Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

KAMAUNAMPENDA MVUMILIE, KAMA KUACHA UTAACHA WANGAPI

 
Mpenzi msomaji wangu, huko mtaani kuna watu ambao wamekuwa wakipachikwa majina mabaya kutokana na tabia zao. Wapo ambao wanaitwa malaya kwa sababu kila mara wamekuwa wakibadili wapenzi.

Unamkuta leo yuko na f’lani, kesho unaambiwa kahamia kwa mwingine. Si ajabu ndani ya muda mfupi akawa ameshatoka na idadi kubwa ya wapenzi.Kimsingi kuna wale ambao wanastahili kuitwa majina hayo mabaya kwa kuwa kubadili kwao wapenzi hakuna sababu za msingi, yaani wao wanaangalia wenye pesa, akishamchuna huyu, anaenda kwa mwingine. Hao ndiyo malaya.
Lakini kuna wale ambao kubadilisha kwao wapenzi ni kutokana na kila wakati kuingia kwenye uhusiano na watu ambao siyo sahihi.

 Mathalani unaweza kukuta msichana leo katokea kumpenda jamaa f’lani, bila kumchunguza vizuri anamkabidhi moyo wake. Baada ya siku chache msichana anagundua mwanaume huyo siyo sahihi kutokana na tabia zake. Anamuacha na bila kuchelewa anahamia kwa mwingine.

Tabia hiyo ndiyo ninayotaka kuizungumzia leo na kiukweli itakuwa si jambo zuri kama kila siku utakuwa ukibadili wapenzi, kisa eti umechoshwa na tabia zao.
 Katika mapenzi kuna kitu kinaitwa uvumilivu. Kila mwenye moyo wa kupenda lazima awe tayari kuvumilia changamoto utakazokumbana nazo.

Kwa mfano unaweza kuingia kwenye uhusiano na mtu ambaye anaonekana hajatulia, huenda ni mtu wa kuchepuka sana, anaweza kuwa ni mlevi kupindukia au ni mkali ambaye hata kwa jambo dogo anafoka.
Katika mazingira hayo, ni mvumilivu tu ndiye anayeweza kudumu na mtu wa sampuli hiyo, kinyume chake ni kwamba utaona huyo ni mtu asiyestahili kuendelea kuwa na wewe na utaamua kumuacha.
Mbaya zaidi utamuacha huyo, utahamia kwa mwingine ambaye naye huna uhakika kama atakuwa ametulia kama unavyotaka. Hata kama atakuwa si mkali, siyo mlevi wala mpenda totozi sana, unaweza kujikuta umehamia kwa mwingine ambaye ana kasoro kubwa za kimaumbile, huyo naye si utaamua kumuacha?

 Ikiwa hivyo unadhani utaacha wangapi? Unadhani utampata ambaye hana kasoro yoyote? Kifupi hakuna! Kila unayemuona yupo kwenye uhusiano kuna mambo mengi anavumilia, si kwamba ni mjinga asiye na pa’ kwenda, anafanya hivyo akiamini uvumilivu wake ni sehemu ya upendo kwa huyo mwenye mapungufu.

Ifahamike tu kwamba, ukiwa na moyo kwa kukata tamaa haraka, huwezi kumpata mpenzi wa kukupa furaha kwenye maisha yako. Hata kama anakukosesha amani vipi, endelea kumpa nafasi huku ukijaribu kumbadilisha, naamini kadiri siku zinavyokwenda ndivyo atakavyokuwa anaacha tabia moja baada ya nyingine.


Naandika haya nikiwa na mifano mingi ya watu ambao waliingia kwenye uhusiano, wakakutana na changamoto nyingi nzito lakini wakavumilia na leo hii wanaishi maisha ya raha mustarehe.
 Kwa maana hiyo usione wapenzi au wanandoa wanatembea barabarani wameshikana mikono huku wakiwa na furaha ukadhani hawana yanayowakera. Wanayo mengi ambayo wakati mwingine hujikuta wakitamani kutokana lakini wanapingana na mawazo hayo na kuona ni ya kawaida katika maisha ya kimapenzi.

Ni wangapi huko mtaani kwenu hawaishi kupigwa na wapenzi wao kila siku sambamba na kutukanwa pale waume zao wanaporudi usiku wa manane wakiwa wamelewa?

 Ni wangapi ambao unawajua wapenzi wao ni wazinzi wa kutupwa na wakiulizwa wanakuwa wakali lakini bado wako pamoja? Unadhani wanaoyavumilia hayo hawana kwa kwenda au ni wajinga?
 Sidhani kama ni hivyo, mapenzi yao ya dhati waliyonayo dhidi ya wale wanaowatenda ndiyo yanayowafanya waendelee kuwakumbatia. Hata wao wanajua siku uvumilivu ukiwashinda hawatakuwa na sababu ya kuendelea kung’ang’ania penzi la manyanyaso yasiyo na mwisho.

Nihitimishe kwa kusema kwamba, najua kuna watu wakorofi ambao huyageuza mapenzi kuwa shubiri. Wanapendwa lakini hawathamini kupendwa huko. Wanaona kwa kuwa wanapendwa hata wafanye nini hawataachwa, hawa watakuwa wanajidanganya.

Uvumilivu nao una kikomo chake, ukiona kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele mwenza wako ndiyo anazidi kukupa presha, yaani badala ya kukupa furaha anakupa karaha, badala ya kukupa vinono anakupa vichungu, huyo muache na wala usijali maneno ya watu, mwisho wa siku ni wewe na maisha yako.
 Tukutane tena wiki ijayo.

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
© Copyright BONGO HABARI
Back To Top