Licha ya Rais Jakaya Kikwete kutoa ufafanuzi
wa sakata la uchotaji fedha kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa
Benki Kuu na kutangaza kuchukua hatua dhidi ya baadhi ya viongozi na
watendaji, nchi wahisani wamesema bado suala hilo linawachanganya na
wanasubiri tamko la Serikali.
Nchi hizo, ambazo
zilizuia takriban Sh1 trilioni za ufadhili na kuchangia nakisi ya bajeti
ya Serikali, juzi zilikiri kuanza kuruhusu sehemu ya fedha hizo baada
ya baadhi ya maazimio ya Bunge la Jamhuri ya Muungano kuanza
kutekelezwa, ikiwa ni pamoja na kumvua uwaziri Anna Tibaijuka,
kumsimamisha kazi Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim
Maswi na kumuweka kiporo waziri wake, Sospeter Muhongo na kusababisha
Jaji Fredrick Werema kujivua wadhifa wake wa Mwanasheria Mkuu.
Tayari Rais Jakaya Kikwete ameshaeleza kuwa fedha hizo hazikuwa za Serikali.
Hata
hivyo, akizungumza na Mwandishi wetu juzi, Balozi wa Jumuiya ya Ulaya
nchini, Timothy Clarke alisema kwamba Serikali imeonyesha jitihada za
mwanzo, lakini wanasubiri kuona hatua kali zaidi zikichukuliwa pamoja na
kuja na kauli moja kuhusu fedha hizo.
Alisema
alichobaini ni kwamba wananchi wengi wanataka kujua hatima ya sakata
hilo ndiyo maana walitumia vyombo vya habari kufanya mijadala mbalimbali
kuzungumzia wizi wa fedha za escrow ambazo haijawekwa wazi kuwa ni za
umma ama ni za Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL.
Balozi
Clarke alisema kwa upande mwingine, Serikali imeonyesha tabia ya kusita
katika kutoa uamuzi kwenye suala hilo na kwamba walitarajia kusikia
tamko kali pamoja na tamko la kuzuia vitendo hivyo visiendelee.
Alieleza
kuwa hadi sasa nchi nyingi hazijaipa fedha Tanzania kama zilivyokuwa
zinatarajiwa kwa kuwa bado zinasubiri hatua zaidi kutoka serikalini.
Sakata
la escrow, lililohusu uchotwaji wa Sh306 bilioni kutoka akaunti hiyo,
lilisababisha Taasisi ya Marekani ya MCC inayosaidia nchi zinazoendelea,
kutangaza kusitisha kusaini mkataba wa awamu ya mpango huo wa maendeleo
kuishinikiza Serikali kushughulikia kashfa hiyo.
Bodi
ya Wakurugenzi ya MCC ilitoa taarifa yake Desemba 16 mwaka jana,
ikieleza kuwa mkutano wake wa Desemba 10 mwaka huu uliruhusu kuanza
maandalizi ya kusaini mkataba wa awamu ya pili ya mpango huo, lakini
ulielezea hofu na masikitiko kuhusu hali ya rushwa inavyoendelea
Tanzania.
Fedha ambazo Tanzania ilipaswa kupata kupitia
mradi huo wa MCC awamu ya pili ni Dola 450 milioni ambazo ni sawa na
Sh765 bilioni.
“Japokuwa bodi ilipiga kura kwa dhati
kabisa ya kuiruhusu Tanzania iendelee na maandalizi kwa ajili ya mkataba
wa pili, inaihimiza Serikali ya Tanzania kuchukua hatua thabiti na
mahsusi za kukabiliana na rushwa kama sharti la msingi kwa bodi hiyo
kufanya uamuzi wa mwisho wa kuidhinisha mkataba huo.
Sakata la escrow lilihusisha fedha zilizokuwa zimehifadhiwa
Benki Kuu wakati kesi baina ya Shirika la Umeme (Tanesco) na IPTL
zikipambana mahakamani. Pande hizo mbili zilikubaliana kufungua akaunti
hiyo ya escrow ili kutunza fedha ambazo Tanesco ilitakiwa iilipe IPTL
ikiwa ni malipo ya ununuzi umeme.
Hata hivyo, akaunti
hiyo ilifungwa kwa njia ambayo ilitia shaka na fedha hizo kulipwa kwa
Kampuni ya Pan African Power Solution Limited (PAP) ambayo ni mmiliki
mpya wa IPTL na kukiwa na mambo mengi yaliyotakiwa kufanyiwa kazi kabla
ya malipo hayo, ikiwa ni pamoja na kulipwa kwa kodi ya Serikali na
kukokotoa upya gharama ambazo Tanesco ilitakiwa ilipe baada ya mzozo wao
kuisha mahakamani.
Pia, fedha hizo zililipwa kwa James
Rugemarila aliyekuwa akimiliki asilimia 30 ya hisa za IPTL na ambaye
baada ya malipo alitoa mgawo wa fedha kwa watu kadhaa, wakiwamo viongozi
wa dini, watumishi wa umma, mawaziri na Mwanasheria Mkuu wa zamani,
hali iliyotia shaka zaidi kuhusu fedha hizo.
Tayari
Tibaijuka amewajibishwa baada ya kupokea Sh1.6 bilioni kutoka kwa
Rugemarila, hali kadhalika Andrew Chenge, ambaye pia alipewa Sh1.6
bilioni na William Ngeleja (40.4 milioni) wametakiwa kuondolewa kwenye
uenyekiti wa Kamati za Bunge sambamba na Victor Mwambalaswa na Fredrick
Werema, akitangaza kujiuzulu wadhifa wake wa Mwanasheria Mkuu kwa
maelezo kuwa ushauri wake haukueleweka na kuzua tafrani.
Naye
Balozi wa Uingereza nchini, Dianna Melrose alisema mazungumzo na
Serikali bado yanaendelea na kwamba hali itaendelea kuwa nzuri kadri
mazungumzo yanavyoendelea.
“Bado tunaendelea na mazungumzo na Serikali huku tukisubiri tamko,” alisema Dianna.
Taarifa
iliyotolewa na Mwenyekiti wa mfuko wa maendeleo wa wahisani, Sinikka
Antila juzi ilieleza kuwa mpaka sasa zimekwishatolewa Dola 84 milioni
sawa na asilimia 15 ya msaada wote kwenye bajeti ya 2014/2015.
Kwa
upande wake, kiongozi wa mabalozi waliopo nchini, Juma Mpango alisema
Tanzania imeonyesha jitihada katika kuleta maendeleo na kupambana na
rushwa.
Balozi Mpango, ambaye pia ni Balozi wa Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), alisema Serikali imeonyesha nia ya
kupunguza matukio ya kifisadi.
“Tumefuatilia namna
ambavyo Tanzania imefanya vita kubwa kuondoa madhara ya ufisadi katika
nchi, ilikuwa kubwa sana,” alisema Balozi Mpango.
Nchi
na wadau wanaochangia kwenye bajeti na sekta nyingine za maendeleo ni;
Canada, Denmark, Finland, Ujerumani, Ireland, Japan, Sweden, Uingereza,
Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Jumuiya ya Ulaya (EU) na Benki ya
Dunia (WB).
Post a Comment