Simba ikishinda mchezo lazima itatoa tambo zake kwa Yanga na vivyo hivyo kwa upande wa pili. Hayo ndiyo maisha waliyoyachagua.
SIMBA na Yanga ni watani wa jadi. Jambo linalofanyika Simba kwa namna moja ama nyingine litakuwa na tambo kwa Yanga.
Simba ikishinda mchezo lazima itatoa tambo zake kwa Yanga na vivyo hivyo kwa upande wa pili. Hayo ndiyo maisha waliyoyachagua.
Yanga ndiyo bingwa wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara
ikiwa imetwaa taji hilo kwa mara 24 na kuzipiku timu nyingine zote
zinazoshiriki ligi hiyo. Simba inafuatia katika rekodi hiyo baada ya
kulitwaa taji hilo kwa mara 18.
Licha ya rekodi hiyo, Yanga bado inafunikwa na
Simba kwenye rekodi nyingine za maana. Simba imefanikiwa kuweka rekodi
kadhaa ambazo Yanga itasota kuzifikia. Makala hii inazungumzia baadhi ya
rekodi za Simba ambazo Yanga inasota kuzifikia na kuzivunja.
Kucheza fainali Caf
Simba ndiyo timu pekee ya Tanzania iliyofanikiwa
kucheza fainali za Kombe la Shirikisho la Vyama vya Soka Afrika (Caf),
ilikuwa mwaka 1993 wakati huo likijulikana kama Kombe la Caf. Simba
ilicheza fainali hiyo na Stella Abidjan ya Ivory Coast na kutoka sare
katika mchezo wa awali kabla ya kukubali kipigo cha mabao 2- 0 katika
marudiano jijini Dar es Salaam.
Licha ya Simba kupoteza mchezo huo ambapo
wachezaji wake waliahidiwa zawadi za magari kama wangeshinda, inasalia
kuwa timu pekee kutoka Tanzania Bara iliyofanikiwa kucheza hatua hiyo ya
fainali hizo. Yanga imewahi kufika hatua ya makundi ya michuano hiyo.
Nusu fainali klabu Bingwa Afrika
Simba inajiweza, hivyo ndivyo unavyoweza kusema
kwa lugha rahisi baada ya timu hiyo kufanikiwa kucheza nusu fainali ya
Klabu Bingwa Afrika mwaka 1974. Simba iliondolewa katika hatua hiyo ya
nusu fainali na Mehala El Kubra ya Misri na kuzima ndoto za kucheza
fainali ya michuano hiyo mikubwa zaidi Afrika.
Rekodi hiyo ya Simba bado haijavunjwa mpaka hii
leo. Yanga kwa upande wake, ilifanikiwa kucheza robo fainali ya michuano
hiyo kwa mara mbili mfululizo mwaka 1969 na 1970 lakini haikuwahi
kufika zaidi ya hapo.
Mbali na rekodi hiyo, Simba bado inajivunia rekodi
ya kuwa timu ya kwanza kutoka Bara kufanikiwa kuiondosha timu ya Misri
katika michuano ya Afrika. Simba ilifanya hivyo mwaka 2003 baada ya
kuifunga Zamalek ya Misri ambayo ilikuwa bingwa mtetezi.
Ubingwa Kombe la Kagame
Licha ya Yanga kujivunia rekodi ya kutwaa taji la Kagame nje ya
Dar es Salaam, Simba ndiyo vinara wa kulitwaa taji hilo nchini. Simba
imewahi kulitwaa taji hilo la Kagame mara sita na kuwa timu ya Bara
yenye historia ya kulitwaa zaidi kombe hilo.
Mbali na kuwa timu ya Bara iliyotwaa taji hilo
mara nyingi, Simba ndiyo timu inayoongoza kwa kutwaa Kombe la Kagame
kwenye historia ya michuano hiyo na kuzipiku timu zote za ukanda huo.
Yanga imewahi kulitwaa taji hilo mara tano na kuwa
timu ya pili kulitwaa kombe hilo mara nyingi baada ya Simba hivyo
inatakiwa kulitwaa mara moja ili kuifikia rekodi hiyo ama mara mbili ili
kuivunja rekodi hiyo kabisa.
Ubingwa wa Mapinduzi
Simba imetwaa Kombe la Mapinduzi mapema wiki
iliyopita huko visiwani Zanzibar na kuweka rekodi ya kulitwaa taji hilo
mara nyingi zaidi kwenye historia ya michuano hiyo. Simba imetwaa taji
hilo mara tatu wakati watani wao Yanga wamewahi kulitwaa mara moja pekee
tangu kuanzishwa kwake miaka tisa iliyopita.
Azam ni timu ya pili kwenye rekodi hiyo ikiwa
imelitwaa mara mbili. Mbali na rekodi hiyo pia Simba inaongoza kucheza
mechi za fainali ya michuano hiyo ikiwa imecheza mara tano wakati watani
wao wamecheza mara tatu pekee.
Kuzalisha, kuuza wachezaji
Simba ina wachezaji ambao inaweza kujivunia kuwa
ni wao. Licha ya kwamba klabu hiyo inafanya usajili wa nyota kadhaa wa
ndani na nje ya nchi, bado timu hiyo ina wachezaji inaojivunia
kuzalishwa klabuni hapo.
Simba ina wachezaji kama Ramadhan Singano, Jonas
Mkude, Said Ndemla, Abdallah Seseme na William Lucian ‘Gallas’
iliyowaibua na kuwazalisha kuwa miongoni mwa nyota wa soka nchini.
Ni wachezaji waliozalishwa klabuni hapo na
kuendelezwa mpaka sasa. Wapo wengine kama Edward Christopher ‘Edo’ ambao
wanacheza timu nyingine lakini chimbuko lao ni Simba. Yanga hakuna kitu
kama hicho.
Kikosi cha Yanga kimejaa nyota wa kununuliwa
kutoka timu nyingine za ndani na nje ya nchi. Achana na Nonda Shaaban
‘Papii’, hakuna mchezaji mwingine aliyefanikiwa kung’ara au kuuzwa nje
ya nchi akitokea Yanga.
Ni rekodi ya kipekee kwa Simba ambayo itaichukua
Yanga miaka mingi kuifikia. Mbali na hilo pia Simba inabaki kuwa
miongoni mwa timu chache nchini zilizofanikiwa kufanya mauzo ya maana ya
wachezaji nje ya nchi.
Simba ndiyo iliyomuuza Mbwana Samatta kwenda TP Mazembe. Timu
hiyo ilimuuza pia mshambuliaji wa timu hiyo, Emmanuel Okwi kwenda Etoile
Du Sahel ya Tunisia. Yanga haina utamaduni huo wa kuuza nyota wake.
Kipigo cha mabao 6-0
Yanga haitaki kabisa kuukumbuka mwaka 1977. Ni
mwaka mchungu kwao. Timu hiyo ilifungwa na Simba mabao 6-0 kwenye mechi
ya ligi shukrani kwa kazi nzuri ya Abdallah ‘King’ Kibadeni aliyefunga
mabao matatu ‘hat trick’, Jumanne Hassan ‘Masimenti’ aliyefunga mawili
na Suleiman Sanga aliyejifunga bao moja na kupeleka kilio hicho
Jangwani. Kipigo hicho kilifuta rekodi ya Yanga ya mwaka 1968
ilipoifunga Simba mabao 5-0. Ikiwa ni miaka 37 imepita bado Yanga
imeshindwa kufuta rekodi hiyo. Hali ilikuwa mbaya zaidi baada ya
kufungwa tena mabao 5-0 mwaka 2012.
Msimu bila kupoteza
Simba ilifanikiwa kuweka rekodi ya kipekee mwaka
2010 baada ya kutwaa ubingwa wa ligi bila kupoteza mchezo. Ulikuwa msimu
wa kipekee kwa Simba baada ya kucheza mechi 22 za msimu huo huku
ikishinda 18 na sare nne. Ilikuwa ni rekodi ya kipekee.
Azam iliweza kuivunja rekodi hiyo msimu uliopita
baada ya kumaliza msimu bila kupoteza mechi na kutwaa ubingwa wa Bara.
Yanga haijaweza kuwa na rekodi kama hiyo na inavyoonekana itachukua
miaka mingi kuivunja rekodi hiyo ya Simba.
USISITE KUTUACHIA UJUMBE WAKO HAPO CHINI
Post a Comment