Andrew Chenge.
Kwako Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge.Najua hunifahamu na hakuna mazingira yanayoweza kutukutanisha pamoja lakini hiyo hainizuii kukufishia ujumbe wangu kwako, najua ‘utamaindi’ lakini ni lazima nikwambie kwa faida yako na ya Watanzania.
Mheshimiwa, mimi sikuzaliwa Desemba 24, 1947 kama wewe. Sikusoma Shule ya Msingi Zagayu kama wewe. Sikusoma Sekondari ya St. Mary’s Junior Seminary iliyopo Nyegezi, Mwanza wala sikwenda kusoma kidato cha tano na sita kwenye Sekondari ya Mkwawa High School, Iringa.
Nakuhakikishia kwamba sijawahi kusoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ulikopata shahada ya kwanza ya sheria (Legum Baccalaureus au kwa kifupi LL.B) na baadaye kwenda kuchukua ‘mastaz’, Chuo Kikuu cha Harvard nchini Marekani. Sijawahi kuwa mwanasheria mkuu kama wewe wala sina mpango wa kuja kugombea ubunge au kushika wadhifa wowote serikalini.
Mimi ni ‘mburula’ tu, nisiyejua chochote kuhusu sheria, utawala wala sina CV yoyote ya maana ya kujivunia kama wewe. Hata hivyo, licha ya ‘umburula’ wangu, nakuhakikishia kwamba ningekuwa mimi kwenye nafasi yako, kwa huu mfululizo wa kashfa nzitonzito zinazokukabili, sikufichi, nisingesubiri kuwajibishwa, tayari mwenyewe ningeshaachia ngazi.
Tayari ningeshaamua kujiondoa mwenyewe kwenye nyadhifa zote ninazozishikilia kwani ningekuwa najua kwamba cheo ni dhamana na kama walionipa dhamana hiyo (wananchi), hawaniamini tena, hakuna haja ya kung’ang’ania bali busara ni kuepusha mbawa zangu mapema.
Mheshimiwa, kwa nini katika kila kashfa kubwa za ufisadi na mikataba mibovu zinazozuka nchini lazima jina lako litajwe? Ulianza kutajwa kuanzia kwenye mkataba mbovu wa Meremeta Gold Mine, ukatajwa kwenye ununuzi wa ndege ya rais, ukatajwa kwenye ununuzi wa rada na kama hiyo haitoshi, jina lako likawa miongoni mwa watuhumiwa wakubwa katika sakata la EPA.
Kipindi kile ukiwa mwanasheria mkuu wa serikali, ‘ukatisha’ tena baada ya kuruhusu sheria ya kutoa takrima ambayo baadaye ilifutiliwa mbali baada ya kubainika kuwa takrima ni rushwa iliyobadilishwa jina!
Kwenye uandishi wa rasimu ya katiba mpya inayopendekezwa, ukiwa kama Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi ya Bunge, ukatajwa tena kuwa miongoni mwa vinara waliofanya kazi ya kunyofoa vipengele muhimu kabisa vya maadili, ukomo wa ubunge na kuondoa nguvu ya wapiga kura kuwawajibisha wabunge mizigo.
Yote tisa, kumi ni hili sakata linaloendelea kuitingisha nchi la mabilioni ya fedha za Escrow ambapo unatajwa kuvuta ‘mtonyo’ wa maana. Mheshimiwa, hayo yote hayatoshi kukufanya ugundue kwamba umeshindwa kuitumia vyema dhamana ya vyeo vyote unavyopewa?
Inatosha ‘mzee wa vijisenti’, jiweke pembeni kwani siku Watanzania wanaoteseka kwenye lindi la umaskini watakapoamua kuonesha hasira zao, sidhani kama utasalimika. Nguo ikimvuka, muungwana huchutama.
Wasalaam.
USISITE KUTUACHIA UJUMBE WAKO HAPO CHINI.
Post a Comment