MSANII wa muziki wa kizazi kipya, Rehema Chalamila ‘Ray C’, amesema kwa sasa hana mpango wa kuwa na mahusiano ya kimapenzi na mtu, na kama ikitokea basi atamtaka kuwa na miaka kuanzia 60.
Akizungumza katika kipindi cha ‘The
Sporah Show’, Ray C alisema anahitaji wanaume wa umri mkubwa, kwa kuwa
wanajua wanachokifanya, na kukiri kwamba vijana walichangia katika
kurudisha nyuma maisha yake.
Msanii huyo ambaye kwa sasa ameanzisha
asasi yake ya kupambana na dawa za kulevya, kutokana na yeye kuwa mmoja
wa waathirika wa dawa hizo, alisema katika moja ya mambo anayoyajutia ni
kuwa na mahusiano na vijana, jambo ambalo hataki kukumbuka
walichomfanyia hadi kudhalilika mbele ya jamii.
Hata hivyo, alitumia fursa hiyo kuwaasa
wazazi kutowatenga watoto wao ambao wamejidumbukiza kwenye utumiaji wa
dawa za kulevya na badala yake, wawakumbatie na kuwaonyesha njia kama
mama yake alivyofanya na kurudia hali yake ya kawaida.
Kuhusu kurudi kwenye muziki, Ray C
alisema yupo mbioni na tayari ameshatengeneza nyimbo kadhaa, ambapo hivi
sasa atakuwa akiimba miondoko tofauti tofauti, ikiwemo taarabu.
Katika kurudi kwenye muziki, jambo la
kwanza alisema anatarajia kupunguza mwili wake kwa kufanya mazoezi,
kwani hata daktari wake alishamwambia anatakiwa kupungua kutokana na
umri wake kutoendana na kilo alizonazo.
Alipoulizwa mwanamuziki ambaye kwa sasa
anamkubali Bongo, Ray C alisema wa kwanza ni AT akifuatiwa na Recho
kutoka Jumba la Kukuza Vipaji (THT).
Post a Comment