Mchumba wa marehemu Saguda akilia kwa uchungu.
Recho alifariki dunia Mei 27, mwaka huu katika Hospitali ya Taifa
Muhimbili alipokuwa amelazwa kwenye chumba cha wagonjwa wanaohitaji
uangalizi maalum ‘ICU’ baada ya kujifungua na mtoto kufariki dunia muda
mfupi baadaye.Staa huyo alijifungua kwa upasuaji mtoto wa kiume, lakini kwa bahati mbaya tatizo la presha ya kushuka na sukari lilimpata na hivyo kuanza kupatiwa huduma ya haraka kabla ya mauti kumkuta.
Recho alijifungua katika Hospitali ya Rufaa ya Jeshi Lugalo, Jumapili Mei 25, mwaka huu na hali ilipobadilika alikimbizwa Muhimbili, kabla ya mauti kumfika.
SIMULIZI YENYEWE
Mchumba anayeonekana ni mume wa marehemu Recho, George Saguda ambaye uhusiano wao ni wa miaka takribani mitano sasa, alisimulia mazito kuhusu uhusiano wake na marehemu huyo.
Waombolezaji wakiwa kwenye mazishi.
Katika mazungumzo na gazeti hili, juzi Jumatano, Sinza – Palestina
jijini Dar, nyumbani kwa mjomba wa marehemu Recho ambapo msiba uliwekwa,
Saguda alisema kamwe hawezi kumsahau Recho.“Nina machungu sana moyoni.
Naumia kumpoteza mke wangu na mwanangu. Walikuwa muhimu sana kwangu. Ndoto zote zimezimika. Ulikuwa mwanzo mzuri wa maisha yetu tuliyokuwa tumeyapanga,” alisema Saguda.
Akaongeza:
“Sikuwa na hili wala lile. Taarifa za kifo cha Recho bado kama ndoto, ningefurahi kama ingekuwa hivyo. Tulipanga mengi na Recho, sikujua kama mwisho wake ulikuwa umefika.”
“Tulijiandaa vizuri sana kumpokea mtoto wetu. Siku chache kabla ya kusikia uchungu, tulikwenda madukani kumfanyia mtoto shopping. Tulitumia zaidi ya shilingi laki nane (800,000).
“Tulimchagulia nguo nzuri na vitu vingine muhimu kwa ajili yake, kumbe Mungu alikuwa ameshapanga yake (analia).”
SIMANZI TUPU
“Tulimfikisha Recho salama Hospitali ya Lugalo, akajifungua vizuri mtoto wa kiume. Nakumbuka ilikuwa Jumapili usiku. Lakini kutokana na hali ya mtoto ilivyokuwa, hakupewa. Aliwekwa chini ya uangalizi wa manesi.
“Mke wangu hakuwa na hali mbaya ya kutisha, niliondoka hospitalini na tukawa tunatumiana meseji ule usiku. Ni picha ambayo inagoma kufutika kichwani mwangu.”
“Kuna meseji alinitumia, akasema: Mume wangu nimekuzalia kidume, naona sasa utakuwa umepata mtu wa kwenda naye uwanjani kushangilia mpira, siku Yanga ikicheza.
“Meseji hiyo inaniumiza sana. Nashindwa kuamini kilichoendelea, moyo wangu una majonzi sana. Ni ngumu kukubali kifo kilichotokea usiku wa Jumatatu wakati Jumapili tu nilikuwa nachati naye. Sijielewielewi kwa kweli.”
WASIWASI
Anasema usiku wa Jumapili akiwa wodini, alimwangalia Recho na kuona namna hali yake ilivyobadilika, akamwambia: “Mke wangu naona kama hali yako siyo nzuri, umechoka sana lakini jikaze, utapata nafuu tu.”
MIPANGO YA MAISHA
Akizidi kumzungumzia marehemu, Saguda alisema Recho alikuwa mwanamke sahihi katika maisha yake kwani walipanga mengi na walianza kutekeleza kwa msaada mkubwa wa mawazo yake.
“Alikuwa mwanamke mwenye akili sana. Recho si mfujaji wa fedha. Unaweza kuacha shilingi milioni kumi (10,000,000) ndani asipate tamaa ya kuziingiza kwenye matumizi ambayo hayakuwa kwenye mipango.
Tulikuwa tupo kwenye mipango ya kuanza kurekodi filamu nyingine.
“Alikuwa mwanamke anayeangalia maendeleo zaidi, hakupenda sana starehe. Kuna wakati nilimwambia sasa tununue gari, akasema hapana, tujijenge kwanza ndipo tununue gari, tena yeye akasema inafaa tununue Noah (Toyota) ili litusaidie pia location (shughuli za kurekodi).
KIAPO KIZITO
“Sijui kama nitakutana na mwanamke kama Recho, Dar es Salaam, nadhani haitatokea. Alizaliwa kwa ajili yangu. Amenibadilisha sana, sikuwa hivi, vitu vingi naweza kusema ni kwa sababu yake. Nimepata pigo kubwa sana.”
RECHO ALIKUWA YATIMA
Habari za ndani kutoka kwa rafiki wa karibu na marehemu Recho zinasema kuwa wazazi wake walishatangulia mbele za haki hivyo alilelewa na bibi mzaa mama.
MJOMBA WA RECHO
Maelezo ya rafiki huyo wa marehemu, yanajidhihirisha yenyewe baada ya Risasi Jumamosi kupata nafasi ya kuzungumza na mjomba wa marehemu, Evance Haule.
Haule alisema kifamilia hawamtambui Saguda kwa sababu hajawahi kujitambulisha rasmi ingawa alikiri kuutambua uhusiano wao.
“Ninachojua walipanga Saguda angekuja nyumbani baada ya Recho kujifungua. Saguda nimemuona kwa mara ya kwanza hapa msibani,” alisema Haule.
TUJIKUMBUSHE
Marehemu Recho alificha ujauzito wake na hakutaka picha zake zionekane mahali popote.
Katika gazeti damu moja na hili, Amani la Aprili 24, mwaka huu, liliandika habari iliyomhusu yenye kichwa, RECHO: NINGEKUWA NA UJAUZITO NINGEJIRUSHA?
MASTAA WAMGEUKIA MUNGU
Kutokana na vifo vya mfululizo vya mastaa wa filamu za Kibongo, wasanii hao wameahidi kumrudia Mungu na kwamba wataanza kuonekana kwenye nyumba za ibada.
Kulwa Kikumba ‘Dude’ ni mmoja wa wasanii wa waliotoa wito kwa mastaa kuachana na starehe za dunia na kumgeukia Mungu, akisisitiza: “Pombe haifai, tukae nayo mbali, ndiyo chanzo cha vifo vya wasanii wengi. Tumrudieni Mungu jamani.”
Marehemu Recho alizikwa Alhamisi, katika Makaburi ya Kinondoni ikiwa ni baada ya misa ya kumuombea na hatimaye kuagwa katika Viwanja vya Leaders Club, Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Mungu aipumzishe roho ya marehemu mahali pema peponi – Amina.
Imeandikwa na Gladness Mallya na Chande Abdallah. Picha na Hamida Hassan na Musa Mateja.
Post a Comment