Dodoma. Pendekezo la Rasimu ya
Katiba kuwa wabunge walau wawe na elimu ya kidato cha nne limetupiliwa
mbali na wajumbe wa Bunge Maalumu, baada ya Kamati karibu zote
kulikataa.
Kamati hizo zimependekeza kigezo cha elimu kuanzia
walau kidato cha nne kama sharti muhimu la mtu anayetaka kugombea
Ubunge kiondolewe, badala yake mgombea ama ajue tu kusoma na kuandika,
au ajue kusoma na kuandika Lugha ya Kiswahili au Kiingereza kama ilivyo
kwenye Katiba ya sasa.Mbali na pendekezo hilo, kamati hizo zimegawanyika
kuhusu Ibara ya 129 ya Rasimu ya Katiba inayowapa wananchi nguvu ya
kumuondoa mbunge wao madarakani kabla ya miaka mitano kumalizika.
Hayo yalijitokeza bungeni Dodoma jana, wakati
kamati hizo zikiwasilisha taarifa zake kuhusu Sura ya 9 na 10 ya Rasimu
ya Katiba iliyowasilishwa bungeni na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Akiwasilisha maoni ya Kamati Namba 10, Mjumbe wa
kamati hiyo, Dk Dalaly Kafumu alisema suala la kugombea nafasi yoyote ni
la kidemokrasia, hivyo haipaswi mtu yeyote kuzuiwa kwa kigezo cha
elimu.
“Haki ya kuamua iwapo mgombea anafaa au hafai ni
ya wapigakura. Wasizuiwe kikatiba kutumia haki yao ya msingi ya kuchagua
mtu wanayemtaka,”alisema na kuongeza: “Utaratibu huu haupo duniani kote
hata nchi zilizo na demokrasia iliyokomaa. Hivyo ibara hiyo isomeke tu
ajue kusoma na kuandika na si kiwango cha elimu kama sifa ya msingi.”
Mapendekezo hayo yaliungwa mkono na Kamati Namba 8
kupitia kwa Mjumbe wake, Juma Alawi aliyesema kuweka kiwango cha elimu
kwa wagombea ubunge ni ubaguzi.
Kuondolewa kwa kigezo cha elimu ya kidato cha nne
pia kumeungwa mkono na kamati namba 10, 4, 12, 9 na 12 za Bunge hilo
zilizowasilisha taarifa zake jana asubuhi.
Kamati namba 12 ndiyo iliyokwenda mbali zaidi na
kudai kuwa ibara hiyo itasababisha ubaguzi kulingana na elimu wakati
kiwango cha chini cha elimu kwa Tanzania Bara ni darasa la saba na
Zanzibar ni darasa la 10.
Hata hivyo, ni Kamati Namba 2 tu inayoongozwa na
Shamsi Vuai Nahodha iliyokubali pendekezo la Rasimu la kutaka kuwapo
kigezo cha elimu. Akiwasilisha maoni ya kamati hiyo, Vuai alitaka ibara
hiyo ifanyiwe marekebisho na kufuta maneno “anajua kusoma na kuandika
Kiingereza na Kiswahili” na badala yake isomeke, “ana elimu isiyopungua
kidato cha nne”.
Wakati kamati karibu zote zikikubaliana kuhusu
kuondoa kigezo cha elimu katika kuwania ubunge, zimetofautiana kuhusu
Ibara ya 129 ya inayowapa wananchi nguvu ya kumuondoa mbunge wao
asiyewajibika kwao.
Mapendekezo ya Tume ya Jaji Warioba yalitaka
wananchi wawe na haki ya kumuondoa mbunge, endapo ataunga mkono sera
zinazokwenda kinyume na masilahi ya wapigakura wake au iwapo atashindwa
kutetea kwa dhati hoja zinazotokana na kero zao au ataacha kuishi au
kuhamisha makazi yake kutoka jimbo lake kwa miezi sita bila sababu.
Kamati Namba 12 iliafiki wananchi kupata nguvu
hiyo ya kumuondoa mbunge endapo tu atakuwa ameunga mkono sera ambazo
zinakwenda kinyume na masilahi ya taifa na si ya wapiga kura
waliomchagua.
Post a Comment