- Balozi Sefue asema Rais Kikwete ataamua hatima yake wakati wowote, Profesa Muhongo akataa kuzungumzia hatima yakeDar es Salaam/ Zanzibar. Licha ya watu mbalimbali kutaka Rais Jakaya Kikwete kumwajibisha Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kuhusiana na sakata la fedha za escrow, Ikulu imesema suala hilo litatolewa uamuzi wakati wowote baada ya mapumziko ya sikukuu.
Hivi sasa Rais yupo katika mapumziko ya Sikukuu za
Krismasi inayosherehekewa Desemba 25 kila mwaka na Mwaka Mpya
itakayofanyika Januari Mosi.
Akizungumza na wazee wa Dar es Salaam Desemba 22
mwaka huu, Rais Kikwete alisema amemweka kiporo waziri huyo hadi
atakapopata ufafanuzi wa mambo kadhaa na kwamba atakapojilidhisha
ataujulisha umma.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue
aliliambia gazeti hili jana kuwa Rais Kikwete bado hajakamilisha
kulishughulikia suala hilo na kwamba litakapokuwa tayari wananchi
watajulishwa hatua alizozichukua.
“Unakumbuka Rais alichosema? Bado analifanyia
kazi, atakapomaliza tu mtajulishwa, sasa hivi ni kipindi cha sikukuu,”
alisema Sefue.
Profesa Muhongo
Hata hivyo, Profesa Muhongo alipotakiwa
kuzungumzia shinikizo linalotolewa la kutaka ajiuzulu kabla ya Rais
Kikwete kutoa uamuzi wake, aliliambia gazeti hili jana kwa simu kuwa;
“Mimi sasa sitaki kuzungumza na waandishi, mambo yangu yote wapo watu
ambao wanaweza kuyazungumzia.”
Hata hivyo, katika hotuba yake, Rais Kikwete
aliagiza kuchukuliwa hatua kwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya
Nishati na Madini, Eliakimu Maswi ili kupisha uchunguzi wa tuhuma kuhusu
ushiriki wake kwenye kashfa hiyo.
Siku iliyofuata, Sefue alimweka ‘kando’ Maswi na
kumteua Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, Ngosi Mwihava
kukaimu nafasi hiyo hadi uchunguzi utakapokamilika.
Kutokana na kuchelewa kutekelezwa kwa maazimio ya
Bunge yaliyotaka viongozi hao kuwajibishwa, Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa) umeahidi kuwasilisha hoja bungeni ya kupiga kura ya kutokuwa na
imani na waziri mkuu na kufanya maandamano nchi nzima.
Mpaka sasa viongozi watatu wameshakumbwa na
dhoruba inayotokana na sakata la escrow baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa
Mwanasheria Mkuu, Jaji Frederick Werema, kung’olewa kwa Waziri wa
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka na kuwekwa
kando kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Maswi.
Vyama vya upinzani Zanzibar vimeshangaa kitendo cha Rais Kikwete
cha kutomwajibisha Waziri Mkuu Mizengo Pinda, wakati huko nyuma kuna
mawaziri akiwamo Waziri Mkuu waliwajibika kwa makosa yaliyofanywa na
watendaji wao.
Katibu Mkuu wa Chama cha Tadea, Juma Ali Khatibu
alisema kwamba kuna viongozi wengi ambao walilazimika kujiuzulu kwa
makosa ambayo hawakuhusika lili kulinda misingi ya uwajibikaji wa pamoja
na kushangaa serikali kuendelea kumlinda Waziri Mkuu Mizengo Pinda,
wakati kashfa hiyo imetia hasara taifa baada ya wahisani kusitisha
misaada yao.
Alisema kwamba kama Rais Kikwete ameamua kumuachia
Waziri Mkuu kuendelea na wadhifa wake wakati umefika kwa Serikali
kuwaomba radhi viongozi wote ambao walijiuzulu nyadhifa zao kwa makosa
ya wengine.
Upande wake Makamu Mwenyekiti wa Chadema Zanzibar,
Said Issa Mohamed alisema kwamba licha ya kuwa Waziri Mkuu Mizengo
Pinda, hakuhusika kuchota fedha hizo. lakini alitakiwa kujiuzulu ili
kulinda heshima yake na kupunguza hasira za wananchi.
“Kwa heshima ya misingi ya Utawala bora Kiongozi
hata kama hukuhusika moja kwa moja, unalazimika kuwajibika kulinda dhana
ya uwajibikaji wa pamoja.” alisema Mohamed.
Upande wake Mkurugenzi wa Uenezi na Mawasiliano ya
Umma wa CUF, Salim Bimani Abdalla alihoji ni kigezo gani kilichomfanya
Mzee Ali Hassan Mwinyi akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Abdallah
Said Natepe (marehemu), Shamsi Vuai Nahodha, Dk Emanuel Nchimbi na
Balozi Khamis Kagasheki wajiuzulu lakini Pinda abaki katika Ofisi za
umma.
Mwinyi hakuwapo wakati mauaji yaliotokea mkoani
Shinyanga, Natepe hakujua kama kina Pius Lugangira, Hatibu Gandhi na
Christopher Kadego waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya uhaini kama
wangetoroka katika Gereza la Ukonga.
Nahodha, Dk Nchimbi na Balozi Kagasheki pia
hawakuhusika wala kufika katika eneo la utesaji wa watu wakati
utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili.
Bimani alisema kwamba viongozi wote walioguswa na
kashfa ya escrow wanatakiwa kufukuzwa, kushtakiwa na mali zao
kutaifishwa na Serikali na kusisitiza kama serikali itashindwa kazi hiyo
itafanywa na Ukawa mara baada ya kuingia madarakani mwakani.
Makamu Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, Ambar Khamis
Haji alisema kwamba maamuzi ya Rais Kikwete yameshindwa kumaliza kiu ya
Watanzania wengi waliokuwa wakisubiri kuona viongozi waliohusika na
kashfa ya escrow wanafukuzwa na kufikishwa mahakamani na mali zao
kutaifishwa.
Alisema kinachoonekana sasa Serikali imeamua
kuwalinda wahalifu, kitendo ambacho hakitasadia kujenga misingi ya
utawala bora pamoja na kufanikisha vita dhidi ya rushwa na ufisadi.
Haji alisema kwamba ni jambo la kushangaza Rais
Kikwete amekuwa mzito kutekeleza uamuzi ya Bunge, wakati Serikali ni
sehemu ya bunge na ilishiriki katika kupitisha maazimio hayo baada ya
kamati za uchunguzi kuwasilishwa ripoti za uchunguzi.
Wapinzani Zanzibar wakoleza moto
CHANZO; MWANANCHI.
CHANZO; MWANANCHI.
USISITE KUTUACHIA UJUMBE WAKO HAPO CHINI.
Post a Comment