SERIKALI wilayani Kiteto mkoani Manyara imewataka watu wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi kuacha kuambukiza wengine kwa makusudi kwa kufanya ngono zembe.
Akizungumza kwenye maadhimisho ya Ukimwi ambapo kiwilaya yalifanyika Mbeli kata ya Partimbo Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo Mainge Lemalali alisema sheria ipo na jambo hilo la kuambukiza kwa makusudi halikubaliki.
“Serikali hatutafumbia macho kuona watu wakisambaza virusi vya Ukimwi kwa makusudi tutawachukulia hatua mara moja na sheria zipo,” alisema Lemalali.
Akieleza hali ya maambukizo ya Ukimwi Ofisa Maendeleo ya Wilaya Joseph Mwaleba alisema maambukizi yanazidi kuongezeka kwa kuwa na asilimia 2.6 tofauti na mwaka jana ambapo yalikuwa asilimia 2.4.
Taarifa ya Ukimwi kiwilaya inaeleza kuwa akinamama waliopima mwaka 2013 -2014 walikuwa 11,646 na waliopatikana na VVU ni 165 sawa na asilimia 2.6.
Katika taarifa hiyo jumla ya vikundi 20 vya Waviu vyenye jumla ya watu 403 vimewezeshwa Sh 17,400,000 kwa ajili ya kuanzisha vikundi vya ujasiriamali ili viweze kujitegemea na kuondokana na utegemezi wa kipato.
USISITE KUTUACHIA UJUMBE WAKO HAPO CHINI.

Post a Comment