Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

NAONGEA NA JIDE NA WANAWAKE WANAOPIGWA NA WAUME ZAO

Jumanne tena! Jumanne hii iko ndani ya msimu wa sikukuu, kuna Krismas na Mwaka Mpya! Lakini sikukuu ya kwanza ni Mwaka Mpya halafu inakuja Krismas, si ndiyo?Wiki hii nina mada nzito jamani! Ndiyo maana nimeipa uzito wa kichwa kisemacho; naongea na Jide na wanawake wanaopigwa na waume zao.

Mada hii kwanza inataka utulivu kuielewa kwani mtu akisoma kwa juujuu anaweza kutoka kapa. Lakini naamini wasomaji wangu wote wana ufahamu mzuri hivyo itakuwa rahisi kujua ninachokizungumzia.
MALALAMIKO YA VIPIGO
Malalamiko ya wake kudai wanapigwa ndani ya ndoa ni mengi sana, hata taasisi mbalimbali za utetezi zimekuwa zikipiga vita ukandamizaji huu wa wanaume kuwapiga wake zao.Kwa Tanzania tuna Chama cha Wanahabari Wanawake (Tamwa) ambao pia wapo mstari wa mbele kutetea tabia ya baadhi ya wanaume kuwapiga wake zao.
KUNA MGAWANYO
Kwanza ningependa iweleweke kwamba, kuna makundi mawili ya wanaume wenye tabia hii. Kundi la kwanza ni lile ambalo kimsingi katika malezi, wanaume wanajua ni wababe, kwa hiyo kuwapiga wake zao si suala linaloanzia mbali. Yaani hakuna msukumo wa ugomvi unaotoa mwanya kwa mume kumpiga mke bali ni suala la kawaida hata kama kosa ni dogo.
Kundi la pili ni la wanaume ambao ndani ya nafsi zao hakuna msukumo wa kumpiga mkewe bali mke mwenyewe ndiyo hutengeneza mazingira ya kupigwa kwa njia yoyote ile.
TUCHAMBUE SASA
Kabla sijaandika mada hii nilizungumza kwanza na watu mbalimbali, hususan wanaume na wanawake ambao wapo ndani ya ndoa.Nilipata simulizi ndefu sana na nikajifunza mengi kupita maelezo yao ndiyo maana nikajiridhisha kwa kuweka makundi mawili ya wanandoa wanaopigwa!
TWENDE NA MIFANO
Mzee Samuel Marwa, mkazi wa Kitunda jijini Dar yeye alisema kwa mila na desturi za kwao, mwanamke asipopigwa hakuna mapenzi wala ndoa. Na aliongeza kuwa, kwao (nadhani mkoani Mara) mwanaume haonekani ni mwenye hatia au kosa kwa kumpiga mkewe.
Alisema: “Mke anaweza akachelewa kufungua mlango tu au kukuletea maji ya kunywa unaweza kumpiga ili kumfundisha tabia njema kwa mume wake.”Hoja au madai ya mzee Marwa yalisemwa na wengi lakini utafiti wangu ukaonesha kuwa, wengi wa hao wanatoka maeneo yanayofanana.
WANAWAKE HULAZIMISHA KUPIGWA?
Kundi jingine la watu niliozungumza nao ni lile ambalo, liliwapa mzigo wanawake kwamba wao ndiyo wanaolazimisha kupigwa na wanaume zao.“Ndugu yangu, mimi mpaka wakati naoa sikuwa na wazo la kumpiga mke wangu na wale niliokuwa nawasikia wanapiga nilikuwa nawalaani sana.
“Siku moja mke wangu alirudi nyumbani saa tatu usiku, nikamuuliza alikokuwa, akawa anajikanyagakanyaga, kwa hasira nikamwambia akalale kwa watoto mpaka asubuhi.
“Akanijia juu, tena anapandisha sauti akisema siendi kulala, kalale wewe. Sasa nikifikiria, kwanza kanikosea, karudi usiku bila kuweka wazi alikokuwa halafu anapandisha, kwa kweli nilimpa kipigo cha nguvu.
“Kisa cha kumwambia akalale chumba cha watoto kwa sababu alishaanza kupandisha sauti na mimi nilikuwa nimechoka sana kazini,” anasimulia Masoud Ally, mkazi wa Magomeni-Kagera, Dar.
Naye Mkande, mkazi wa Mbezi Beach jijini Dar, yeye alikuwa na ushuhuda huu:
“Mimi niliwahi kunyanyua mkono kumpiga mke wangu mara mbili. Kwanza, siku moja aliniudhi sana, kwa hasira nikaamua kutoka chumbani ili nikakae sebuleni kwa muda na kuangalia tivii, yeye akasimama mlangoni kunizuia nisipite.
“Nilimwomba kama mara nne hivi anipishe akagoma. Sasa katika kutumia nguvu nikajikuta nampiga ili aachie kuzuia mlango mimi nipite. Unaona sasa hapo, kama angeniacha nipite nisingempiga, alitaka mwenyewe.”
WANAVYOSEMA WANAWAKE
“Wanaume wanapenda sana kutuonea sisi wanawake kwa vile wanajua hatuna nguvu, lakini kusema kweli mimi kama mimi sipendi kabisa kupigwa,” mama Salome, mkazi wa Ubungo, Dar.
Mada hii ni ndefu sana, itaendelea wiki ijayo, usikose tafadhali.

USISITE KUTUACHIA UJUMBE WAKO HAPO CHINI

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
© Copyright BONGO HABARI
Back To Top