Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

NDOA SIYO RAHA PEKEE, JIPANGE KWA MATATIZO PIA! - 3

 
NIMEFURAHI tumekutana tena hapa katika All About Love, safu ambayo inatengeneza maisha ya wengi kuhusu uhusiano wao. Bila shaka hata wewe umebadilika sana baada ya kuwa mdau wa kona hii.

 
Hata hivyo, wale ambao ndiyo kwanza mmeanza kusoma ukurasa huu, mnatakiwa kujivunia sana maana ni sehemu sahihi zaidi ya kujifunza kuhusu uhusiano na maisha.
Tunaangalia kuhusu ndoa, leo ikiwa ni sehemu ya mwisho.  Je, unawaza nini katika ndoa yako ijayo? Unategemea nini zaidi kwa mwenzako? Kwa wiki mbili mfululizo nimelizungumzia hili kwa mapana, lakini bado kuna vitu vya kujadiliana zaidi. Leo nitamalizia vipengele vilivyobakia.
NASABA YAKE
Kama ni kweli una matarajio mazuri kutoka kwa mwenzako, kipengele hiki ni muhimu kabla ya kufanya uamuzi wa kuingia kwenye ndoa.
Lazima uijue vizuri familia yake. Anatoka katika familia ya namna gani? Kabila gani? Ukiachana na hilo, hapa lazima ufahamiane na ndugu zake, japo kidogo na upate muda wa kuwazoea.
Kuna familia nyingine ni wakorofi, kama ukiolewa huko ni tabu tupu. Pengine ukiona katika familia yao, labda wana tabia ya udokozi...si ajabu ukaibiwa hata wewe.
Kweli umempenda na unataka kuishi naye, lakini utaratibu mbaya wa ndugu zake ni kielelezo cha matarajio ya maisha yenu ya ndoa. Kuwa makini.
KUHUSU AFYA
Baadhi ya watu kwa bahati mbaya wana matatizo ya kudumu kiafya. Utakuta huyu ana udhaifu wa kusumbuliwa na shinikizo la damu, mwingine vidonda vya tumbo, kifafa n.k.
Ni udhaifu ambao yeyote anaweza kuwa nao. Kwa nini nimegusia hili? Kuna baadhi ya rafiki zangu wanaingia kwenye ndoa wakiwa hawajui matatizo ya wenzao, hivyo kusababisha usumbufu.
Hujui mwenzako anasumbuliwa na nini, mnagombana kidogo unaanza kumpiga, unashangaa ameanguka chini, damu zinaanza kumiminika puani! Si kosa lako, maana hukujua!
Hapa kuna umuhimu mkubwa wa kujua afya ya mwenzako. Kama ana maradhi ya kudumu ni vyema ukajua, ili pia ufahamu utakavyotakiwa kuishi naye ndani ya ndoa.
Hakikisha unaijua historia ya afya yake vyema. Hakuna maana mbaya kufahamu, isipokuwa utakuwa na uwezo wa kumchukulia kulingana na udhaifu wake.
MILA & DESTURI
Kuna makabila mengi nchini, kila watu wana mila zao, lazima uzijue japo kwa ufupi. Unaweza kuzungumza naye au ukawashirikisha watu wazima ambao wana ufahamu mkubwa, watakusaidia.
Unaweza kuingia kwenye kabila ambalo mila zake zinaruhusu mwanaume kulala na shemeji yake kama kaka yake hayupo; itakuwaje hapo kama ulikuwa hujui?
 
Kuna mengi ambayo siwezi kuyaandika yote, lakini jambo kubwa na muhimu kwako hapa ni kuhakikisha unafahamu mila na desturi za mume/ mke wako mtarajiwa.
MJADALA WA DINI NI MUHIMU
Inapendeza zaidi kama mkioana ndani ya imani moja ya dini. Upo utaratibu wa wachumba kufunga ndoa bomani, ambapo kila mmoja huwa na dini yake. Siku za hivi karibuni wengi wanafanya hivyo, lakini si sahihi kwa asilimia mia moja.
Ndoa imara, ukiacha juhudi za wahusika wenyewe hujengwa na hulindwa na imani thabiti ya dini ya wahusika. Mnapokuwa katika imani moja, ni rahisi kumfikia Mungu pamoja katika maombi au kwenda kwa viongozi wa dini pamoja na kupewa ushauri wa kiroho.
Jambo hili lisiwe la mwisho, kama tayari dalili za kuoana zinaonekana wazi, muanze kujadiliana mapema juu ya suala la dini. Lazima muwe dhehebu moja, kama mpo tofuati, mshauriane ili mmoja amfuate mwenzake. Hakuna kinachoshindikana kwenye mazungumzo.
MUWE NA NIA MOJA
Hapa namaanisha kwamba, ili ndoa yenu iwe bora lazima kuanzia mapema muwe na nia moja kwa kila jambo. Sina lugha nyepesi sana ya kudadavua hili, lakini kikubwa ni kwamba mnapaswa kuwa na mawazo ya aina moja kwa maana ya kushirikishana tangu mapema.
Jengeni mazoea ya kushirikishana kila kitu. Hii itawajengea uaminifu na kila mmoja kujiona sehemu ya mwenzake.
Kwa nini?
Ndiyo taswira ya kile unachokiendelea ndani ya ndoa. Ikiwa uhusiano wenu awali haukuzingatia niliyoyataja hapo juu, matarajio ya ndoa yako yatakuwa kinyume.
Acha utaratibu wa kuamini kwamba kwenye ndoa kuna furaha, kuna starehe tu, kuna kusaidiana tu. Zipo changamoto ambazo lazima ukubaliane nazo au ujiandae kukutana nazo kuanzia mapema.

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
© Copyright BONGO HABARI
Back To Top