Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

KING KIKI: KILA SIKU NASALI BABU SEYA AACHIWE

MWANAMUZIKI mkongwe katika muziki wa dansi nchini, Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’ amesema huwa anasali kila siku kumuombea mwanamuziki mahiri nchini, Nguza Viking ‘Babu Seya’ na mwanaye Johnson Nguza ‘Pakii Kocha’ waachiwe kutoka gerezani.

 
Mkongwe katika muziki wa dansi nchini, Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’ akisisitiza jambo katika ofisi za Global Publishers.
Nguza na mwanaye wapo kwenye Gereza Kuu la Ukonga jijini Dar es Salaam wakitumikia kifungo cha maisha kufuatia kupatikana na hatia ya kulawiti watoto 10 katika hukumu iliyotolewa Juni 25, 2004,  Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
Katika mahojiano na Live Chumba cha Habari Alhamisi iliyopita, King Kiki alisema anamuombea Babu Seya kwa Mungu kwa sababu bila yeye asingekuwa Tanzania na kuimbia Bendi ya Marquis Du Zaire.
Kiki alisema wakati anatunga mtindo wa Kamanyola Bila Jasho, Babu Seya ndiye alikuwa akikung’uta gitaa la solo na akajipatia umaarufu mkubwa hadi kupewa cheo cha kijeshi cha Field Marshal wa solo. Baadhi ya mahojiano yalikuwa kama ifuatavyo:
Mwandishi: Kwa maoni yako unadhani Nguza au Babu Seya walifanya makosa waliyohukumiwa nayo?
Kiki: Binafsi kwa jinsi ninavyomjua Babu Seya, naamini hakufanya, alionewa na ipo siku yanaweza kutokea maajabu akaachiwa huru.
Mwandishi: Unaamini katika miujiza?
Kiki: Naamini miujiza ipo na huwa inatokea sana duniani.
Mwandishi: Ulitunga mtindo wa Kamanyola ukiwa na Bendi ya Marquis Du Zaire, nini maana ya mtindo huo?
Kiki: Kamanyola ni mji kule DRC Kongo, sasa mimi niliongeza Bila Jasho kwa maana kuwa mchezaji wa muziki huo atacheza taratibu kwa raha zake. Nilitunga mtindo huo baada ya kujiunga na bendi hiyo mwaka 1977.
Mwandishi: Ulianza kuimba muziki wa dansi mwaka gani? Halafu tupe historia yako kwa ufupi.
Kiki: Kwanza kabisa, nilizaliwa mwaka 1947. Nilianza kuimba mwaka 1962 baada ya kuacha masomo nikiwa sekondari kwa sababu muziki uliniingia katika damu.
 
“Nilijiunga na Bendi ya Fouvette kabla ya kubadilishwa jina na kuitwa Safari Nkoi. Tuliingia Tanzania na bendi hiyo chini ya Fred Ndala Kasheba miaka ya 1970.
“Baadaye tulirudi nyumbani Lubumbashi (DRC) lakini mwaka 1977 nilikuja tena Tanzania na kujiunga na Bendi ya Marquis kabla ya kuiacha na kujiunga na Orchestra Safari Sound, nikaanzisha mtindo wa Masantula Ngoma ya Mpwita.
“Hata hivyo, mwaka 1983 nilianzisha bendi yangu ya King Kiki Double O na mtindo wa Embalasasa Shika Breki.
“Bendi hiyo ilikufa kutokana na uchakavu wa vyombo, nikaongoza kwa muda Bendi ya Sambuluma na Nguza lakini mwaka 1994 nikiwa na marehemu Ndala Kasheba tukaanzisha Bendi ya Zaita Musica.
“Mwaka 2003 nikiwa na Ndala huyohuyo tukaanzisha Bendi ya Wazee Sugu La Capital. Bahati mbaya mwenzangu Kasheba akafariki dunia mwaka mmoja baadaye, yaani 2004, lakini mpaka sasa nina bendi mbili, moja ipo Mwanza.”
Mwandishi: Una historia ndefu. Je, unaweza kutueleza mafanikio yako katika muziki?
Kiki: Namshukuru Mungu nina mafanikio ya kawaida, nina nyumba Temeke Wailes (Dar), nina watoto saba, walikuwa tisa wawili  walishafariki dunia.
“Nina mke Mtanzania na bendi hizo mbili. Niliwahi kwenda Uingereza tulipata mwaliko na mwaka 2011 tulienda Marekani tulialikwa katika sherehe ya miaka hamsini ya uhuru wetu na nashukuru Bendi ya Wazee Sugu. Mimi kwa sasa ni Mtanzania nilipata hati hiyo mwaka 1997.
Mwandishi: Kwa nini uliamua kuishia Tanzania?
Kiki: Ni ukarimu wa Watanzania. Nilipofika hapa mara ya kwanza mwaka 1970, niliona watu ni wakarimu sana, nikaamua kurudi mwaka 1977 na nikaamua kuishi hapa.
Mwandishi: Mpaka sasa umetunga nyimbo ngapi?
 
‘King Kiki’ akikumbushia waandishi wa Global Publishers wimbo wa kitambaa cheupe.
Kiki: Nimeshatunga nyimbo nyingi, hamsini kwenye Bendi ya Marquis na ishirini Safari Sound. Kuna wakati nilikuwa na uwezo ndani ya wiki mbili kutunga nyimbo ishirini.
“Baadhi ya nyimbo zilizotikisa ni Kyembe, Safari Yetu Mbeya, Nasema Sina Ndugu, Msimamo wa Nyerere, Noele (Krismas), Haruna Kaka na kadhalika.
Mwandishi: Kuna tetesi kwamba ulikuwa na mpango wa kumuoa mwanamuziki Ngalula enzi hizo. Je, kuna ukweli?
Kiki: Hapana. Ngalula alikuwa mcheza shoo wa Marquis na mwenzake Frida. Alikuwa na uhusiano na mpiga solo wetu Bizo Matuka na ndiye aliyemuoa, ni mke na mume hadi leo.
Mwandishi: Miaka yote nakuona unaimba. Je, kupiga ala za muziki huwezi? Na kati ya watoto wako kuna aliyefuata nyayo zako?
Kiki: Naweza kupiga magitaa yote lakini huwa napendelea kuimba kwani hata waswahili walisema kila ndege na mti wake. Katika watoto wangu, Veronica Kikumbi amefuata nyayo zangu, huwa naimba naye, hata ule wimbo wa Fungua Njia nimerekodi naye.
Mwandishi: Nini kifanyike ili kuinua muziki wa dansi unaoonesha kuporomoka nchini?
Kiki: Kama angepatikana mdhamini, tukarekodi upya nyimbo zilizovuma na zikatangazwa, kukafanyika onesho, maajabu makubwa yataonekana.
 
Mkongwe katika muziki wa dansi nchini, Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’ akiwa na wahariri wa Global Publishers.
Siku hizi tunatunga nyimbo nzuri lakini hazipigwi kwenye vituo vya redio na tv, hivyo watu hawajui kinachoendelea na muziki unaporomoka.
Mwandishi: Kuna mwanamuziki kijana anaitwa Diamond anafanya vizuri, unamshauri nini?
Kiki: Ni kweli kijana huyu ana nyota ya muziki na anakubalika. Namshauri asilewe sifa, afuate miiko ya muziki, atapaa zaidi.
Mwandishi: Upo tayari kufanya kazi na mwanamuziki yeyote wa kizazi kipya?
Kiki: Huwa nafanya nao kama vile Joh Makini na nduguye, nilifanya naye muziki na hata MwanaFA. Wote nawakaribisha, nipo tayari kuwasaidia uzoefu wangu.
Mwandishi: Katika muziki, nini unakikumbuka?
Kiki: Ni safari yetu ya Tanga miaka ya 1980, Bendi ya Atomic ilitupokea vizuri sana lakini pia siku hiyo tulizindua OSS na mtindo wetu wa Masantula pale Safari Resort, watu walijaa sana na walinishangilia sana. Sizisahau siku hizo kwani Ibrahim Sembreno mwenyeji wetu alitupokea vizuri.
Mwandishi: Kwa sasa watu wakitaka kuona shoo yako unapatikana wapi hapa Dar?
Kiki: Tunapiga Whips Bar kila Ijumaa, Jumamosi tunakuwa La Prima, Victoria na Jumapili Shekina Bar, Mbezi Beach.
Mwandishi: Nakushukuru kwa kuja Global.
Kiki: Ahsante.
Ili kuyapata mahojiano haya kwa undani na picha nzuri, angalia Global Tv Online sasa hivi.

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
© Copyright BONGO HABARI
Back To Top