JESHI la Polisi Mkoa wa Arusha limewatia mbaroni watu kadhaa kwa kuhusishwa na tukio la ujambazi wa kuteka mabasi sita ya abiria yaliyokuwa yanatoka nchini Kenya kuelekea jijini Arusha.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa, Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alisema katika msako huo ulioanza jana
wamefanikiwa kukamata watu hao katika maeneo tofauti mkoani humo.
Kamanda Sabas alisema kwa sasa jeshi hilo haliwezi kutaja majina ya
watuhumiwa hao kutokana na utaratibu wa uchunguzi unaofanywa na jeshi
hilo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi.
“Kutokana na taratibu za uchunguzi kwa sasa hatuwezi kutaja majina ya
watuhumiwa tuliowakamata kwa kuhusika na tukio la ujambazi. Hadi sasa
bado hatujamaliza uchunguzi wetu na pindi tukikamilisha tutawafikisha
mahakamani kwa mujibu wa sheria,” alisema Kamanda Sabas.
Alisema magari mawili kati ya sita yaliyotekwa yalikuwa na mizigo na wafanyakazi.
“Tukimaliza uchunguzi tutawapatia taarifa rasmi na kila kitu kuhusu
tukio hili, ila kwa sasa tumeongeza nguvu ya ulinzi katika njia hiyo,”
alibainisha Kamanda Sabas.
Alisema mabasi hayo yaliyotekwa yanamilikiwa na kampuni za Perfect,
Dolphine, Taqwa na Spider ambayo yote yanafanya safari zake kati ya
Arusha na Nairobi.
Kamanda Sabas alisema katika kukabiliana na uhalifu kama huo, Jeshi la
Polisi litaongeza magari ya doria katika barabara hiyo inayounganisha
Kenya na Tanzania.
“Kazi ya ulinzi ina changamoto nyingi kwani wahalifu nao wanabadili
mbinu, eneo walikofanya utekaji ni eneo la wazi kabisa ambalo huwezi
kuamini wangeweza kuteka magari, lakini tutahakikisha kuwa barabara hii
inakuwa salama muda wote,” alisema Sabas.
Katika tukio hilo, dereva wa basi la Perfect alijeruhiwa jicho la kushoto baada ya kupigwa jiwe alipotaka kutoroka.
Tukio la kutekwa mabasi hayo lilitokea juzi usiku baada ya watu
wanaodhaniwa kuwa majambazi kuvamia na kuteka mabasi hayo katika eneo la
Mbuga Nyeupe, Wilaya ya Longido.1
MATANGAZO
USISITE KUTUACHIA UJUMBE WAKO HAPO CHINI
Post a Comment