Assalam
alaikum mpenzi msomaji wangu wa safu hii. Ni matumaini yangu kwamba kwa
uwezo wake Mwenyezi Mungu umzima bukheri wa afya na unaendelea vyema na
majukumu yako ya kila siku hasa katika kuyatimiza yale uliyopanga
kuyafanya kwa mwaka huu wa 2015.
Mpenzi
msomaji wangu, asilimia kubwa ya watu tuko katika ulimwengu wa mapenzi.
Wapo walio katika ndoa, wapo walio katika uchumba na kuna wale wenzangu
na mimi ambao bado wapo katika urafiki wa kawaida.
Niliodhamiria kuwazungumzia wiki hii ni wale walio na wapenzi
wababaishaji ambao wapo katika penzi lisilokuwa na nyuma wala mbele.
Yaani mtu anakuwa na mpenzi wake kwa muda mrefu lakini hawana malengo
yoyote zaidi ya kuliendesha penzi kisanii huku siku zikisogea na
kuzinguana kukiwa hakukauki.Huwa najiuliza, ni kupendana kwa aina gani huko ambako watu wanakaa tu na wala hawana mpango wa kuingia kwenye maisha ya ndoa?
Mimi nadhani ni vyema ukamweleza kabisa huyo mpenzi wako kwamba, sawa kakupenda lakini huu siyo wakati wa kuchezeana na kuachana, muulize yuko tayari siku moja uje kumuita mke/mume wako?
Ukiona anajiumauma na kutokupa majibu ya msingi, huna sababu ya kuendelea kuwa naye bali muache na uangalie utaratibu mwingine.
Tatizo walilonalo wengi ni kushindwa kujizuia pale mmoja anapotokea kumzimia mtu fulani, yaani anakuwa hasikii la kuambiwa na yuko tayari kwa lolote.
Sidhani kama una sababu ya kujiweka kwenye mazingira hayo. Kama wewe ni mwanaume ujue kabisa huu si wakati wa kuwa na demu wa kuzugia, kutumia naye wala kupitishia siku. Na kama wewe ni msichana, usikubali kugeuzwa mwanamke wa matanuzi tu, mchunguze vizuri huyo uliye naye.
Mpenzi msomaji wangu, mapenzi yamekuwa yakiwasumbua walio wengi katika maisha yao hadi wengine kufikia hatua ya kujilaumu kwa nini wamewapenda walionao sasa.
Wapo
ambao wamepoteza maisha kwa sababu tu ya mapenzi, wapo
waliochanganyikiwa, kuathirika kisaikolojia na wengine kuachishwa kazi
kwa sababu tu ya mapenzi. Kimsingi mapenzi ni hatari sana hasa pale
unapojikuta umedondokea sehemu ambayo hukustahili.
Lakini sasa, licha ya mapenzi kuleta matatizo kwa binadamu bado
tunaambiwa kwamba, utakuwa peke yako kwa muda f’lani tu wa maisha yako
lakini mwishowe utalazimika kutafuta mwenza ambaye utaishi naye katika
maisha ya mume na mke.Suala la kujiuliza ni kwamba, kama huyo unayempenda haonyeshi dalili za kukupenda kwa dhati, kuna ulazima gani wa kuendelea kung’ang’ania penzi lake? Mimi nasema, hakuna ulazima wa kuendelea kuwa naye bali unatakiwa kumuacha na kuangalia maisha yako. Kamwe usikubali kuwa mtumwa wa mapenzi. Usikubali kila siku mapenzi yakulize.
Nalazimika kusema hivyo kwa sababu mapenzi ya sasa yamejaa usanii wa hali ya juu kiasi kwamba ukifanya uchunguzi wa harakaharaka utabaini kuwa, wengi wanachezeana tu.Si ajabu huyo uliyenaye anaonesha kukupenda ile mbaya lakini amini usiamini inawezekana ni geresha tu na wala hana penzi la dhati moyoni mwake dhidi yako.
Ndiyo maana inashauriwa kuwa unapotokea kumpenda mtu fulani na yeye akakutamkia kwamba anakupenda, kuwa na imani kwamba ana penzi la dhati kwako kisha endelea kufanya utafiti katika kila analolifanya. Kama wewe ni mjanja utabaini tu kama umepata au umepatikana.
USISITE KUTUACHIA UJUMBE WAKO HAPO CHINI.
Post a Comment