Profesa Sospeter Muhongo.
Kwako mheshimiwa, Profesa Sospeter Muhongo.Nilizungumza nawe kupitia ukurasa huuhuu mara ya kwanza, nikakueleza ujumbe wangu ambao najua hukuupokea vizuri japo lengo langu lilikuwa ni kukusaidia uepukane na hii kadhia inayoendelea kukukuta sasa. Kwa mara nyingine nataka kuzungumza nawe kwani naamini wewe si sikio la kufa.
Najua unapitia kipindi kigumu sana tangu kuibuka kwa sakata la mabilioni ya Akaunti ya Tegeta Escrow, hata usingizi wako sidhani kama unaupata vizuri kama ilivyokuwa kabla ya kuibuka kwa skendo hiyo.
Mheshimiwa, mimi sikuzaliwa Juni 25, 1954 huko Musoma kama wewe. Mimi si msomi mwenye ‘CV’ ya nguvu na kubobea kwenye sayansi ya miamba na madini kama wewe. Sijawahi kufundisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wala sijawahi kujiunga na chama au taasisi yoyote ya kisayansi duniani kama wewe.
Sijawahi kufanya kazi kama mtafiti kwenye Chuo Kikuu cha Mainz, Ujerumani kama wewe wala mimi sijawahi kuteuliwa kuwania ukurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco). Mimi si mbunge wa kuteuliwa wala waziri mwenye dhamana kubwa kama wewe.
Mimi ni mlalahoi tu, nisiye na mbele wala nyuma, niponipo tu mjini naganga njaa kuhakikisha mkono unaenda kinywani.Hata hivyo, pamoja na ulalahoi wangu, narudia kukwambia kwamba ningekuwa mimi kwenye nafasi yako, tayari ningeshakuwa nimesoma alama za nyakati, nisingekubali kuwekwa kiporo kwa kipindi chote hicho. Ningeshachukua hatua ili kuepusha kelele hizi zinazoendelea kupigwa kila kukicha na kila sehemu, chanzo kikiwa ni wewe.
Ningekuwa wewe, nakuapia kwa jina la Mungu, tayari ningeshang’atuka madarakani kwa sababu huo ndiyo uwajibikaji.Nisingesubiri uamuzi wa mamlaka iliyoniteua kutengua uteuzi wangu, tayari ningeshajifanyia ‘soul searching’ na kujua ni kwa namna gani nimeigharimu nchi hii maskini, ningekuwa na huruma na ndugu zangu wanaoteseka kwa umaskini uliokithiri wakati mimi nikiendelea kutanua na magari ya kifahari ya serikali na kula posho kibao wakati najua kabisa kazi niliyopewa inalalamikiwa na wengi na mpaka sasa naendelea kuwepo ofisini ‘kimagumashi’.
Ndiyo! Hata kama bado unaendelea kushikilia msimamo wako kwamba hukushiriki kwa namna yoyote kutafuna mabilioni ya Akaunti ya Tegeta Escrow, lazima dhamira yako ikutume kuchukua uamuzi ambao ni wa busara, achia ngazi kwa ridhaa yako kuliko kuendelea kuwekwa kiporo kwa kipindi chote hiki kwani cheo ni dhamana!
Hatima yako inajulikana mheshimiwa, badala ya kusubiri mpaka dakika za mwisho, huoni kama ingekuwa busara kuamua tu kung’atuka madarakani ili uendelee kulinda hiyo heshima yako ‘kiduchu’ iliyobakia katika jamii? Unafurahi kuendelea kuitwa majina mabaya wakati ukiendelea kutimiza majukumu ya kila siku?
Hebu usomi wako ujipambanue kwa vitendo, wahenga wanasema, ‘Muungwana akivuliwa nguo huchutama.’ Chutama mheshimiwa, ofisi haikufai tena hiyo kwa sababu cheo ni dhamana.
Wasalaam.
USISITE KUTUACHIA UJUMBE WAKO HAPO CHINI
Post a Comment