Dar es Salaam. Serikali
imesema imeyafungia mashindano ya Miss Tanzania baada ya waandaaji
kukiuka taratibu na kanuni huku pia yakitajwa kukithiri kwa rushwa ya
ngono na upendeleo.
Mashindano hayo yalifunguliwa mwaka 1994,
yamefungiwa kwa miaka miwili baada ya kuwapo kwa malalamiko kutoka kwa
wananchi na washiriki.
Kaimu Katibu Mtendaji wa Bazara la Sanaa Tanzania
(Basata), Godfrey Mngereza alisema jana kuwa Kamati ya Miss Tanzania
kupitia kampuni yake ya Lino Agency, imekiuka kanuni na taratibu
zinazoongoza mashindano hayo.
“Ni kweli kwamba tumeifungia Miss Tanzania kwa
miaka miwili, lakini haya si maazimio ya tathmini iliyofanyika mapema
mwezi huu, bali kulikuwa na vikao mbalimbali vilivyofanyika na si
kimoja, ni uamuzi mgumu ambao umekuja kutokana na sababu maalumu,”
alisema Mngereza.
Imeelezwa kuwa maazimio ya tathmini ya mashindano
hayo yaliyofanyika Desemba 12, mwaka huu hayakufikia uamuzi, bali vikao
mbalimbali vilivyoendeshwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na
Michezo kwa kushirikiana na Basata ndivyo vilivyofikia hatua hiyo ili
kutoa nafasi kwa waandaaji kujipanga upya.
Mngereza alisema baraza limegundua kuwa baadhi ya washiriki walichaguliwa kwa upendeleo bila ya kuwa na sifa zilizowekwa.
“Katika tathmini yalitolewa pia mambo mengi
ikiwamo warembo kudaiwa kutumiwa kingono hili ni suala lisilo jema.
Hakuna utaratibu maalumu wa kufanya usaili kwa warembo, hivyo wanaopita,
wanapita kwa njia zisizo halali tangu vitongoji mpaka ngazi ya
fainali,” alisema Mngereza.
Aliongeza kuwa tangu mwaka 2006 namna ushindi
unavyopatikana umekuwa ukilalamikiwa, kwamba wanapewa watoto wa viongozi
serikalini na wenye uwezo kifedha.
“Kwa mfano mwaka huu walikuwa wakitetea majibu
yasiyo sahihi, hatimaye kamati ikasema kwamba cheti cha Sitti Mtemvu
walichotuletea ni sahihi, sasa ninajiuliza wewe unawezaje kusema cheti
ni sahihi huku hujadhibitisha,” alisema na kuongeza:
“Ndicho kilichojitokeza katika tathmini, alitakiwa
kuwasiliana na mamlaka husika, kama ni mtihani kuna Necta na kama cheti
cha kuzaliwa kuna Rita, kwa hiyo wasingengoja wadau wapige kelele,
waandishi wa habari wamkalie kooni kwa kulisimamia hili ndipo
utekelezaji ufanyike.”
Lundenga: Sina taarifa na kifungo
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Lino Agency
International, Hashim Lundenga aliliambia gazeti hili kuwa hajapokea
barua yoyote kutoka wizarani wala Basata, huku akilaumu taarifa
zilizotolewa kabla hajapewa barua rasmi.
“Sijapokea barua yoyote kutoka Basata na wala sijaitwa huko
tangu ifanyike tathmini Desemba 12 ambapo tuliambiwa kwamba kamati
ingepewa maazimio, lakini kabla ya kukabidhiwa barua na vitu vingine
tunaona kwenye vyombo vya habari kwamba tumefungiwa,” alisema Lundenga
na kuongeza:
“Tumefanya Miss Tanzania kwa miaka 21 na
hatujawahi kuingia katika misukosuko kama ilivyokuwa kwa mwaka huu,
unajua bwana wakati mwingine akufukuzaye hakwambii toka, hivi vitu
vinakwenda kwa utaratibu na siyo hivyo.”
Itaendelea kesho
USISITE KUTUACHIA UJUMBE WAKO HAPO CHINI.
Post a Comment