Mkurugenzi wa Kituo cha Vipaji Tanzania (THT), Ruge Mutahaba.
Awataka wanaoanzisha vita dhidi yake wasihusishe wasanii wanaotokea THT
Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Kituo cha Vipaji
Tanzania (THT), Ruge Mutahaba amesema taasisi hiyo ni sehemu ya mikakati
ya kukuza vipaji vya wasanii, na kamwe wanafunzi wake hawahusiani na
mambo binafsi yanayowahusu viongozi.
Ruge aliyasema hayo wakati wa hafla fupi ya
kumuaga msanii Amini Mwinyimkuu aliyekuzwa na kituo hicho kwa muda wa
miaka tisa iliyofanyika makao makuu ya THT juzi jioni.
Alisema chuo hicho kinachochukua vijana zaidi 100
kila mwaka, kinatoa mchango mkubwa kwa jamii na hivyo huharibu taswira
yake wakati mambo binafsi yanapoingizwa na kuwahusisha moja kwa moja
wasanii wanaotokea THT.
“Inapofika mahali kuna vurugu, vita ambazo
zinamhusu mkurugenzi, kwa bahati mbaya wasanii kutoka katika lebo hii
huingizwa katika mikasa ya ajabu na hilo huwaumiza sana. Mara nyingi
wanateseka bila ya kuhusika kwa namna yoyote ile na hiyo imetokea siyo
mara moja ama mbili. Acheni hiki kitu hakiwahusu hawa. Wanifuateni mimi
mwenyewe,” alisema Ruge.
Ruge, ambaye pia ni mkurugenzi wa vipindi na
uzalishaji Clouds Media Group, alisema amekuwa akipambana na hali hiyo,
lakini inapofikia hatua fulani, wasanii wakajituma na kuweza kupata lebo
nyingine, inakuwa ahueni kwa THT kuendelea kuzalisha vijana zaidi.
“Ninafurahi hasa ninapoona msanii akaweza kusimama
na akashinda majaribu yote haya na mpaka akapata lebo mpya na kuanza
kupiga hatua ya kujitegemea lazima nimshukuru Mungu, na wote ambao
walisaidia. Nia yetu ni kuwapa daraja na nilishawaambia kwamba itafikia
hatua nitawaachia wakajitegemee,” alisema.
Alisema lebo hiyo inafahamika kwamba ni familia,
hivyo ikihusishwa na mtu mmoja inaathiri wengi, kwani wapo wanaotumia
lebo hiyo kutengeneza kazi mbalimbali kwa ajili ya kuendeleza muziki
Tanzania.
“Akina Davido, Diamond wanarekodi hapa. Hakuna
anayelipa hii ni sehemu ya mafunzo, wengine wanajua kwamba hii ni sehemu
ya wanafunzi, lakini hii ni kwa ajili ya wasanii wote, ni nyumba ya
vipaji. Ninachotaka kuona ni watu wanabadilisha mtazamo wao kuhusu THT
ibaki kuwa kama shule,” alisema Ruge.
“Amini endelea kupenda kile unachopenda kufanya.
Linah naye amekwenda kwenye lebo nyingine ya No Fake Zone, Amini na wewe
unakwenda DME Company Limited. Barnaba naye yupo mbioni. Siyo kwamba
tunafukuza waliopo, ila tunataka kuendelea kuzalisha vipaji vipya,”
alisema.
THT imemuaga rasmi Amini ambaye ni miongoni mwa wasanii wanaotokea THT baada ya kuishi kwa zaidi ya miaka tisa.
Post a Comment