Mwenyekiti wa Bodi ya Tamasha la Sauti za Busara Simai Mohamed Saidi (wa pili kushoto) akizungumza.
Sehemu ya waandishi wa habari waliokuwa kwenye hafla hiyo.
Msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Ally Kiba (kulia) akielezea namna alivyojipanga kuburudisha kwenye tamasha hilo.
…Akipeana mkono na viongozi kwenye mkutano huo.
TAMASHA la Sauti za Busara linatarajiwa kufanyika Februari 12 hadi 15 mwaka huu huko Mji Mkongwe (Stone Town) Zanzibar.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, muandaaji wa tamasha hilo,
Dave Ojay Haashim, alisema madhumuni ya tamasha hilo ni kuwaweka
pamoja watu kutoka sehemu mbalimbali duniani ili kusherehekea muziki wa
Afrika chini ya anga la Zanzibar ambapo pia kutakuwa na wasanii wa
muziki wa kizazi kipya.
Tamasha hilo la 12 tangu kuanzishwa kwake limekuwa likifanyika kila
mwaka kwa kuhusisha wasanii kutoka pande mbalimbali za dunia ambao
huimba moja kwa moja jukwaani (live) kwa kutumia zana za muziki.
Naye Mkurugenzi wa Busara Promotion, Yusuf Mahmoud, alisema msimu huu
jumla ya wasanii na vikundi 680 viliomba kushiriki lakini baada ya
mchujo vilibaki vikundi 37 pekee.
Alisema kati yake 19 ni kutoka Tanzania na wengine wanatoka nchi
mbalimbali wakiwemo Blitz The Ambassador mwenye asili ya Ghana anayeishi
na kufanya kazi zake huko Brooklyn, Marekani.
Pia aliongeza kuwa kutakuwa na filamu maalum kwa ajili ya kumuenzi
Fatuma binti Baraka (Bi Kidude ) na kila mshiriki atatakiwa kuimba wimbo
wa kuhamasisha amani na watatu watakaoimba vizuri watapewa tuzo pamoja
na kitita cha Sh. milioni tisa.
USISITE KUTUACHIA UJUMBE WAKO HAPO CHINI