MBUNGE wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), kwa mara ya kwanza amefunguka na kusema ana nia ya kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 iwapo chama chake kitaridhia.
Ametoa
kauli hiyo ikiwa ni miaka miwili tangu Mbunge wa Kigoma Kaskazini,
Zitto Kabwe (Chadema), alipojitokeza hadharani akisema kwamba hatawania
tena ubunge katika jimbo hilo katika Uchaguzi Mkuu ujao na badala yake
atajitosa kwenye urais.
Hata
hivyo, kauli hiyo ya Zitto ilisababisha mvutano mkubwa kati yake na
viongozi wenzake ndani ya chama hicho, huku mmoja wa waasisi wake, Edwin
Mtei, akipinga uamuzi wa mwanasiasa huyo na akidai hakuutoa wakati
mwafaka. Mtei alisema hatua ya Zitto kutangaza kutaka kuwania urais wa
mwaka 2015 haikuwa na shida kwa sababu alionyesha hisia zake lakini
alikuwa ikitengeneza mzozo ndani ya chama.
Mwanasiasa huyo alimshauri Zitto kuhakikisha anakiunganisha chama na si kukigawa na kukivuruga.
Akizungumza
katika mahojiano maalumu na MTANZANIA mwishoni mwa wiki iliyopita,
Lissu alisema ana uzoefu wa uongozi hivyo yuko tayari kuwania urais
iwapo vikao vya chama chake vitaridhia.
“Mimi
ni Mwenyekiti wa Movement For Change Kanda ya Kati, pia ni mjumbe wa
Kamati Kuu ya chama, vile vile ni mwanasheria mkuu wa chama.
“Kwa kuwa nina uzoefu mzuri wa uongozi, nitakuwa tayari kugombea urais iwapo vikao vya chama vitaamua,” alisema Lissu.
Huku
akitabasamu, Lissu alimtania mwandishi wa habari hizi na hata kumhoji
kama kauli yake itapewa nafasi ya juu katika gazeti lake.
“Tena hiyo kesho inaweza kuwa headline eeh!” alisema Lissu huku akitabasamu.
Lissu
alisema kazi ya ubunge imempa fursa ya kuwatumikia wananchi katika
kutatua matatizo yao, kuibua hoja na masuala yanayolitatiza taifa.
Alisema
katika kipindi chote cha ubunge, pia alitumia utaalamu wa sheria
kuboresha mfumo mzima wa ubunge ikiwa ni pamoja na kulifanya Bunge la 10
la Jamhuri ya Muungano kuwa bora na machachari kuliko Bunge la Tisa.
Lissu,
ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Sheria na Katiba, alisema hana hofu na
watu wanaotaka kugombea ubunge katika Jimbo la Singida Mashariki ambako
aliwakaribisha kwa mikono miwili.
“Sina wasiwasi. Ninawakaribisha sana Singida Mashariki waje tupambane kwenye uchaguzi mkuu unaokuja,” alisema.
Akizungumzia uamuzi huo wa Lissu, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema kauli ya mwanasiasa huyo haina tatizo.
“Sioni tatizo la Lissu kutangaza nia kwa sababu kila mtu anao uhuru wa kutamka na kugombea urais,” alisema Mbowe.
Post a Comment