kutoka kwa wenzake. Watu wengi hapa Mafuriko wanasema wamesikia hivyo, jeshi lingekanusha au kufafanua kama kuna ukweli,” alisema Mgaya, mkazi wa kijiji hicho.
WANANCHI MAPEMA NDANI
Baadhi ya wakazi walizungumza na Uwazi walisema licha ya kuwepo kwa polisi maeneo hayo lakini wanalazimika kuingia ndani mapema kwani kuna minong’ono kuwa, wahalifu hao wamejipanga kurudi na nguvu mpya baada ya kwenda kukutana na wenzao kwenye nchi jirani lakini jeshi la polisi mkoani hapa limekanusha uvumi huo na kuwataka wananchi waendelee na shunguli zao za kila siku.
Magaidi wa Al-Shabaab.
AL- SHABAAB ALIYEKIMBILIA KANISANI DAR...
Wakati huohuo, kijana mmoja aliyefahamika kwa jina moja la Shaban, mwenyeji wa Iringa ambaye alikiri kanisani kupewa mafunzo ya kigaidi nchini Afghanistan ili kwenda kutumika na Kundi la Al-Shabaab nchini Somalia ametoweka.
Akizungumza na Uwazi, Mchungaji wa Kanisa la Victoria lililopo External-Ubungo jijini Dar, John Said alisema Shaban alifika kanisani kwake mwaka jana na kutoa ushuhuda mzito kwamba yeye na Watanzania wenzake wawili walipelekwa Afghanistan kwa ajili ya mafunzo ya dini lakini walipofika wakakuta  ni mafunzo ya kigaidi.
“Shaban alitoweka, haji tena kanisani kama zamani. Alipokuja kwa mara ya kwanza alitoa ushuhuda huo mzito lakini baadaye akakata mguu,” alisema mchungaji huyo.
Katika ushuhuda wake, Shaban alisema kuwa, baada ya kufuzu walipelekwa Somalia kuungana na Al-Shabaab na kupigana na majeshi ya serikali ya nchi hiyo kwa kutumia silaha nzito lakini mwishowe aliamua kutoroka kurudi nchini.
 
Anasema: “Siku moja katika mapambano na majeshi ya serikali nilishuhudia wale wenzangu wawili wakiuawa kwa risasi, mimi nikatoroka katika eneo la mapigano kwa kuruka ukuta, ndiyo nikarudi hapa nyumbani Tanzania.”
UWAZI LAZUNGUMZA NA CHAGONJA
Baaada ya gazeti hili kuchimba yote hayo, lilimtafuta Kamishna wa Oparesheni ya Mafunzo Jeshi la Polisi Tanzania, Paul Chagonja ambapo alipopatikana na kumsimulia mambo yote mpaka ya Shaban, alisema:
“Mimi niko nje ya nchi kwa kazi ya kitaifa, wasiliana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga (Juma Ndaki) akupe maendeleo ya oparesheni yetu kule.
“Kuhusu huyo Shaban, nawasiliana na kitengo cha intelejensia sasa hivi ili atafutwe mpaka apatikane. Si yeye tu msako mkali unaendelea kwa umakini juu ya watu hao.”Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga alipotafutwa juzi, simu yake ilikuwa hewani lakini hali ya hewa ilikuwa mbaya hivyo kukosa usikivu.
USISITE KUTUACHIA UJUMBE WAKO HAPO CHINI
© Copyright BONGO HABARI
Back To Top