NAMSHUKURU
Mungu kwa kunikutanisha nanyi marafiki Jumamosi ya leo. Mungu ni mwema
sana ndiyo maana anazidi kutubariki kila kukicha. Tunakutana tena katika
darasa letu huru, tunafundishana masuala yahusuyo uhusiano wa mapenzi.
Leo
nimependa tujadili mada hii ambayo naamini inagusa watu wengi. Wengi
wetu tunakubaliana kwamba tumekutana na jambo hili kwa nyakati
tofauti.Unampigia simu mpenzi wako hapokei, meseji hajibu na wala hana
habari na ujumbe wako lakini ukikutana naye na kumuuliza kama anakupenda
anakwambia anakupenda.
Tatizo hili linawapata watu wote lakini mara nyingi zaidi limekuwa
likiwatesa wanawake. Wanaume wengi wanapoingia kwenye uhusiano wanakuwa
mafundi sana wa kutuma meseji.Tena meseji zile zenye kumfanya mwanamke
ajione mwenye thamani ya hali ya juu.Wanakuwa mahodari wa kuandika maneno matamu, wanapiga simu mara kwa mara. Hicho ndicho kipindi huwa wanapiga simu kuuliza kama wapenzi wao wamekula au wamelala au kuuliza ‘unafanya nini sa hivi.’ Mwanamke anajaliwa kiasi cha kuona kama ulimwengu wote ni wake.
Hapo wanawarubuni wanawake kuficha makucha yao. Mwanamke huona amepata. Kama ni mahitaji muhimu atayatoa, anahakikisha mwanamke hapati shida ya aina yoyote. Wakati utamu ukiwa unakolea, ghafla tu wanaanza kubadilika. Ukituma meseji hajibu, ukipiga simu hapokei.
Ndugu zangu hapo ndipo kwenye msingi wa mada yangu ya leo. Kitendo cha kutopokea simu, kutokubali kukuona au kutaka kumuona hadi umlazimishe ni ishara kwamba kuna tatizo.Mbaya zaidi bora kama angekuwa hapokei kwa muda fulani halafu baadaye apokee, hapana. Anakunyamazia hata mwezi mzima.
Yeye anaamua tu kutopokea kwa wiki, miezi na hata mwaka mzima. Tena bora basi angekwambia kwamba sikuhitaji, anakunyamazia kimya na hata ukibahatika kukutana naye anakwambia; ‘nakupenda sema tu kazi zinabana ndiyo maana unaona kimya, usijali lakini mpenzi wangu bado nakupenda.’
Marafiki tutazame mfano hai kutoka kwa msomaji wangu mmoja. Aliniambia hivi:
“Anko naomba ushauri wako. Mimi ni msichana mwenye umri wa miaka 21, nina mchumba wangu ambaye tulikuwa na mipango mizuri ya kutambulishana kwa wazazi sambamba na kufikia hatua ya ndoa lakini nimeshangaa ghafla amebadilika.
“Siku
hizi kila nikimpigia simu hapokei, nikimtumia meseji hajibu na hata
nikimtumia marafiki zake anawaambia waniambie nisiwe na wasiwasi eti
yupo bize tu na kazi lakini ananipenda. Ninapata shaka kwa sababu
mwanzoni hakuwa hivi, kwa miezi mitano sasa amekuwa kimya tu.”
Mfano huo unatufundisha nini? Mada yangu ya leo. Mpenzi wa msomaji
huyo anakuwa amebadilika kutokana na sababu zake anazozijua.
Anamsababishia mwenzake mawazo ya hali ya juu. Hamuelezi ukweli juu ya
mabadiliko yake anajifanya kama penzi lipo sawa kumbe halipo sawa.Ndugu zangu, kwa mwanaume wa aina hiyo, mwanamke unapaswa kujiongeza. Unapaswa kupima uwiano wa muda unaopoteza na majibu unayoyapata kutoka kwa mwenzako.
Kama majibu ni ‘usijali tuko pamoja’ halafu kiuhalisia hampo pamoja kwa zaidi ya miezi mitano au sita ni tatizo.
Penzi la aina hiyo huwa ni maumivu kwa upande mmoja. Mwanamke anateseka moyoni wakati mwenzake haumii wala hajui maumivu anayoyapata mpenzi wake. Utafiti usio rasmi ambao nimeufanya, mara nyingi wanaume wa aina hiyo wanakuwa tayari wameshaanzisha uhusiano na mtu mwingine.
Wanashindwa kusema ukweli tu. Wanakuzungushazungusha pasipo kuwa na sababu za msingi, hapo mwanamke unapaswa kujiongeza.Msake mwenzako kinaga ubaga, mweke chini uzungumze naye na ujue msimamo wake. Kama akikiri amebadilika kwa bahati mbaya, mpe muda lakini ukiona ni yaleyale basi ni bora kuachana naye na usubiri umpate ambaye atakuwa na mapenzi ya dhati.
USISITE KUTUACHIA UJUMBE WAKO HAPO CHINI
Post a Comment