Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

WATANZANIA TUMEJIFUNZA MENGI KUTOKANA NA SAKATA LA ESCROW

Zitto Kabwe.
MWANDISHI  Eric Shigongo
MUNGU ni mwema ndiyo maana leo tupo salama na tunapumua tukiwa na afya njema, kwa wale wanaoumwa nawaombea kwake wapate afya njema ili warejee waweze kumtumikia na kumhimidi daima.

Baada ya kusema hayo nianze kwa kusema kuwa suala la pesa za umma zilizokuwa kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow limekuwa gumzo kubwa nchini kwa muda mrefu sasa.
Ukaguzi maalum uliofanywa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na uchuguzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwenye akaunti hiyo, ulimalizwa na ripoti zikatolewa na bunge, likajadili na kufikia tamati kwamba kuna kodi ya umma iliibwa.
Kwa vile suala hili limegusa utendaji wa viongozi wa ngazi za juu serikalini pamoja na wanasiasa wengine, tumejifunza kuwa bunge lilitaka kuyumba kutokana na kupendeleana. Fedha zilizochukuliwa ni nyingi sana na hakika dawa pekee iliyobakia kwa Watanzania ni kuzidai zirejeshwe na wananchi kwa ujumla wetu tupaze sauti kuzidai.
Limekuwa ni jambo la kawaida wezi wa kodi za wananchi kuwajibishwa, kisha kuachwa na fedha za umma, hilo lisifanyike, badala yake wote waliofanya uovu huo warudishe  kodi hiyo. Kipekee nimpongeze Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mwigulu Nchemba kwa kuwapa hadi Desemba 31 wawe
wamerudisha fedha hizo, hakika huyu ndiye kiongozi anayefaa, maana ameweka kando itikadi za kisiasa.
Ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), chini ya Uenyekiti wa Zitto Kabwe ilipitia kwa ufasaha ukaguzi wa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, (CAG)  na uchunguzi wa Takukuru wakatoa ripoti yao na uthibitisho wa kutosha kuwa kuna Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, Waziri wa Madini na Nishati, Profesa Sospiter Muhongo pamoja na watendaji wengine serikalini wamehusika kwa njia moja au nyingine na upotevu wa fedha hizo za Escrow ama kwa kukusudia ama kwa kutojua, kitu ambacho kimeelezwa kuwa ni uzembe.
Kitu ambacho Watanzania wengi tumejifunza na kutushangaza ni kuona baadhi ya wabunge kukaza misuli ya shingo zao na kutetea wizi ili wahusika wasiwajibishwe. Wengine kupingana na ripoti ya CAG, kweli tumefika huko? Kwa nini tuwalinde wezi wa fedha za umma? Tumejifunza kuwa kuna watu ambao hawana uzalendo kabisa.

Spika wa bunge, Anna Makinda.
Sijui kama kuna chembe ya hofu ya Mungu ndani ya wabunge waliokuwa wakitetea wizi huo mkubwa ambao umetikisa ndani na nje ya nchi. Wote wanaotetea wizi huu ni lazima watambue kwamba kumlinda mwizi ni dhambi kubwa mbele ya Mungu aliyesema katika moja ya amri zake; “Usiibe” .
Tumejifunza kuwa wabunge wanaotetea waovu ndiyo wanaosababisha bunge kuvurugika na kuonekana kuna ukosefu wa nidhamu bungeni kwa sababu baadhi ya wabunge wazalendo hawakubali kuungana na wanaosema haya ni maziwa wakati kila mmoja anaona kuwa ni uji, hali inayompa shida aliyekaa kwenye kiti siku hiyo kuliongoza bunge.
Ni lazima sasa Watanzania wamueleze Rais wetu mpendwa Jakaya Kikwete kwamba sasa tumechoka kuendelea kuwalinda wezi wa mali ya umma. Navyo vyama vya siasa, vipaze sauti bila kukoma kukemea viongozi tunaowapa dhamana ya uongozi  kufanya usaliti huu wa  nchi.
Viongozi wa dini zote waitishe maombi, sala na kutoa mafundisho juu ya madhara ya wizi na ufisadi uliokatazwa na maandiko matakatifu. Waonyeshe jinsi Mungu anavyochukizwa na wala rushwa wanaowadhulumu wanyonge na maskini.
Nashauri viongozi wa dini kwa niaba ya waumini wao kwa pamoja wapeleke ujumbe kwa Rais Kikwete, kumtaarifu ubaya wa wizi wa aina hii unaosababisha nchi kukosa misaada ya kimaendeleo kutoka kwa wafadhili kwa sababu ya watu wachache wenye roho mbaya.
Waumini wa madhehebu ya dini yote nchini wanaunda kundi kubwa sana la wanajamii ya Watanzania, hivyo  viongozi wao wanao wajibu wa kuonyesha kwamba wanakerwa na kuchukizwa na wizi wa fedha za umma kama huu wa Escrow.
Nchi yetu imefika pabaya, bila kujali imani yako, itikadi ya kisiasa, kabila, rangi, cheo, elimu na kipato chako wote tupaze sauti kwa pamoja kwamba wezi hawa wa fedha za umma wazirejeshe, lakini pia wachukuliwe hatua za kisheria.
Wabunge waliopewa jukumu la kuishauri serikali na kuisimamia chini ya Spika Anne Makinda nao watimize wajibu wao bila kuingiza urafiki au itikadi linapokuja jambo muhimu la kitaifa, naami wale wote waliokuwa wakitetea wizi huu bungeni wamejifunza kitu na hivi sasa wanainamisha vichwa vyao chini kwa aibu.

Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.
chanzo; GPL
USISITE KUTUACHIA UJUMBE WAKO HAPO CHINI.

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
© Copyright BONGO HABARI
Back To Top