Akizungumza
jijini Dar es Salaam jana, Spika Anne Makinda aliwaambia waandishi wa
habari katika Ofisi ndogo ya Bunge, waliotaka kujua hatima ya wenyeviti
hao, kuwa hawapo tena katika nafasi zao baada ya kujiuzulu.
“Wenyeviti
hao kwa ninavyojua mimi wamejiuzulu, kama ambavyo azimio lilivyotaka,
kama wapo hizo taarifa mimi sina na sijui kinachoendelea, nawaambia mimi
wameshajiuzulu,” alisema Spika Makinda.
Makinda
alisema wenyeviti hao, ambao ni wa Kamati ya Nishati na Madini, Victor
Mwambalaswa, wa Katiba, Sheria na Utawala William Ngeleja na Andrew
Chenge wa Kamati ya Bajeti, hawaendelei tena na nafasi zao, kupisha
viongozi wengine kuchaguliwa ndani ya kamati husika.
Hata
hivyo, Makinda alipoulizwa kama wenyeviti hao kama wamejiuzulu rasmi
kwa barua na kama yeye amezipokea lini, alisema viongozi hao ni wa
kamati na hivyo wamewajibika katika kamati zao.
“Mimi
ndiye Spika, nasema wamejiuzulu… msiniulize barua zao wala nini,
heshima ya mtu ni kujiuzulu mwenyewe bwana na wao wamefanya hivyo,” alisema Spika Makinda.
Katika
Azimio namba tatu la Bunge katika majadiliano ya sakata hilo, Bunge
lilielekeza kuwa kamati husika za kudumu za Bunge, zichukue hatua za
haraka na kwa vyovyote vile kabla ya mkutano wa 18 wa Bunge, kuwavua
nyadhifa zao wenyeviti tajwa wa kamati husika za kudumu za Bunge.
Utekelezaji
wa azimio hilo, unakuja baada ya Serikali kutekeleza maagizo ya Bunge
hilo kwa kuwawajibisha baadhi ya viongozi wake, waliotajwa katika ripoti
hiyo.
Chenge
ambaye ni Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), alitajwa katika ripoti ya
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuwa aliwekewa Sh bilioni
1.6 katika akaunti yake binafsi na Ngejela ambaye ni Mbunge wa Sengerema
(CCM) aliingiziwa Sh milioni 40.4 kwenye akaunti.
Waliingiziwa
fedha hizo na mmiliki wa Kampuni ya VIP Engineering & Marketing,
James Rugemalira. Mwambalaswa ambaye pia ni Mbunge wa Lupa (CCM),
ametajwa kuwa alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Umeme
nchini (TANESCO), ambayo Bunge liliazimia kuwa wajumbe wake wote
wawajibishwe.
Katika
utekelezaji wa maazimio hayo, Rais Jakaya Kikwete alimtaka Waziri wa
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka kupisha
katika nafasi hiyo ili ateuliwe mtu mwingine na tayari Profesa huyo
ameshapisha.
Profesa Tibaijuka aliingiziwa Sh bilioni 1.6 katika akaunti yake binafsi, kinyume na kanuni za maadili ya viongozi wa umma.
Rais
Kikwete pia alimweka kiporo Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim
Maswi amesimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yake.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, alishajiuzulu
USISITE KUTUACHIA UJUMBE WAKO HAPO CHINI
Post a Comment