Wazazi ndiyo dira ya watoto na ndiyo maana haishangazi kuona mtoto wa mzazi ambaye ana tabia flani mbaya akawa ameirithi kutoka kwa wazazi.Waswahili wanasema mtoto umleavyo ndivyo akuavyo, wazazi wana nafasi kubwa katika maamuzi ya watoto wao hadi pale na wao watakapofikia hatua ya kuwa na familia yao.
Wazazi wanaweza kuwa na msimamo fulani katika jambo la vijana wao, mwisho wa siku vijana wao wanalazimika kukubaliana nao. Wazazi kwa sababu zao wanaweza kuonesha msimamo katika jambo fulani ikiwemo hata kuzuia suala la ndoa na kweli isifungwe.
Inapotokea mvutano wa wazazi katika suala la ndoa ndipo mfarakano mkubwa unapotokea. Wapendanao watakuwa wanayumbishwa, kutokana na nguvu hiyo, mara nyingi waathirika wanakuwa wanandoa watarajiwa.
Wanaathirika kwa sababu wao wanaweza kuwa wamekubaliana kwa hali yoyote lakini wazazi wanaweza kuweka kipingamizi kulingana na vigezo ambavyo wao wanavifahamu.Hapo utakuta upande mmoja unataka ndoa mwingine unakuwa hautaki. Msukumo unakuwa mkubwa, wanandoa watarajiwa nao wanabaki njia panda. Upande unaokataa ndoa unakuwa na sababu zake kulingana na matakwa ya dini, desturi na hata imani.
“Tumekaa vikao na vikao ili kujaribu kutafuta suluhu lakini wapi hatukupata muafaka, kwa kweli nimechoka. Kinachoniuma zaidi ni kwamba sisi wenyewe hatuna tatizo, tumekubaliana kufunga ndoa hata bomani kila mmoja akabaki katika dini yake lakini wazazi wangu hawataki hata kusikia suala hilo, tafadhali nishauri nifanyeje ili kunusuru ndoa yangu?”
MFANO HUO UNATUFUNDISHA NINI?
Kupitia mfano huo tunaona ni jinsi gani nguvu ya wazazi inavyoweza kupenya kwa vijana wao hadi kufikia hatua ya kukwamisha suala la ndoa. Vijana wamependana lakini kikwazo kinakuwa ni wazazi.
KUNA ULAZIMA WAZAZI KUINGILIA?
Hapa kuna kitu cha kujifunza. Kwanza wazazi wanapaswa kusikilizwa lakini katika suala hili ni vyema wakakupa mwongozo mapema, wasisubiri wakati mambo yameshaharibika.Kama nilivyoeleza awali, wakujengee misingi mizuri, wakufundishe nini unapaswa kufanya pindi unapotaka kuingia katika hatua ya uchumba na baadaye ndoa.
USISITE KUTUACHIA UJUMBE WAKO HAPO CHINI
Post a Comment