Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

NINGEKUWA MIMI HAWA GHASIA, NINGEKUWA WA KWANZA KUJIUZULU

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa- tamisemi), Hawa Abdulrahman Ghasia.
Kwako Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa- tamisemi), Hawa Abdulrahman Ghasia.

Ni matumaini yangu kwamba bado upo kwenye wakati mgumu kutokana na madudu yaliyotokea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na kusababisha sehemu nyingine uchaguzi uahirishwe kutokana na dosari za mbalimbali za wazi zilizojiri.
Najua itakuwa vigumu kuonana na wewe kwa sasa kutokana na presha uliyonayo ndiyo maana nimeamua kufikishia ujumbe wangu kupitia ukurasa huu.Mheshimiwa, mimi sikuzaliwa Januari 10, 1966 mkoani Mtwara kama wewe. Sikusoma Shule ya Msingi Naumbu mwaka 1976 hadi 1982 na baadaye kujiunga na Sekondari ya Ndanda na kuhitimu kidato cha sita mwaka 1986.
Mimi sikusomea Vyuo Vikuu vya Mzumbe na Sokoine mjini Morogoro wala sijawahi kushika wadhifa wowote kwenye Chama cha Mapinduzi (CCM) kama wewe. Mimi si Mbunge wa Mtwara Vijijini kama wewe na nakuhakikishia sijawahi wala haiwezi kuja kutokea nikawa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi) kama wewe.
Sijui chochote kuhusu siasa wala kuhusu mipango ya maendeleo au utawala bora, niponipo tu! Sina mbele wala nyuma. Hata hivyo, licha ya umbumbumbu wangu huo, ningekuwa mimi katika nafasi yako, kwa haya madudu yaliyotokea kwenye chaguzi za serikali za mitaa, walahi nakwambia ningekuwa wa kwanza kuwajibika kwa kujiuzulu!
Ndiyo! Kwa nini niendelee kupigwa na kipupwe ofisini, kutembelea gari la kifahari na kupokea mshahara mnono na marupurupu wakati kazi niliyopewa imenishinda? Suala la uchaguzi wa serikali za mitaa halikuwa la kushtukiza. Tangu unakabidhiwa madaraka, ulikuwa unajua kwamba kuna jukumu la kuratibu, kusimamia na kufanikisha uchaguzi huo.
Mheshimiwa, kulikuwa na haja gani ya kufanya maandalizi ya zimamoto wakati serikali ilishawahakikishia wananchi kwamba licha ya bunge maalum la katiba kuendelea kwa muda mrefu, hakukuwa na haja ya kuusogeza mbele uchaguzi huo kwa sababu maandalizi yalikuwa yanaendelea vizuri?
Inawezekana kabisa Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda anaonekana hafai au anashambuliwa sana kwamba anashindwa kutimiza majukumu yake kwa sababu ya watendaji mlio chini yake ukiwemo wewe. Mheshimiwa, wizara yako inawezaje kufanya mzaha kwenye jambo muhimu kama uchaguzi? Mnamponza mzee Pinda.
Serikali kupitia kwa watendaji wake ilitangaza kwamba maandalizi ya uchaguzi yamekamilika kwa asilimia 100 na kuwataka watu wajitokeze kwa wingi kupiga kura wakati sehemu nyingine hata karatasi za kupigia kura zilikuwa hazijafika kabisa, sehemu nyingine zilifika lakini zikiwa na dosari kibao ikiwemo kukosea majina ya wagombea, wapiga kura na vyama vyao? Tuuiteje hali hii kama siyo uzembe wa hali ya juu?
Yote tisa, kumi ni siku yenyewe ya upigaji kura. Vituko vilikuwa vingi mno, ulinzi ulionekana kupwaya kwenye vituo vya kupigia kura huku mianya ya udanganyifu ikijionesha waziwazi. Unataka sisi walalahoi tuamini nini? Kwamba haya yote yalitokea kwa bahati mbaya au ulikuwa ni mchezo ulioandaliwa ili kutimiza matakwa ya wachache?
“Nitakuwa tayari kuwajibika kama nitapatikana na kosa la kuwa sehemu ya kuvuruga uchaguzi wa serikali za mitaa. Kushindwa kusimamia vizuri uchaguzi na kusababisha kasoro ni moja ya makosa makubwa na kwa wale watakaobainika, watachukuliwa hatua kali kulingana na uzito na kiwango cha uhusika wao.”
Kauli hii uliyoitoa mheshimiwa wakati ukizungumza na waandishi wa habari baada ya kutokea madudu hayo kwenye uchaguzi, inaonesha kwamba wewe ni mtu ambaye umekomaa kisiasa.
Hata hatua ulizozichukua baada ya hapo za kutengua uteuzi wa wakurugenzi watendaji sita wa halmashauri za wilaya, kuwasimamisha wengine watano na kuwapa onyo kali wengine sita kwa kushindwa kutimiza wajibu wao katika kusimamia uchaguzi huo uliofanyika Desemba 14, mwaka huu zinaonesha kwamba wewe ni kiongozi ambaye unajua kuwawajibisha wengine.
Hata hivyo, kuwawajibisha wengine pekee hakutoshi, kilichotokea kilikuwa chini ya wizara yako na ulikuwa na uwezo wa kuzuia kisitokee, hilo ni kosa kubwa ambalo linatosha kukufanya ukubali kuwa wa kwanza kuwajibika. Achia ngazi mheshimiwa!
Wasalaam.
USISITE KUTUACHIA UJUMBE WAKO HAPO CHINI.

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
© Copyright BONGO HABARI
Back To Top