Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

Benki Kukopesha Vijana Nchini......Wasomi Vyuo Vikuu kuzoa hadi milioni 50,Walio katika vikundi kuanzia na Milioni 200



KATIKA kuhakikisha vijana nchini wanajiajiri, Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) na Benki ya TIB, wameingia mkataba wa kuwawezesha kwa mikopo wajasiriamali vijana wanaomaliza vyuo vikuu nchini na vingine vya kati ili waweze kujiajiri.
Katika makubaliano hayo, TIB itatoa mikopo hiyo na kwa kuanzia kiasi cha Sh bilioni 1 kimetengwa kwa ajili ya mpango huo utakaoratibiwa na NEEC, ambayo itakuwa na jukumu la kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana hao, ikiwa ni pamoja na kusaidia namna ya kutayarisha andiko la miradi kwa nia ya kuomba mikopo.
 
 
Katika makubaliano hayo yenye lengo la kusaidia vijana kujikita katika miradi ya kilimo, uzalishaji, biashara na huduma, viwango vya mikopo vitakavyotolewa ni Sh zisizozidi milioni 200 kwa vikundi, washirika au ushirika, wakati kwa mjasiriamali mhitimu wa chuo kikuu, atakopesheka hadi Sh milioni 50.
 
Hata hivyo, watakaokopesheka ni wale watakaofaulu mafunzo ya kuwaandaa wajasiriamali, yatakayokuwa yakitolewa na NEEC. Waliosaini mkataba huo ni Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Peter Noni na Katibu Mtendaji wa NEEC, Dk Anacleth Kashuliza katika ofisi za benki hiyo jijini Dar es Salaam.
 
Akizungumza mara baada ya kusaini makubaliano hayo, Dk Kashuliza alisema vijana wengi wanamaliza vyuo vikuu, lakini wanakosa cha kufanya kutokana na tatizo kubwa la ajira.
 
Alisema Benki ya TIB na NEEC wamekubaliana kuanzisha mfuko wa kuwakopesha vijana, watakaoandika michanganuo ya miradi ambayo itakidhi vigezo vya kukopeshwa.
 
Alisema vijana wengi wanakabiliwa na changamoto ya kuandika miradi bora hivyo kupitia mradi huo ambao ni endelevu, watawapa elimu ya ujasiriamali pamoja na ujuzi wa kuandika michanganuo.
 
Kwa upande wake, Noni alisema vijana wengi wanakabiliwa na changamoto ya kupata dhamana kwa ajili ya mikopo, hivyo mfuko huo unaweza kuwa mkombozi kwao.
 
“Vijana watapata mikopo ya mitaji isiyohitaji dhamana ambayo watatakiwa kuirejesha ndani ya miaka mitatu, hivyo tunawahamasisha vijana wanaomaliza vyuo vikuu wachangamkie fursa hii,”alisema Noni.
 
Alisema vijana watakaokopeshwa, watakuwa kwenye vikundi vikundi na hata mmoja mmoja, kwani watakachoangalia si ukubwa au wingi wa watu, bali ni ubora wa mradi ulioombewa mkopo.
USISITE KUTUACHIA UJUMBE WAKO HAPO CHINI. 

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
© Copyright BONGO HABARI
Back To Top