NAMSHUKURU
Mungu muweza wa yote kutukutanisha tena siku ya leo katika uwanja wetu
wa mahaba. Najua Valentine’s Day imepita, naamini kabisa marafiki
mliitumia vyema siku hiyo kuoneshana upendo wa kutosha.
Bila
shaka mtakuwa mmejadili na kupanga mikakati mbalimbali ya penzi lenu na
kujua mnaelekea wapi. Penzi ambalo halina malengo ya baadaye halina
maana.Usikubali kuishi katika penzi ambalo halina muelekeo. Fanya
maamuzi, lazima kila wakati ulitathimini penzi lako na kuona kama lina
uhai mrefu mbeleni au ni la muda mfupi, kimjinimjini kama wanavyosema
vijana wa kisasa.
Tukirejea katika mada yetu ya leo kama inavyojieleza hapo juu. Hakika
kila mmoja anatambua kwamba wazazi ndiyo ambao wametuleta
duniani.Wazazi ndiyo waliokutana na changamoto nyingi za maisha kabla
yetu. Wao ndiyo wenye uzoefu wa kutosha katika maisha.Wazazi ndiyo dira ya watoto na ndiyo maana haishangazi kuona mtoto wa mzazi ambaye ana tabia flani mbaya akawa ameirithi kutoka kwa wazazi.Waswahili wanasema mtoto umleavyo ndivyo akuavyo, wazazi wana nafasi kubwa katika maamuzi ya watoto wao hadi pale na wao watakapofikia hatua ya kuwa na familia yao.
Wazazi wanaweza kuwa na msimamo fulani katika jambo la vijana wao, mwisho wa siku vijana wao wanalazimika kukubaliana nao. Wazazi kwa sababu zao wanaweza kuonesha msimamo katika jambo fulani ikiwemo hata kuzuia suala la ndoa na kweli isifungwe.
Inapotokea mvutano wa wazazi katika suala la ndoa ndipo mfarakano mkubwa unapotokea. Wapendanao watakuwa wanayumbishwa, kutokana na nguvu hiyo, mara nyingi waathirika wanakuwa wanandoa watarajiwa.
Wanaathirika kwa sababu wao wanaweza kuwa wamekubaliana kwa hali yoyote lakini wazazi wanaweza kuweka kipingamizi kulingana na vigezo ambavyo wao wanavifahamu.Hapo utakuta upande mmoja unataka ndoa mwingine unakuwa hautaki. Msukumo unakuwa mkubwa, wanandoa watarajiwa nao wanabaki njia panda. Upande unaokataa ndoa unakuwa na sababu zake kulingana na matakwa ya dini, desturi na hata imani.
Wakati
tukiendelea kusoma makala haya, hebu tuusome mfano huu hai kutoka kwa
msomaji aliyeniomba ushauri:“Naomba ushauri, nimeishi katika uhusiano na
mwenzangu kwa takriban miaka mitano sasa. Kiukweli yeye ananipenda na
mimi nampenda sana. Tulipanga kufunga ndoa mwaka jana lakini ndoto hiyo
haikuweza kutimia kutokana na msukumo wa wazazi wangu.
“Yeye ni imani tofauti na mimi, wazazi wangu wamebobea katika masuala
ya dini na hata mimi pia. Wamenizuia kabisa nisibadili dini, wanasema
nikithubutu tu wananitenga.“Wakati huohuo mwenzangu naye ndugu zake,
wazazi wake nao wamemzuia kutokana na sababu zao wanazozijua wenyewe na
wala si suala la dini.“Tumekaa vikao na vikao ili kujaribu kutafuta suluhu lakini wapi hatukupata muafaka, kwa kweli nimechoka. Kinachoniuma zaidi ni kwamba sisi wenyewe hatuna tatizo, tumekubaliana kufunga ndoa hata bomani kila mmoja akabaki katika dini yake lakini wazazi wangu hawataki hata kusikia suala hilo, tafadhali nishauri nifanyeje ili kunusuru ndoa yangu?”
MFANO HUO UNATUFUNDISHA NINI?
Kupitia mfano huo tunaona ni jinsi gani nguvu ya wazazi inavyoweza kupenya kwa vijana wao hadi kufikia hatua ya kukwamisha suala la ndoa. Vijana wamependana lakini kikwazo kinakuwa ni wazazi.
KUNA ULAZIMA WAZAZI KUINGILIA?
Hapa kuna kitu cha kujifunza. Kwanza wazazi wanapaswa kusikilizwa lakini katika suala hili ni vyema wakakupa mwongozo mapema, wasisubiri wakati mambo yameshaharibika.Kama nilivyoeleza awali, wakujengee misingi mizuri, wakufundishe nini unapaswa kufanya pindi unapotaka kuingia katika hatua ya uchumba na baadaye ndoa.
USISITE KUTUACHIA UJUMBE WAKO HAPO CHINI
Post a Comment