Heri
ya Mwaka Mpya! Mimi na wewe tunapaswa kumshukuru Mungu kwa kutuwezesha
kuumaliza salama mwaka 2014 na kuuanza mwaka mpya wa 2015. Najua wapo
wengi ambao walitamani kuuona mwaka huu lakini kwa namna moja au
nyingine, wakashindwa.
Karibu
tena tujadili mambo mbalimbali yahusuyo uhusiano wa kimapenzi. Njia
nzuri ya kuuanza mwaka mpya, ni kupata muda wa kukaa na kutathmini
nyendo zako na mambo yote yaliyotokea katika maisha yako kwa kipindi cha
mwaka mzima wa 2014.
Wengi huwa wanakumbuka kujadili mambo yao ya kimaisha ikiwemo kazi,
malezi ya watoto, ujenzi wa nyumba, maendeleo ya biashara au vitu
vinavyofanana na hivyo lakini huwa wanashindwa kufanya tathmini ya jambo
muhimu zaidi; mapenzi na maisha ya ndoa.Mipango yako yote inategemea amani ya moyo na utulivu wa akili yako, huwezi kuvipata vitu hivi kama utakuwa na migogoro ya mapenzi ndani ya ndoa au uhusiano wako kila kukicha.
Kwa kuzingatia hilo, ndiyo maana wataalam wa saikolojia ya mapenzi, wanashauri kwamba wakati ukikaa na kutafakari mafanikio na matatizo uliyokumbana nayo mwaka uliopita na kuandaa mikakati ya mwaka mpya, ni muhimu sana kulitazama suala la mapenzi kwa upana wake.
1. ALIKUKOSEA NA WEWE UKAMKOSEA
Sisi si malaika, kila binadamu hukosea na hakuna mtu ambaye ni mkamilifu kwa asilimia 100. Yawezekana ukitafakari maisha uliyoishi na mwenzi wako kwa kipindi cha mwaka mzima uliopita, unayaona makosa makubwa aliyowahi kukufanyia.
Hiyo ni hatua ya kwanza lakini ya pili unapaswa kujitazama na wewe, lazima yapo ambayo ulimkosea na pengine kusababisha kulegalega kwa mapenzi yenu. Unapouanza mwaka mpya, ni muhimu sana kukaa na mwenzi wako na kwa pamoja mkajadili mambo mliyokoseana kwa lengo la kuyamaliza na kufungua ukurasa mpya.
Tafuta muda ambao nyote mtakuwa mmetulia, kila mmoja aeleze dukuduku lake na makosa aliyowahi kutendewa na mwenzake kisha kubalianeni kuweka pembeni tofauti zote za mwaka uliopita na kuangalia mwaka mpya.
Lazima zipo ahadi ambazo ulimuahidi mwenzi wako, na yeye lazima zipo ahadi ambazo alikuahidi. Mnapoanza mwaka mpya, ni wakati wa kila mmoja kutathmini jinsi alivyotimiza ahadi alizomuahidi mwenzi wake.
Wahenga wanasema ahadi ni deni, hakuna kitu kibaya kama kumuahidi mwenzi wako jambo halafu ukashindwa kulitimiza bila kuwa na maelezo yoyote. Hebu orodhesha ahadi zote ambazo uliwahi kumpa na jiulize umezitimiza kwa kiwango gani?
Ukigundua ahadi nyingi zimekuwa hewa, ni wakati wa wewe kuzungumza na mwenzi wako kabla hata hajakukumbusha. Mueleze nini kilisababisha ukashindwa kutimiza ulichomuahidi, hiyo itamfanya aone kwamba wewe ni mtu unayejali, atauanza mwaka vizuri akiwa na uhakika kwamba yupo na mtu makini.
3. UMEMSALITI MARA NGAPI?
Nilisema na nitaendelea kusema kwamba hakuna kitu kibaya kama usaliti. Wakati ukiuanza mwaka mpya, jiulize mwenyewe ndani ya moyo wako; ulimsaliti mwenzi wako mara ngapi? Yawezekana mwenyewe hajui lakini ndani ya moyo wako unao ukweli.
Kama hujawahi kumsaliti, una haki ya kujipongeza na kuendelea na moyo huohuo kwani uaminifu ndiyo nguzo kuu ya mapenzi. Hata hivyo, kama unajua kwamba umesaliti mara kadhaa, zungumza na moyo wako mwenyewe na jiahidi kwamba hutamsaliti tena na tekeleza ahadi hiyo kwa vitendo, bila kujali vishawishi unavyokutana navyo.Tukutane wiki ijayo kwa mwendelezo wa mada hii. Kwa maoni, ushauri, nicheki kwa namba za hapo juu.
USISITE KUTUACHIA UJUMBE WAKO HAPO CHINI.
Post a Comment