Dodoma. Waziri wa Maji, Profesa Jumanne
Maghembe na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk
Binilith Mahenge, jana walituhumiwa kutumia vibaya nafasi zao kwa kuweka
fedha nyingi za miradi ya maji katika maeneo wanakotoka, huku sehemu
zenye matatizo ya huduma hiyo zikitengewa fedha kiduchu.
Ilielezwa bungeni jana kuwa Profesa
Maghembe ambaye ni Mbunge wa Mwanga, Kilimanjaro, wizara yake imetenga
Sh1.4 bilioni kwa ajili ya miradi ya maji, ambazo ni zaidi ya mara saba
ya Sh190 milioni zilizotengwa kwa ajili hiyo katika Wilaya ya Ikungi,
Singida.
Akichangia Bajeti ya Wizara ya Maji
jana, Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu alihoji kile
alichokiita upendeleo wa wazi katika ugawaji wa fedha za maji, unaoipa
kipaumbele baadhi ya mikoa wanakotoka mawaziri.
Pia aliitaja Wilaya ya Makete, Njombe
anakotokea Dk Mahenge ambaye amewahi kuwa Naibu Waziri wa Maji kuwa
imetengewa Sh1.9 bilioni na kusema: “Upendeleo wa aina hii haufai kwa
sababu utaleta matatizo na siyo haki hata kidogo.”
“Profesa Maghembe atueleze sababu za
kutenga bajeti hii kwa upendeleo, huku mikoa isiyokuwa na vyanzo vya
maji, mito ya kudumu na mabwawa ya maana imepewa bajeti kidogo
ikilinganishwa na ile yenye mifumo mizuri ya maji,” alisema Lissu.
Alisema licha ya Profesa Maghembe katika
hotuba yake kutaja mikoa ya Dodoma, Singida, Simiyu na Shinyanga kuwa
inakabiliwa na upungufu wa maji, imetengewa kiasi kidogo cha fedha, huku
mikoa inayopata mvua za kutosha na vyanzo vya uhakika vya maji
ikitengewa mabilioni ya fedha.
“Dodoma imetengewa Sh7.2 bilioni,
Singida Sh3.2 bilioni, Shinyanga Sh3.2 bilioni na Simiyu Sh2.8 bilioni,
wakati mikoa yenye vyanzo vya maji na mvua za kutosha imetengewa fedha
nyingi; mfano ni Tanga Sh10.7 bilioni, Kilimanjaro Sh6.3 bilioni, Mbeya
Sh9.2 bilioni na Mtwara Sh7.5 bilioni,” alisema.
Lissu alisema hali hiyo inaweza
kutafsiriwa kuwa mawaziri hao wanatumia mamlaka yao kujipendelea na
kuhoji kama huo ndiyo utaratibu wa Serikali ya CCM... “Kama utaratibu wa
mgawanyo wa fedha ndiyo huu sisi tunaotoka mikoa yenye ukame tutapataje
maji?”
Jana Profesa Maghembe aliendelea kuwa
katika wakati mgumu, baada ya kuandamwa na Mbunge wa Ubungo (Chadema),
John Mnyika ambaye alimwita kuwa ni mzigo kutokana na kutokutolewa kwa
fedha za miradi ya maji.
Mnyika alionyesha kushangazwa na wabunge
wenzake kuunga mkono bajeti ya wizara hiyo, licha ya kuwa ndogo na
fedha za miradi zimekuwa hazitolewi kama inavyotakiwa.
“Kwa kufanya hivi sidhani kama
tunamsaidia Profesa Maghembe ambaye ni CCM. Fedha zilizotengwa mwaka
jana kuisaidia wizara hii hazijatoka na za bajeti hii hazitatoka kwa
kiwango cha kuwezesha utekelezaji. Namna bora ya kumsaidia ili viongozi
wa CCM wasiendelee kumwita mzigo ni kuikataa bajeti hii ili Serikali
irudi mezani na kujiuliza.”
Post a Comment