Jumanne yetu ya leo tutakuwa na mada isemayo ‘wanaoficha ‘makucha’ kabla ya ndoa ni hatari zaidi’.
Nimelifungia neno ‘makucha’ kwa sababu kimazoea tunaita hivyo lakini kiuhalisia si makucha ni kucha. Zikiwa nyingi, ikiwa moja ni kucha!
Kuna wanaoficha makucha kabla ya ndoa ni msemo au hoja ambayo ipo miongoni mwa jamii yetu! Wengi hudai wapo wanawake au wanaume wenye tabia hii! Kwamba, kabla hajaolea au hajaoa anaonesha tabia tofauti na ile akishaolewa au kuoa.
NINI MAANA YA KUFICHA MAKUCHA
Kwanza kabisa naomba ijulikane maana ya kuficha makucha. Kuficha makucha ni ile tabia ya mtu kutotaka kuonesha tabia yake ya asili na kuonesha tabia bandia.
KIPENGELE CHA KWANZA
Jamii tunayoishi kuna watu wamelelewa na kukua kwa tabia za kuwa wagomvi, wasemaji sana, wasiotaka suluhu, wasiojiheshimu wala kuheshimu wengine nakadhalika.
KIPENGELE CHA PILI
Lakini pia, wapo waliolelewa kwa tabia ya kuheshimu watu, kuwapenda, kuwanyenyekea na wasikivu achilia mbali kusamehe na kusahau.Sasa chukua mtu mwenye tabia ya kipengele cha kwanza awe anafanya mambo ya kipengele cha pili. Mtu huyo ndiyo atakuwa ameficha makucha sasa! Siku akiamua na kurudia mambo yake ya kipengele cha pili ndiyo anakunjua makucha!
ZAIDI SANA!
Hata hivyo, wanawake ndiyo wanatajwa sana kuwa na tabia hii. Kwamba, kuna mwanamke wakati wa uchumba huonesha heshima kubwa kwa mumewe mtarajiwa, lakini akishafunga pingu za maisha huanza polepole kuonesha tabia yake ya asili.
Utafiti wangu umeonesha kuwa, kuna wanaume wengi wanajikuta wakitamani kuacha wake zao, sababu wanasema wamebadilika tabia ghafla, lakini ukweli si kubadilika tabia ghafla bali wamerudi kwenye kipengele kinachowahusu!
KUNDI HILI PIA
Pia wapo wanaume wenye tabia hiyo, japo hawatajwi sana kama wanawake. Na wao, kabla ya ndoa wanakuwa na tabia tofauti na wakishafunga ndoa. Mifano ya wengi ipo kwenye kulewa sana, kutolala nyumbani au kupiga!
Japokuwa mchanganuo uliopita pia unahusiana na tabia za mabadiliko ya ndani ya nyumba. Asilimia kubwa ya wanaume wamebobea kunywa pombe baada ya kuoa. Hii ni kutokana na kukumbana na kero mbalimbali kwa mwanamke aliyeamua kukunjua makucha yake!
KINACHOSEMWA
Nilibahatika kuzungumza na watu mbalimbali katika jinsi zote, ikaonekana kuwa kwa wanawake na wanaume pia, wengi wanakuwa na tabia ya kukunja makucha wakijua wana tabia zisizoweza kukubalika na mwenzake.
Wengi wanaamini kuwa, kuonesha tabia ya asili, kwamba yeye si mwaminifu au si mwadilifu kwa mambo mbalimbali kunaweza kumfanya mwenza wake kughairi kufunga naye ndoa.
Pia inasema kuwa, ujasiri wa wengi kukunjua makucha huja baada ya ndoa kufungwa, hasa kwa Wakristo kwa vile wanaamini ndoa zao kuvunjika ni vigumu sana hoja ambagyo huwasumbua wengi kwenye uhusiano matokeo yake mke au mume hugeuka kuwa mzigo au msalaba kwa mwenzake.
HATARI YAKE NINI?
Ni vyema wakati wa uchumba, wawili wakaamua kuanikana tabia ili kama mtu ataamua kuingia basi aamue huku akijua kuliko kufichiana makucha kwa sababu ya kuamini hataweza kuolewa halafu baada ya ndoa yanaonekana mazito ni hatari sana kwani lolote linaweza kutokea, hata kuuana au kupeana vilema vya maisha baada ya mwingine kuchoshwa na tabia ambazo hakutarajia kuziona kwa mwenza wake!
USISITE KUTUACHIA UJUMBE WAKO HAPO CHINI.
Post a Comment