Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

SIMULIZI TAMU YA KHADIJA KOPA - 8

 
ILIPOISHIA..
Bado Khadija anaendelea kusimulia historia ya maisha yake. Ametoka mbali, ameishia pale alipojiunga na Bendi ya Culture Music All Club ambayo ilikuwa ikitumbuiza Zanzibar tu.
Hapo ndipo uwezo wake ulipoonekana zaidi na kuwachanganya kabisa watu.
ENDELEA...

 
Malkia wa mipasho bongo khadija omari kopa.
Naendelea kuyakumbuka maisha yangu, kila ninapojiangalia na kuona hapa nilipofika, huwa ninamshukuru sana Mungu kwa kuniongoza na kunifanikisha kuwa hapa nilipo. Nilipitia mengi, wengi walinivunja moyo lakini niliendelea kusonga mbele na mwisho wa siku, leo hii nakula matunda ya kipaji changu cha kuimba.
Niliendelea kuimba ndani ya kundi hilo, mara nyingi tulikuwa tukiitwa katika sherehe mbalimbali za viongozi na wakati mwingine kuanzisha matamasha yetu wenyewe ambapo watu waliingia kwa viingilio na kupata burudani.
Sifa za sauti yangu hazikuishia hapo, hata watu walioingia katika matamasha ambayo kundi letu lilikuwa likitumbuiza, nilikuwa nikisifiwa sana, taratibu nikaanza kuwa maarufu, hiyo ilikuwa mwaka 1991. Kitambo sana ila bado nakumbuka mengi.
Kwa kiasi fulani, bendi hiyo ikaanza kunipa jina, tulikuwa tukiimba sehemu mbalimbali hapo Zanzibar. Katika kila hatua ambayo nilikuwa nikipiga bado kichwa changu kilikuwa kikifikiria kuyafikia mafanikio aliyokuwa nayo Bi. Kidude.
Nilihitaji heshima, maskini mimi, nilitaka kuwa na fedha hapo baadaye kwani maisha niliyokuwa nimepitia kipindi cha nyuma sikutaka yanirudie tena, yaani pale ambapo ningeanza kupiga hatua za mafanikio, basi iwe mpaka ninafukiwa katika kaburi langu.
“Kuna safari nyingi sana tutafanya, cha msingi tuendeleeni tu kuimba sehemu mbalimbali,” alituambia kiongozi wetu.
“Kwa hiyo kuna safari nyingi zinakuja?” niliuliza.
“Ndiyo. Cha msingi ni kuongeza juhudi sana, tukifanikiwa, nakuahidini kwamba malipo yatakuwa makubwa zaidi ya haya mnayoyapata,” alituambia kiongozi huyo.
“Na hatuwezi kwenda Bara?”
“Huko tunaweza kufika, na ndiyo maana nimewaambia muongeze juhudi. Ninataka siku ya kwenda huko tuwe na moto mkubwa kwani staili ya nyimbo hizi zimekwishaanza kuingia huko, tukichezacheza tu, hatutofanikiwa,” alituambia kiongozi wetu.
Kila mmoja wetu alikuwa na kiu ya kusonga hapo tulipokuwa, hakukuwa na mtu aliyeridhika na pale alipokuwa kwa kipindi hicho, tuliendelea kufanya mazoezi kwani bado tulihitaji kuwa bora kuliko bend zote nchini Tanzania.
Katika kila hatua tuliyokuwa tukipitia, bado jina langu lilikuwa likisikika sana. Kiukweli nikatokea kupendwa na wengi kutokana na sauti yangu ilivyokuwa nzuri kipindi hicho. Kupitia muziki, kuna wanaume ambao walinifuata huku wakiniambia maneno matamu ya kutaka kuwa nami lakini nilikuwa mgumu sana.
Sikujisikia kuingia kwenye mahusiano, bado akili yangu niliiweka katika muziki tu. Nilihitaji kufanikiwa, kitendo cha kuwa na mahusiano ya kimapenzi na mwanaume niliona ingekuwa njia mojawapo ya kuniangusha pale nilipotaka kufika.
Nisingekuwa huru kama nilivyokuwa, hata kama ningekuwa na ratiba ya kusafiri na kundi sehemu fulani, mume wangu asingeniruhusu, hivyo nilihofia kuingia katika mahusiano ya kimapenzi na kufunga ndoa.
“Unaogopa nini sasa?” aliniambia mwanaume mmoja, alikuwa na asili ya Kipemba, aliongea kwa sauti ya utaratibu sana, kwa kumwangalia, alionekana kuwa mwanaume aliyejiheshimu sana.

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
© Copyright BONGO HABARI
Back To Top