Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.
Baada ya kusema hayo niseme wazi tu kwamba Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar ni suala ambalo limekuwa likiitesa Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na ile Serikali ya Mapindizi ya Zanzibar (SMZ) kwa
miaka mingi na kuzisababishia kuingia hasara kwa kuunda kamati au tume
mbalimbali kushughulikia kero za muungano huo kwa gharama kubwa.Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejikuta ikiingia katika mkondo wa kuunda tume na kamati nyingi zaidi kuliko Serikali ya Muungano kushughulikia jambo hilo. Serikali zote zinapounda kamati au tume juu ya mambo mbalimbali ya kiserikali, suala la muungano ‘huchomekwa’ viongozi wake wanapokutana na wananchi.
Suala hilo limekuwa likiibuka katika mijadala mikubwa ya kikatiba na kisiasa nchini, kwa upande mwingine katika uendeshaji wa shughuli za serikali za kila siku na matatizo na vikwazo kadhaa ya kiutawala na kiutendaji, vimekuwa vikiripotiwa kila mara kwamba vinakwamisha uimarishaji wa Muungano.
Tume na kamati kadhaa zimeundwa kuainisha matatizo ya Muungano na kupendekeza njia za kuyatatua. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeunda tume na kamati ambazo pamoja na mambo mengine, zilijikita pia kuzungumzia na kuandika ripoti kuhusu suala la muungano.
Baadhi ya kamati hizo ni Kamati ya Mtei, Tume ya Jaji Francis Nyalali mwaka 1991, Kamati ya William Shellukindo ya mwaka 1994, Kamati ya Shellukindo ya pili ya kuandaa muafaka juu ya Mambo ya Muungano baina ya SMZ na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kamati ya Jaji Mark Bomani ya mwaka 1995, Kamati ya Jaji Robert Kisanga ya mwaka 1998 na kadhalika.
Nayo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ‘imeteseka’ zaidi kwani imetia fora kwa kuunda kamati ambazo zimejadili kero za muungano bila mafanikio.
Kamati ilizounda ni Kamati ya Baraza la Mapinduzi (Kamati ya Amina) (1992), Kamati ya Rais ya Kupambana na Kasoro za Muungano (Kamati ya Shamuhuna) (1997), Kamati ya Rais Kuchambua Ripoti ya Jaji Kisanga (Kamati ya Salim Juma Othman), Kamati ya Kuandaa Mapendekezo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Juu ya Kero za Muungano (Kamati ya Ramia) (2000).
SMZ iliunda pia Kamati ya Baraza la Mapinduzi Juu ya Sera ya Mambo ya Nje, Kamati ya Rais ya Wataalamu Juu ya Kero za Muungano (2001), Kamati ya Baraza la Mapinduzi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Kamati ya Mafuta, Kamati ya Madeni Baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Muungano wa Tanzania, Kamati ya Suala la Exclusive Economic Zone (EEZ), Kamati ya Masuala ya Fedha na Benki Kuu, Kamati ya Rais ya Masuala ya Simu (1996 –1999), Kamati ya Baraza la Mapinduzi Juu ya Matatizo na Kero za Muungano na Taratibu za Kuyaondoa (2004).
Ukiacha tume, kamati na ripoti hizo, kuanzia mwaka 1985 kulianzishwa utaratibu wa Kamati ya Pamoja ya Waziri Mkuu na Waziri Kiongozi wa Zanzibar pamoja na Mawaziri wa Serikali zote mbili ambayo ilitarajiwa iwe ndiyo jukwaa la kuzungumzia matatizo kutoka kwa washiriki wakuu wa muungano huu na kuyapatia ufumbuzi unaofaa, lakini nayo iligonga mwamba.
Utaratibu huu uliachwa kwa muda mrefu lakini sasa umerejeshwa upya kufuatia agizo la Rais Jakaya Kikwete alilolitoa katika mkutano na mawaziri na watendaji wakuu wa serikali yake huko Ngurdoto, Arusha Februari, 2006.
Mikutano hiyo sasa imebadilishwa utaratibu wake na inaongozwa na kusimamiwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano na timu za pande mbili zikiongozwa na Waziri Mkuu na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mikutano, makongamano, semina zimefanywa kujadili masuala ya muungano na kupendekeza hatua za kuchukuliwa lakini bado kuna malalamiko na ndiyo maana nasema serikali hizo zimeteseka sana na suala la muungano wa nchi zetu mbili hizi.
Ndugu zangu siyo siri, wasomi mbalimbali wameona kuna kasoro katika muungano wetu na kupendekeza kuboreshwa lakini jambo hili limekuwa kama donda ndugu maana hata Bunge Maalum la Katiba limevurugika kwa baadhi ya wajumbe kususa na wengine wamo ndani lakini suala la Muungano likiibuka kutoka nje ya vikao.
Hii maana yake ni kwamba bila kuwa na mikakati inayokubalika na watu wa pande zote mbili za muungano, suala hili litakuwa kama jini ambaye hakamatiki, viongozi wa serikali walione hili.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.
chanzo;GPL
Post a Comment