Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

SIMULIZI TAMU YA BAHATI BUKUKU; AWAPIGA WANAFUNZI WENZAKE - 2

 
Mwimbaji wa nyimbo za injili, Bahati Bukuku.
ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA
Nilikifuata kisima kile na kutulia pembeni huku nikiwa nimejikunyata.
Ni sauti za ng’ombe na mbuzi tu ndizo zilizokuwa zikisikika asubuhi hiyo, watu wengine walikuwa wamelala kwani ilikuwa ni asubuhi sana.
SASA ENDELEA...

Watoto tulikuwa na mchezo fulani hivi, ukisikia mzazi wako kakwambia uende kuoga, ukifika kule wala haujisugui, kama ni bafuni unajimwagia maji tu au kama ni kwenye kisima unaingia na kutoka, yaani mwili ukiloa tu, tayari unajifanya kwamba umeshaoga.
Japokuwa siku hiyo kulikuwa na baridi kali huku nikitetemeka, nikajikuta nikiingia ndani ya kisima, wala sikujisugua, ndani ya sekunde kumi, nikatoka na kuelekea ndani huku nikitetemeka na meno yakigonganagongana.
Ndani, nikawakuta wazazi wamekwishaamka. Kwanza wakashangaa, haikuwa kawaida yangu kuamka asubuhi na mapema kiasi kile, ila walipokumbuka kwamba siku hiyo niliahidiwa kwenda kuanza chekechea, wakajua ndiyo ilikuwa sababu ya kuamka mapema namna ile.
Mama akaniita chumbani na kunivalisha nguo mpya. Nakumbuka ilikuwa sketi ya kijani, shati la drafti na soksi za pundamilia huku viatu nilivyopewa vikiwa vipya kabisa, nilijiona nimependeza mno.
ATANGULIA SHULE MWENYEWE
Japokuwa siku hiyo nilitakiwa kwenda shuleni na baba, niliona anachelewa, nilichofanya ni kumtoroka, nikatangulia zangu kwa sababu nilikuwa na hamu ya kusoma lakini baba hakuwa akifanya mambo yake kwa haraka.
Nilipofika kwenye ile shule ya chekechea, wanafunzi wengi walikuwa nje. Wengine walikuwa wakicheza, wengine wakiandikaandika ardhini.
Wala sikukaa sana, baba akaja shuleni na kunipeleka kwa Mwalimu Rose ambaye aliniandikisha jina na kuanza masomo shuleni hapo.
“Ila huyu ni cha utundu, kuwa naye makini,” baba alimwambia mwalimu huku akimwangalia Mwalimu Rose.
“Hakuna tatizo,” alisema Mwalimu Rose ingawa nilikuwa na uhakika asingeweza kunidhibiti kwa jinsi nilivyokuwa mtundu.
MAISHA YA SHULE
Kila siku shuleni tulikuwa tukipewa uji hasa baada ya masomo. Rose alikuwa mtu mzuri, mwalimu mwenye huruma asiyejua kuchapa lakini mapenzi yetu wanafunzi yalikuwa kwa mpishi wa uji.
Huyu ndiye alikuwa rafiki yetu mkubwa kwa kuwa alikaa jikoni.
Urafiki wetu na Mwalimu Rose ulikuwa darasani, ila tulipokuwa tukitoka tu, tulimfuata ‘rafiki yetu wa ukweli’, mpishi na kuanza kusubiri uji.
Kiukweli, uji ulinifanya kupenda shule zaidi, kila siku nilikuwa nikiamka asubuhi na mapema na kuwahi shule, uji ndiyo ulionifanya kutamani sana kulala hukohuko shuleni. Hapa haimaanishi kwamba nyumbani hatukuwa na uwezo wa kunywa uji, tulikuwa tukinywa sana lakini siku zote uji wa shule niliuona mtamu sana.
AZUNGUMZIA KUJIKOJOLEA
Ndani ya shule hiyo ya Jani Bichi kulikuwa na watoto kutoka sehemu mbalimbali ambapo kila mmoja alikuwa na tabia yake. Kulikuwa na watoto waliokuwa wakijikojolea mara kwa mara darasani.Hapa ninaweza kusema kwamba walimu wa shule za chekechea wana wakati mgumu sana kuliko wa msingi au sekondari.
Kukutana na kundi la watoto waliokuwa na tabia tofautitofauti hasa zenye kukera na bado unaweza kuwaweka chini na kutulia, huwa ni jambo gumu sana.
Kwa upande wangu, sikuwa mtoto wa kujikojolea, kitu pekee ambacho kilikuwa kikimsumbua mwalimu wangu ni utundu tu. Sikuwa nikitulia darasani, kila wakati ilikuwa lazima nisimame na kuanza kufanya mambo mengine ambayo sikutambua kwamba yalikuwa yakimuudhi mwalimu.
AWAPIGA WANAFUNZI WENZAKE
Japokuwa nilikuwa msichana, lakini nilikuwa mchokozi sana, nakumbuka mara kwa mara nilikuwa nikiwapiga watoto wenzangu tena wa kiume, watoto wengine wakawa wananiogopa kwani nilikuwa mtemi kama mvulana.
ATAPIKIWA NA MWANAFUNZI MWENZAKE
Kulikuwa na mambo mengi ambayo yalitokea shuleni, ila kuna jambo moja ambalo kwangu sitoweza kulisahau. Kulikuwa na mtoto mmoja siku moja alishiba uji mpaka tumbo lake lilionekana kubwa kama kitambi, watoto tulimcheka kutokana na hali hiyo.
Wakati nimekaa huku nikiwa sina hili wala lile, yule mtoto alinisogelea nyuma na kunitapikia! Alinilowesha na matapishi yake, nguo zangu zote zilichafuka. Nilikasirika sana, badala ya wanafunzi kumcheka mtoto yule, wakaanza kunicheka.
Kwa sababu nilikuwa mtemi kwa watoto wote shuleni, nilisimama kwa lengo la kumpiga lakini mwalimu akaniwahi. Moyo wangu uliumia mno, sikuwa na jinsi, kutokana na hasira nilizokuwa nazo, nikaanza kulia.
“Lusako tughala pasi,” (wewe Lusako kaa chini) mwalimu aliniambia.
“Andekile,” (amenitapikia) nilimwambia mwalimu huku nikiwa na hasira kupita kiasi.
Bado nilimwangalia yule mtoto kwa hasira, niliyauma meno yangu huku nikitetemeka mwili mzima. Mwalimu aliligundua hilo, akanichukua na kunitoa eneo lile.
“Ngakughana,” (nakuchukia) nilimwambia yule mtoto huku nikiwa na hasira.
Siku hiyo imekuwa kama alama kubwa maishani mwangu. Japokuwa nimejitahidi sana kuisahau siku ile  lakini moyo wangu umeshindwa kufanya hivyo.
Kila ninapotulia, iwe sebuleni au chumbani kwangu, picha ya siku ile huwa inanijia kichwani. Tukio hilo limekuwa kubwa kwangu huku likiendelea kujirudia kama mkanda wa filamu.

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
© Copyright BONGO HABARI
Back To Top