Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

WEWE TIBAIJUKA! JEMBE LISILOLIMA LINA FAIDA GANI?

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.
WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, ameleta hoja ya kujadili ndani ya kaya yangu ‘alipojisheheresha’ kuwa yeye ni jembe kwa mkuu mwenzangu wa kaya yaani Rais Jakaya Kikwete, hii ni kauli ya hivi majuzi tu.

Ametumia msemo huo kama kifusi cha kufukia skendo iliyomkumba ya kujipatia fedha chafu kiasi cha shilingi Bil. 1.6, kutoka kwa mmoja wa watuhumiwa wa wizi wa fedha za Escrow.Mkuu wa Kaya najiuliza; katika akili nyepesi ujembe wake kwa rais wa nchi una uhusiano gani na fedha zisizokuwa na maelezo alizopokea kutoka kwa mmiliki wa Kampuni ya VIP Engineering ya James Rugemalira inayotuhumiwa kushiriki wizi wa zaidi ya bilioni 300?
Ni wazi; hoja iliyopo kwenye kaya ni yeye kujipatia fedha hizo, hata waliomtaka ajiuzulu waliangalia doa alilojiweka mbele ya jamii siyo mbele ya rais anayejikinga kwake kwamba anamuona ni jembe lake na kwamba hawezi kujiwajibisha.
Pengine Mkuu wa Kaya nawaza tofauti na profesa huyu, ndiyo maana naitafsiri dhambi kuwa kosa hata kama limetendwa na malaika mkuu. Msingi huu haunipi sababu ya kumuona mtuhumiwa huyu ni mkamilifu bila kujitakasa.
Na utakaso wake mbele ya Wananzengo uko wazi, ni kujiuzulu au kurudisha fedha alizopewa kiharamu, siyo kumgeuza rais kama kinga yake bila kujua kuwa anamchafua na kumshushia hadhi mbele ya jamii iliyompa madaraka ya kuongoza.
Naona siyo sawa; kwa waziri kusimama mbele ya hadhara na kutamka kuwa hawezi kujiuzulu kwa sababu yeye ni jembe na kuacha kuzungumzia tuhuma za msingi. Najiuliza, shabaha yake ilikuwa nini?  Je, ni kuiambia jamii mchezo wa kujigawia fedha rais anaufahamu?
Halafu hoja ya kuwa jembe la rais inamsaidia nini waziri huyu endapo atabaki kuwa si jembe kwa wananchi wenye mamlaka kwake na kwa rais anayemkimbilia kijinga? Mimi nafikiri Tibaijuka angelikuwa na kiburi zaidi kama angekuwa jembe la wananchi kwamba ameweza kuondoa migogoro ya ardhi, ameifanya ardhi kuwa mali ya wote tofauti na sasa ambapo matajiri ndiyo wanaomiliki ardhi kubwa kuliko maskini.
Nafikiri angekuwa jembe la wananchi kwa kuifanya ardhi kuwa mali kamili ya Watanzania badala ya kuwapendelea wageni kwa kuwapatia maeneo yenye rasilimali za nchi mfano migodi ya madini mbalimbali! Vinginevyo kujivunia jembe lisilolima hakuna faida yoyote.
Jambo jingine linalonifanya nione profesa huyu kama ni kiongozi wa tofauti, ni uthubutu wake wa kujitaja kuwa ni jembe. Najiuliza kinachomfanya awe wa tofauti na wengine ni kipi, yapo majembe kama Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa, Balozi Hamis Kagasheki, Emannuel Nchimbi, yaliwekwa kando kwa maslahi ya nchi, kwa nini asiwe yeye? Ni kiburi cha hali ya juu sana!
Nami kama Mkuu wa Kaya siwezi kuyafumbia macho mambo haya, lazima niyaweke wazi ili utumishi wangu kwa Wananzengo uwe na tija. Huwezi kuwa na mawaziri ambao wanaiona ikulu kama sehemu ya familia, wanamtazama rais kama mtu wa kumchezeachezea na kuwaona wananchi kama sanamu ambazo haziwezi kuongea.
Huu ni wakati wa dhambi kuchukuliwa kuwa ni kosa la kumhukumu mtu hata kama aliyelitenda amekuwa kigori kwa miaka 50. Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema, ikulu ni mahali patakatifu na aliyeko hapo anatakiwa kuwaambia rafiki zake wajue jambo hilo. Namshauri Rais Jakaya Kikwete asikubali kuwa sehemu ya wenye dhambi!
USISITE KUTUACHIA UJUMBE WAKO HAPO CHINI. 

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
© Copyright BONGO HABARI
Back To Top