Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, muandaaji wa tamasha hilo, Dave Ojay Haashim, alisema madhumuni ya tamasha hilo ni kuwaweka pamoja watu kutoka sehemu mbalimbali duniani ili kusherehekea muziki wa Afrika chini ya anga la Zanzibar ambapo pia kutakuwa na wasanii wa muziki wa kizazi kipya.
Tamasha hilo la 12 tangu kuanzishwa kwake limekuwa likifanyika kila mwaka kwa kuhusisha wasanii kutoka pande mbalimbali za dunia ambao huimba moja kwa moja jukwaani (live) kwa kutumia zana za muziki.
Naye Mkurugenzi wa Busara Promotion, Yusuf Mahmoud, alisema msimu huu jumla ya wasanii na vikundi 680 viliomba kushiriki lakini baada ya mchujo vilibaki vikundi 37 pekee.
Alisema kati yake 19 ni kutoka Tanzania na wengine wanatoka nchi mbalimbali wakiwemo Blitz The Ambassador mwenye asili ya Ghana anayeishi na kufanya kazi zake huko Brooklyn, Marekani.
Pia aliongeza kuwa kutakuwa na filamu maalum kwa ajili ya kumuenzi Fatuma binti Baraka (Bi Kidude ) na kila mshiriki atatakiwa kuimba wimbo wa kuhamasisha amani na watatu watakaoimba vizuri watapewa tuzo pamoja na kitita cha Sh. milioni tisa.
USISITE KUTUACHIA UJUMBE WAKO HAPO CHINI
Post a Comment