
Ni
Jumatatu nyingine nzuri tunapokutana katika uwanja wetu huu,
nakukaribisha kwa moyo mkunjufu ujumuike nami jamvini. Wiki iliyopita,
tulianza kujadili mada yetu kama inavyojieleza kwa kuhoji kwamba kipigo
kinaweza kusaidia kumnyoosha mwenzi wako?

Nianze kwa kukushukuru wewe ambaye ulituma ujumbe wako mfupi wa
maandishi (SMS) ukichangia mada hii. Maoni yako ni ya muhimu sana na
binafsi nimejifunza kitu kikubwa kutoka kwako.
WENGI WANACHUKIA SANA KUPIGWA Wanawake wengi
waliopo ndani ya ndoa na wale ambao bado hawajaingia kwenye ndoa,
inaonesha kwamba hakuna kitu wanachokichukia kama kupigwa na wenzi wao.
Wapo ambao wametoa ushuhuda wa jinsi walivyoamua kukatisha ndoa zao kwa
sababu ya vipigo na ubabe wa waume zao. Wengine wameeleza jinsi
walivyoamua kuwakimbia wenzi wao bila taarifa, kwa sababu ya kuchoshwa
na vipigo na manyanyaso ndani ya ndoa.
Nilichokibaini ni kwamba hakuna mtu anayependa kupigwa, kutukanwa au
kunyanyaswa na mwenzi wake kwa sababu tu ya mapenzi. Kama wewe ni
mwanaume na unataka kudumu kwenye ndoa yako, acha mara moja tabia ya
kumpiga mwenzi wako.
KIPIGO HUONGEZA KIBURI Kingine nilichokibaini, wanawake wengi hubadilika kitabia na kuwa wajeuri au wenye kiburi, kwa sababu ya kupigwa na wenzi wao.
“Kama nimefanya makosa, ni bora mume wangu anirekebishe kwa upole,
mimi ni mtu mzima naelewa. Lakini akijifanya kutumia nguvu kwa kunipiga
au kunitukana, kile alichonikataza nitakifanya maradufu,” huo ni ujumbe
kutoka kwa msomaji wangu, Mama Zahoro wa Unguja, Zanzibar.
Kingine
cha kujifunza hapa, kama wewe mwanaume kuna jambo hulipendi kuhusu mke
wako, kama kweli unataka abadilike, usitumie ubabe au ukali
kumrekebisha, zungumza naye kwa upole na bila shaka atakuelewa na
kubadilika.
KWA WANAOJITAKIA KUPIGWA
Katika msafara wa mamba, kenge pia wapo. Wakati wanawake dunia nzima
wakiunganisha nguvu kupinga ukatili dhidi yao, wapo wengine ambao kwa
makusudi kabisa wanajitakia kupigwa na waume au wenzi wao.
Wengi inakuwa ni kwa sababu ya malezi waliyolelewa au maisha
waliyowahi kupitia kabla ya kuwa na wenzi wao. Wanaume wengi waliotuma
meseji kwangu, walionesha kwamba huwa hawapendi kuwapiga wenzi wao
lakini wanalazimishwa kufanya hivyo kutokana na matendo ya wenzi wao.
UFANYEJE ILI USIPIGWE NA MUMEO? Jibu ni jepesi
sana, kitu cha kwanza; wanawake wanapaswa kujiepusha kujibizana na waume
au wenzi wao inapotokea kuna ugomvi. Badala ya kuanza kupeana mipasho
na mumeo utafikiri unasutana na shoga yako, ni vizuri kunyamaza hata
kama unaonewa mpaka hasira zenu ziishe kisha ndiyo mjadiliane kwa upole.
Pia epuka kufanya jambo ambalo mwenzi wako ameshakukataza zaidi ya
mara moja. Ukishajua mumeo hapendi ukae vibarazani kutwa ukipiga umbeya,
ni vizuri kujitahidi kujizuia kwani ukishindwa kufanya hivyo, huenda
ukaamsha hasira zake ukasababisha upigwe.
MWANAMKE HUPIGWA KWA UPANDE WA KHANGA Mwisho
ningependa kusisitiza nilichokieleza awali; tabia ya kupigana kwenye
mapenzi siyo nzuri kwa watu wanaopendana ambao wana ndoto za kuishi
pamoja kwa maisha yao yote. Kama ulikuwa na tabia hiyo, badilika,
jifunze kukabiliana na hasira zako na badala ya kumtwanga mkeo kwa
mangumi, muadhibu kwa kumfanyia kitu kizuri. Wahenga wanasema mwanamke
hapigwi bali kwa upande wa khanga mpya.
Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri.
USISITE KUTUACHIA UJUMBE WAKO HAPO CHINI.