Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

UNYAGO WA KICHINA NA WANAWAKE WA KISASA, BALAA TUPU

Kama kawa nimerudi tena nikiwa na hasira kama faru aliyejeruhiwa, nakuuliza hivi kwa nini lakini? Tabia hiyo ndo uliyofundwa mkoleni? Jamani kabila lako si ndiyo  mafundi wa kuwaweka ndani wanawari, mnafundishwa nini, kuogea machicha ya nazi?
Loh! Mwana mbona unatia aibu kabila lako? Unamuaibisha somo yako na kuonekana mafunzo yote aliyokupa ulipokuwa mkoleni kazi bure.Jamani hivi ewe mwana, kutulia kwako kuna nini? Nyumba yako ina moto kila kukicha kiguu na njia na kusababisha kulichafua kabila lako na kuonekana kama mtu akioa kabila hilo kauoa moto. Sifa nyingine mbaya kuongea kama umemeza kanda, jamani nani aliyekufunda mkoleni kwamba mwanamke anazungumza kuliko mwanaume? Wewe mtoto wa kike umeolewa lakini mtu akikuangalia ulivyo anajua wewe ni changudoa, jamani mbona aibu, natamani kulia na kujiuliza hawa masomo wa sasa ni wakosa haya wasiojua nini maana ya mafunzo ya kumuandaa mwanamke.
Haya hukushika mafunzo ya kuishi na mwanaume hata uanamke wako huujui?
Mungu wangu! Yote tisa kumi ingia kwenye kicheni pati za sasa uozo mtupu, mwanzo zilivyoanza kwa kweli zilikuwa zikizingatia maadili kwa mtu aliye ndani ya ndoa yake kumfunda mwari japo nayo haikutosha kwa vile mafunzo ya kumuandaa binti huchukua zaidi ya mwezi mmoja.
Lakini leo inatisha, mpaka kuna kipindi huwa namuomba Mungu atusamehe kwa vile uchafu tunaofanya kwenye kicheni pati zetu matokeo yake ndoa zimekuwa mnaoana asubuhi mnaachana jioni.Sasa hivi umekuwa unyago wa Kichina kila mtu ana ruksa kuingia na kusema, na anayeelezwa yanaingilia kulia yanatokea kushoto akitoka ana yake basi ndani ya nyumba balaa tupu. Jamani hii kali inafikia hatua eti watu wanamchukua shoga (mwanaume si riziki) kwenda kumfunda mwari, jamani hii ni laana au nini. Mbona tumekuwa tunautia najisi uanamke wetu.
Leo hii wanawake tumeshindwa kufundana wenyewe tunawaita mashoga. Hii si laana na kutufanya kila kukicha wanawake tupoteze maadili na nyumba zetu kuwa kama kaa la moto hazikaliki.
Hivi jamani huyo shoga anajua usafi wa mwanamke akiwa katika siku zake afanye nini? Kuna wanawake wengi leo hii hawajui wakiwa katika siku zao wafanye nini na uchafu wao wauhifadhi vipi. Sasa hivi kicheni pati imekuwa ndiyo sehemu ya watu kukaa utupu na kutukana kila neno baya kusemwa ndani ya kicheni pati.Kingine kinachochekesha ni pale unampa mtu asiyeijua ndoa kumfunda anayetaka kuolewa. Mtaani ana sifa mbaya kishata mtaa, yeye tambara la deki, yeye jamvi la wageni ndiyo unampa kipaza sauti amfunde muolewaji. Jamani eeh!  Usiyoionja huijui ladha yake, mwenye ndoa ndiye atakueleza ndoa ipo vipi.
Mwari ndoa ina mambo mengi ndoa bila uvumilivu hukai, haya huyo kishata mtaa atayajuaje kama siyo kuyasema asiyoyajua. Kuna ndoa leo hii ukiambiwa ina miaka hamsini lakini ndani yake kuna kila aina ya taabu na raha, maumivu na furaha lakini yote walivumiliana na kuwafanya wawe mfano bora wa kuigwa. Hebu mtu huyo asimame au akufunde kwa wakati wake utagundua vitu vingi ambavyo vitakufanya uijue ndoa kiundani. Jamani ukiingia ndani ya ndoa unatakiwa utulie ubadilike uonekane kweli mke wa mtu kwa tabia na mavazi yako. Tulia nyumbani msikilize mumeo toka kwa amri si kila kitu mtaani unakitaka wewe, sherehe gani ipite bila kwenda na kushona sare. Ukinyimwa unadai talaka, shuuutu mwari ndoa mbaya ukiwa nayo ikikutoka utaitafuta mpaka kwa waganga.
Hebu basi tutumie mafunzo ya unyagoni tuzilinde nyumba zetu pia tuufahamu uanamke wetu ili tufute ile dhana mbaya wanawake mwalimu wetu kipofu, kwa mambo yanayoendelea naona mwalimu wetu hana kichwa kabisa. Yangu nimemaliza.

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
© Copyright BONGO HABARI
Back To Top