Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

WEMA, AUNT NINI KILITOKEA PALE MSIBANI?

 
 Diva wa filamu za Kibongo, 'Wema sepetu' akilia wakati wa mazishi ya Kuambiana.
NIMEWAHI kumzungumzia Wema Sepetu mara kadhaa, ingawa hii itakuwa mara yangu ya kwanza kumleta katika safu hii Aunt Ezekiel. Nimeamua kuwazungumzia kwa pamoja kutokana na tukio lililotokea hivi karibuni la kufariki na kuzikwa kwa mmoja wa watu muhimu sana kwenye filamu Tanzania, Adam Kuambiana.
Nimemfahamu Wema kwa muda mrefu kidogo, tokea pale alipoukwaa Umiss Tanzania mwaka 2006. Katika uigizaji, nadhani ni mmoja kati ya waigizaji wachache wa kike wenye vipaji vya kweli.
Nimemuona katika filamu chache alizoshirikishwa na niwe mkweli, anajua kuigiza. Nadhani amefanya vizuri kwa kila kipengele alichowekwa. Kwa hili, nitakuwa sijatenda haki kama nitashindwa kumpa sifa zake.
 
Staa kunako tasnia ya filamu za kibongo, Aunt Ezekiel akiwa na simanzi nzito kwenye mazishi ya Kuambiana.
Nimeona pia kazi za Aunt Ezekiel. Huyu ni miongoni mwa wale ambao kwangu mimi, ni wauza sura zaidi kuliko uhalisia wa wanachoigiza. Katika filamu zake nilizoziona, anapenda zaidi kuuachia mwili wake ili pengine mashabiki waone alivyo na figa kali.
Kama utaniuliza kuhusu Aunt, nitakueleza wazi kuwa hajawahi kuwa mwigizaji wa kunivutia. Kwa muda mrefu wakati ule nikichambua filamu, nimewahi kumwelezea kama mtu anayeharibu ladha kwa kitendo chake cha kupenda kujionyesha zaidi mwili, ambao kwa kweli, Mwenyezi Mungu amemjaalia.
Ni mmoja kati ya waigizaji wanaoamini katika mavazi ya nusu utupu kwenye kazi zao na ndiyo maana mara zote hutokea akiwa hivyo.
Juzi wakati wa msiba wa Kuambiana, wasichana hawa walikuwepo, lakini kwa sisi ambao tunawafahamu waigizaji na jinsi wanavyoishi, hasa katika matukio kama haya, unatambua kabisa kwamba kulikuwa na tatizo baina ya mabinti hawa na wenzao.
Baadhi ya marafiki wa Bongo Movie wanasema kulikuwa na ushirikiano usioridhisha kutoka kwao, wakati wote wa tukio hilo, kuanzia hospitalini kwa Mama Ngoma, Muhimbili hadi nyumbani kwa marahemu. Kwamba, wasanii walipanga kukutana katika Viwanja vya Leaders Club Jumatatu iliyopita, ili wapande gari moja au kuwa katika msafara mmoja kuelekea Bunju, kulikokuwa na msiba huo.
Wao hawakutokea. Wanadai pia kwamba Wema na Aunt wamekuwa wagumu kujitokeza kwenye misiba inayowahusu wanafamilia wa Bongo Movie. Mrembo huyu wa zamani wa Tanzania alipofiwa na baba yake mzazi, baadhi ya wasanii hawakujitokeza msibani na walipoulizwa, walisema yeye hafanyi hivyo kwa wenzake.
Inawezekana ikawa ni staili ya maisha waliyoichagua, kwa sababu wapo watu wa aina yao duniani. Kuna baadhi ya wenzetu wameacha hadi wosia kuwa siku watakapokufa, mazishi yao yasihudhuriwe na watu wengi. Lakini ni jambo la ajabu kidogo kwa kitu kama hiki kutokea katika jamii kama yetu.
Tunaamini kuwa kufa ni jambo kubwa, linalohitaji ushirikiano, hata kuwe na uadui wa kiasi gani. Huenda akina dada hawa wana bifu na wenzao, lakini sidhani kama mambo hayo yanapaswa kuzingatiwa katika matukio kama haya.
Hii ni kwa sababu huwezi kujua kesho kuna nini kinaweza kukutokea. Wanaweza kuwa wanajiamini kwamba watu wao wa karibu wanatosha kuwapa sapoti wakati wa matatizo, lakini siku zote nafsi husononeka sana unapokosa uungwaji mkono kutoka kwa watu wako wa karibu, hasa unaofanya nao kazi.
Labda wanapotoshwa na ustaa wanaodhani wanao. Niwashauri tu kama wadogo zangu kwamba katika dunia hii isiyotabirika, siyo jambo zuri watu kukutazama kwa jicho la kukusema kwa mambo kama haya. Hata kama lipo tatizo na wenzao, haipendezi kulionyesha kama ilivyokuwa kwao.
Sidhani kama kuna jambo lolote lingeharibika, endapo kwa mfano, wawili hao wangejichanganya na wenzao, hata kama ni kinafiki, ilimradi baada ya hapo kila mmoja na hamsini zake.
Ninajua binadamu tunaishi zaidi kinafiki kuliko uhalisia, ndiyo maana siku hizi hakuna urafiki wa kuchanjiana damu kama ilivyokuwa enzi hizo, baadhi ya watu huenda kwenye misiba ya wenzao wakiwa wanachekelea mioyoni mwao, ingawa wakiwa hapo hutoa machozi ya uongo.

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
© Copyright BONGO HABARI
Back To Top