Dk Salim alitoa kauli hiyo katika mahojiano maalumu na gazeti hili nyumbani kwake Masaki, Dar es Salaam wiki iliyopita.
“Hatukutarajia
kama hali ingefikia hatua iliyofikia,” alisema Dk Salim na kuongeza:
“Lakini Rais ana uamuzi wake na anazingatia mambo mengine mengi.”
Akilihutubia
Bunge maalumu la Katiba Machi 21, mwaka huu Rais Kikwete aligusia mambo
saba ya msingi yaliyomo katika Rasimu ya Katiba na kutaka yatazamwe kwa
kina, huku akibainisha kuwa mengine hayawezekani kutekelezeka. Miongoni
mwa mambo hayo ni muundo wa Serikali. Alipinga waziwazi pendekezo la
serikali tatu lililopendekezwa na Tume na kuegemea katika muundo wa
serikali mbili na idadi ya watu walioupendekeza akionyesha kuwa ilikuwa
ni ndogo.
Pia
alisema ni vigumu kutenganisha uwaziri na ubunge kama ilivyokuwa
imependekezwa na Tume kwa maelezo kuwa mawaziri wanatakiwa kuwepo
bungeni ili kujibu hoja za Serikali.
Jambo
lingine alilokosoa katika Rasimu ni pendekezo la mtu kupoteza ubunge
kwa sababu ya kuugua kwa miezi sita mfululizo huku akisema baadhi ya
vifungu vya Katiba vinayopendekezwa vimekuwa na mambo mengi ambayo
hayapaswi kuwamo katika Katiba, bali katika sheria zinazotafsiri
utekelezaji wa Katiba yenyewe.
Katika
mahojiano hayo maalumu, Dk Salim alisema baada ya kuteuliwa kuwa Mjumbe
wa Tume aliacha kuhudhuria vikao vya chama chake ili aweze kufanya kazi
hiyo kwa usahihi na alimtaarifu Mwenyekiti wa CCM ambaye ni Rais na
katibu mkuu wake na walimwelewa.
Alipoulizwa
anaitazama vipi Tanzania iwapo Katiba Mpya haitapatikana, Dk Salim
alisema ana wasiwasi kwa kuwa suala hilo limeingizwa siasa na Bunge
Maalumu limegeuka la kisiasa hivyo linaweza kuleta matatizo.
“Tuko
katika hali ambayo si nzuri inayohitaji uongozi thabiti, viongozi wote
watambue umuhimu wa zoezi hili kwa lengo la kulinda amani na utulivu wa
nchi yetu,” alisema.
Alisema
kunahitajika ufumbuzi wa kudumu na hicho ndicho kipimo cha uongozi kwa
CCM, Chadema na wengine kwa kutafakari masilahi ya Watanzania wa leo,
kesho na keshokutwa.
Nini kifanyike?
Dk
Salim alisema jambo muhimu sasa ni pande mbili zinazoshindana kuhusu
idadi ya Serikali kutumia mwezi ujao wa Julai kukaa pamoja na kumaliza
tofauti zao ili Bunge la Katiba liendelee bila misuguano.
“Mwezi
huu wa Julai ni muhimu sana, ni mwezi pekee uliobaki wa kuwaweka pamoja
wanaotofautiana. Kila jitihada zinatakiwa kufanyika ili kuhakikisha
Bunge Maalumu linakutana tena Agosti na wapinzani waliosusa wanarejea
ili kumaliza kazi hiyo kabla ya kutoa rasimu ya tatu kwa ajili ya kura
za maoni,” alisema na kuonya kuwa kuendelea na katiba ya sasa kunaweza
kuleta matatizo.
Neno ‘wasaliti wa Mwalimu Nyerere’ lamchefua
Aidha,
Dk Salim ameeleza kusikitishwa na kukatishwa tamaa na kauli za baadhi
ya wanasiasa dhidi yake na wajumbe wenzake wa Tume kwa kuwaita wasaliti
na hasa kitendo cha kutilia shaka uzalendo wao.
“Inakatisha
tamaa sana. Mimi nina umri wa miaka 72, kati yake zaidi ya miaka 30
nimeitumikia nchi yangu, haiingii akilini katika umri huu wa mwisho
nianze kuisaliti nchi yangu, inasikitisha sana kusikia eti hawa wasaliti
wa Mwalimu Nyerere,” alisema.
Dk
Salim ambaye ni Mwenyekiti wa Mfuko wa Mwalimu Nyerere (MNF),
alisisitiza kuwa wajumbe hao wamekuwa wakishutumiwa na watu wenye
malengo yao, akitolea mfano kuwa hata Dk Mwesiga Baregu aliwahi
kushutumiwa na chama chake na kutakiwa ajitoe kwenye tume hiyo
iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.
Itakumbukwa
kwamba Tume ya Mabadiliko ya Katiba imekuwa ikishutumiwa na wanasiasa
hasa kutoka CCM kutokana na mapendekezo yake ya mfumo wa Muungano wa
serikali tatu badala ya mbili zinazoungwa mkono na chama hicho.
Kutokana
na tofauti hiyo, wajumbe walio wengi wa Bunge Maalumu la Katiba kutoka
CCM waliamua kubadili baadhi ya vifungu vya rasimu.
“Ni
bahati mbaya sana binadamu unapotukanwa, unatupiwa madongo, tunaonekana
wapuuzi kwa kazi ya kukusanya maoni ya wananchi, inaumiza sana,”
alisema.
Kama
ambavyo Jaji Warioba amesema mara nyingi, Dk Salim aliitetea Rasimu ya
Katiba, akisema kilichopendekezwa ndiyo picha halisi ya maoni ya
Watanzania.
Alisema
Tume hiyo ilikusanya maoni ya wananchi yenye hoja nzito yakieleza hasa
matatizo yao katika nyanja mbalimbali kama afya, elimu, ardhi na
mengine, ingawa hoja kuhusu muundo wa Serikali ndizo zinaonekana
kushikiwa bango na wanasiasa.
Alisema
ushahidi wa watu waliohojiwa upo katika maandishi, sauti na picha za
video na idadi yao inatosha kuwakilisha Watanzania wote.
“Wanasema
hatukuhoji watu wengi, waliohojiwa ni representative sample (sampuli),
huwezi kuhoji Watanzania wote milioni 45,” alisema Dk Salim.
Alisema
ni jambo la kushangaza kuwa mchakato umetekwa nyara na wanasiasa lakini
Katiba inastahili kuwa ya kitaifa ya Watanzania wote, wenye vyama na
wasio na vyama vya siasa.
Alisema
hata kwenye tume, walikuwapo wajumbe zaidi ya 12 ambao hawatokani na
CCM, wakitoka vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi na wote walikuwa na mawazo
tofauti lakini waliamua kuyaweka kando na kutoa rasimu inayotoa taswira
ya mawazo na masilahi ya wananchi.
Post a Comment