Askofu Eusebius Nzigirwa.
WIKI iliyopita niliandika mada juu ya viongozi wa
dini kushindwa kunilisha neno juu ya sakata la Escrow. Nilikosoa
mahubiri yao ya Sikukuu ya Krismasi yaliyoishutumu zaidi serikali katika
ufisadi huku wakiacha kuwazungumzia viongozi wenzao wa dini ambao
wanatajwa kujipatia mgao wa fedha zenye utata.Niliwaambia viongozi wa dini nchini kuwa, siyo sawa kujihusisha na utoaji wa kibanzi kwenye jicho la mwingine na kuliacha boriti lililopo kwenye jicho lao; naam bado naamini hivyo hata leo.
Wakati naandika mada ya wiki iliyopita nilijua kitakachonipata kwa sababu nilithubutu kuwagusa wasiogusika, lakini kwa sababu ya haki nilichagua kwenda Galilaya hata kama huko kuna kifo.
Msimamo wangu kuhusu viongozi wa dini, Askofu Methodius Kilaini (aliyechota Sh 80.9 milioni), Askofu Eusebius Nzigirwa (Sh 40.4 milioni) na Padri Alphonce Twimannye Simon (Sh 40.4 milioni), uko palepale kwamba fedha walizopokea zina harufu ya dhambi.
Pamoja na vitisho kutoka kwa watu wasiojulikana walioniambia kuwa nastahili kutengwa na kanisa kwa sababu nimewanenea mabaya watumishi wa Mungu; nasema niko tayari kwa yote, lakini sitaacha kujadili utakaso wa Kimungu ndani ya kanisa.
Wiki iliyopita siku tatu baada ya kuandika makala ya kuwakosoa viongozi wa dini, Askofu Eusebius Nzigirwa ambaye ni Askofu msaidizi wa Kanisa Katoliki Jimbo kuu la Dar es Salaam, aliibuka na utetezi juu ya upokeaji wa fedha zenye utata kutoka kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya VIP Engireering & Marketing Ltd, James Rugemalila.
Katika utetezi wake Baba Askofu Nzigirwa alisema: “Katika moja ya mawasiliano yetu mwanzoni mwa mwaka jana, Rugemalila aliniomba nimpatie namba yangu ya akaunti ya Benki ya Mkombozi ili aweke matoleo yake.
“Kwa kweli nilimshukuru kwa ukarimu wake mkubwa, kutokana na matoleo hayo kutolewa na mtu anayefahamika kwa ukaribu wake katika kusaidia kanisa na watumishi wake.”
Bila shaka huu ni utetezi dhaifu mno kutolewa na kiongozi wa dini, inawezekanaje matoleo ya muumini yaache kuwekwa kwenye akaunti ya kanisa na badala yake aingiziwe mtu binafsi?
Je, kwa maana ya kusaidia kanisa, inawezekana Askofu Nzigirwa ndiye kanisa kwa tafsiri sahihi? Siamini katika hili, kwa sababu najua sadaka, matoleo na michango ya kanisa kubwa kama la jimbo la Dar es Salaam, huingizwa kwenye akaunti ya kanisa.
Kwa msingi huo, Baba Askofu Nzigirwa anaposimama kuueleza umma kuwa alipewa fedha hizo katika msingi alioueleza namtafsiri kama mtumishi wa Mungu anayetaka kuchuma dhambi juu ya dhambi.
Yuda Eskarioti mwanafunzi anayetajwa kumsaliti Yesu, alipogundua kuwa fedha aliyopewa kama shukrani ya kumtoa mwalimu wake kwa Mafarisayo ambao hatimaye walimua, aliichukia fedha hiyo na kuirudisha kisha kwenda kujinyonga.
Kwa kiongozi mtakatifu hasa, kuendelea kukumbatia fedha inayotajwa kupatikana kwa njia ya dhambi, kuitetea na kuijumlisha kwenye utumishi wa Mungu siyo jambo zuri, Askofu Nzigirwa alipaswa kuichukia fedha hiyo na kurudishwa kwa Rugemalila kwa sababu Mungu hapokei sadaka za wenye dhambi, mfano ya ile iliyotolewa na Kaini enzi za Adamu na Hawa.
Bado nauona uovu katika upokeaji wa fedha za Escrow kwa watumishi wa Mungu licha ya utetezi huo. Maana kama kanisa lina mfumo wa kuruhusu watumishi wake kuingiziwa fedha za matoleo, huwa linafanya nini pale wanapohama vituo? Naiona kasoro hata ya utunzaji wa fedha hizo.
Mwisho nishauri, Kanisa Katoliki nchini litoe tamko juu ya sakata hili ili waumini wapate kujua ukweli, vinginevyo kazi ya Mungu itaharibika na mioyo ya waumini itaugua. Nachochea tu!
USISITE KUTUACHIA UJUMBE WAKO HAPO CHINI.
Post a Comment