Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

MKURUGENZI WA MUFINDI MATATANI, KWA TUHUMA ZA UBADHILIFU WA MILIONI 291

Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mufindi, Paulo Ntinika (mwenye bluu) alipokuwa akisikiliza tuhuma dhidia yake
Akajaribu kujitetea lakini hakueleweka
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, Peter Tweve (aliyekunja ngumi) akisistiza makosa ya baadhi ya watumishi wa halmashauri hiyo
Mweka Hazina wa halmashauri hiyo, Athumani Kihamiya ambaye sasa ameteuliwa kukaimu nafasi ya ukurugenzi
Fedha hizo, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa wanahabari na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Peter Tweve zinahusu kazi za ujenzi zilizoongezwa na watendaji wa halmashauri hiyo kinyume na maelekezo ya sheria ya manunuzi namba 40(1) ya mwaka 2005.
Katika kikao hicho kilichofanyika juzi, baada ya madiwani wa halmashauri hiyo (wote wa CCM) kujadili suala hilo katika kikao cha chama chao siku moja kabla, baadhi yao walisikika wakitoa kauli zinazomkataa mkurugenzi huyo.
Na wengine (bila kutaja majina yao) waliomba vyombo vya dola vimchukulie hatua za kisheria kwa madai kwamba za kinidhamu pekee hazitoshi kutoa onyo kwa wengine.
Kabla ya kikao hicho hakijafikia maamuzi dhidi ya wahusika wote waliosababisha hasara ya fedha hizo, hali ya kiafya ya Ntinika ilidaiwa kubadilika ghafla jambo lililosababisha akimbizwe katika hospitali ya wilaya hiyo kwa ajili ya matibabu.
Baada ya kupewa ushauri na matibabu, Ntinika ambaye ni kama amepumzishwa kwa muda usiojulikana kuendelea na majukumu yake hayo ili kupisha kilichoelezwa na Mwenyekiti wa halmashauri hiyo "uchunguzi utakaoainisha wahusika wote wa ubadhilifu wa fedha hizo" hakurudi tena katika kikao hicho kilichomteua mweka hazina wa halmashauri hiyo, Athumani Kihamiya kukaimu nafasi ya ukurugenzi.
Wakati hayo yote yakitokea wanahabari waliohudhuria kikao hicho, walitolewa nje baada ya baraza hilo la kawaida kugeuzwa na kuwa kamati maalumu ya baraza hilo iliyojadili taarifa ya kamati ya ukaguzi ya wilaya kwa siri.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya ukaguzi ya Julai Septemba 2014/2015 ambayo nakala yake tunayo, baadhi ya barabara zinazohusishwa na malipo ya nyongeza ni pamoja na ya Kibengu hadi Kipanga yenye urefu wa km 37, barabara ya Kipanga B hadi Uhafiwa na barabara ya Mkuta Ludilo hadi Ilasa yenye km 21.
Kwa mfano, barabara ya Kibengu Kipanga, taarifa hiyo ya ukaguzi inaonesha Januari 1, 2014 kikao cha zabuni kilikaa na kutoa kazi ya nyongeza yenye thamani ya Sh 21,876,500 kwa ajili ya matengezo yake na kufanya thamani ya kazi yote kuwa Sh 313,956,500.
Hata hivyo taarifa hiyo inaeleza badala ya Sh 21,876,500 iliyopitishwa na bodi ya zabuni, kazi hiyo iliongezwa Sh 85,029,500.
"Kama halmashauri tumeazimia wahusika wote waliofanya matumizi nje ya utaratibu wachukuliwe hatua za kinidhamu. Wakati hayo yakiendelea tunaomba wananchi wawe na subira kuona ni taratibu zipi zitafuatwa," alisema.
Alisema kamati ya fedha ndiyo itakayofanya kazi ya kuainisha watumishi wanaohusika na tuhuma hiyo na kwamba taarifa yake ya kile kitakachopatikana itatolewa Novemba 24.
Tweve alisema halmashauri hiyo itatoa taarifa kwa mamlaka zingine zinazohusika ili wahusika watakaobainika kuhusika wachukuliwe hatua nyingine za kisheria.
Alisema sula la mkurugenzi wa halmashauri hiyo kuendelea au kutoendelea na nafasi yake hiyo litaamliwa na mamlaka za juu ambazo tayari zimejulishwa kuhusu kile kinachoendelea wilayani humo.
"Jambo muhimu ni kwamba, katika kujiridhisha na tuhuma hizi, tumebaini kuna mambo hayakufuatwa kwa mujibu wa taratibu na sheria. Kwahiyo kama mkurugenzi , mhandisi au mhasibu na yoyote yule ambaye ni mtumishi wa halmashauriikithibitika amehusika watachukuliwa hatua za kinidhamu," alisema.
Akizungumzia utaratibu wa sheria ya manunuzi Tweve alisema wakandarasi huingia mikataba na halmashauri baada ya kushinda zabuni zilizotangazwa.
"Kwa mujibu wa sheria wanakandarasi wanatakiwa kufanya kazi zilizopo kwenye mkataba na kwa malipo yaliyopangwa na kama kuna kazi ya nyongeza mkuu wa idara anatakiwa apeleke maombi kitengo cha manunuzi kitakachoitisha kikao cha bodi ya manunuzi ili kilidhie nyongeza ya kazi," alisema
Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, aliwataka wananchi wawe wavumilivu akiwaahidi ufumbuzi wa suala hilo kujulikana katika kipindi kilichowekwa.

USISITE KUTUACHIA UJUMBE WAKO HAPO CHINI.

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
© Copyright BONGO HABARI
Back To Top