Mali za Mbunge wa Mbinga Magharibi, Kapteni John Komba zimetangazwa kupigwa mnada kutokana na kushindwa kulipa deni analodaiwa na Benki ya CRDB.
Mali hizo zinahusisha eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 2,214
lililopo Mbezi Tangi Bovu, Dar es Salaam, kiwanja namba 1030
kilichosajiliwa kwa jina la John Damiano Komba na Salome Komba.
Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa kwenye vyombo vya habari, Kampuni
ya Uwakili ya Mpoki & Associates Advocates inayoiwakilisha CRDB
imetangaza kuuza eneo hilo la kibiashara lililotengwa kwa ajili ya
ujenzi wa vituo vya mafuta, maduka makubwa, benki, sehemu ya kufanyia
mazoezi, hospitali na huduma nyingine za kijamii.
“Tayari eneo hilo lina nyumba kubwa
ya kuishi upande unaotazamana na barabara mpya ya Bagamoyo. Kwa upande
wa kusini mwa jengo kuu linalotazama barabara hiyo kuna nyumba nyingine
ya kuishi, fremu za maduka na ofisi,” ilisomeka sehemu ya tangazo hilo.
Alipoulizwa juu ya gharama halisi anazodaiwa Kapteni Komba na muda wa
deni hilo, mmiliki wa Kampuni ya Mpoki & Associates Advocates
inayoratibu mnada huo, Mpale Mpoki alisema maelezo yote yanayohusu kiasi
cha mkopo na muda wa deni yatajibiwa na CRDB wenyewe.MWANANCHI
Baada ya subira ya wiki mbili ili wenyeviti na wajumbe Mtaa wa
Migombani – Segerea, Dar es Salaam waapishwe na mamlaka husika bila
mafanikio, wananchi wameamua kuwaapisha viongozi hao kwa kutumia wakili
binafsi.
Wakati hali hiyo ikitokea Dar es Salaam, wilayani Rombo mkoani
Kilimanjaro baadhi ya wenyeviti wa vijiji walioshindwa wamekataa
kuwaachia ofisi viongozi wapya wakidai kuwa ofisi hizo ni mali ya CCM.
Katika tukio la Segerea lilitokea jana asubuhi Segerea Mwisho, Japhet Kembo aliapishwa kuwa ‘mwenyekiti’ pamoja na ‘wajumbe’ watatu ambao ni Rose Bernard Mhagama, Nyangeto Justin na Ramadhan Seif wote wa Chadema bila kuishirikisha Halmashauri ya Manispaa ya Ilala.
Akizungumza baada ya kuapishwa, Kembo alisema wananchi wamechoshwa na
danadana wanazopigwa na Manispaa ya Ilala za kutowaapisha viongozi
waliowachagua.
“Wananchi wamemtafuta wakili ambaye amekuja kusimamia suala hili kisheria na ndiyo maana zoezi limefanywa hadharani,” alisema Kembo.
Kembo alisema katika nafasi ya uenyekiti alipata kura 547, Uyeka Idd wa CCM kura 273 na Erick Mchata wa NCCR-Mageuzi kura 205.
MWANANCHI
Wakati Taifa zima likiwa katika kitendawili cha kumjua kiongozi wa
nchi atakayepatikana baada ya Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu, Mwenyekiti
wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema Rais ajaye anafahamika.
Akizungumza katika mahojiano maalumu jana, Jaji Warioba alisema si
kazi ngumu kwa Watanzania kumfahamu rais ajaye kwa kuwa katika miaka 50
tangu tupate uhuru, Watanzania wanazijua sifa za kiongozi bora.
Jaji Warioba alisema; “Tatizo la
kumjua rais afaaye tunalikwepa lakini linafahamika. Wanaotumia fedha na
lugha chafu katika kampeni na hao ndiyo wasiotakiwa.”
Hadi sasa wanasiasa zaidi ya 20 wakiwamo wa CCM na upinzani wamekuwa
ama wanatajwa au wameonyesha nia ya kugombea nafasi ya urais katika
uchaguzi mkuu ujao.
Ukiacha wale wanaotajwa, wanasiasa waliotangaza nia hiyo kutoka CCM
ni Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba, Waziri wa
Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, Mbunge wa Nzega, Hamis Kigwangala
na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, huku Mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid
Mohamed akitangaza nia kupitia ADC.
Kuhusu tetesi za kuwania urais Jaji Warioba alisema amelitumikia
Taifa kwa muda mrefu na aling’atuka kwa mapenzi yake, hivyo hawezi
kurudi tena katika siasa.NIPASHE
Misamaha ya kodi imeongezeka kutoka Sh. trilioni 1.48 mwaka 2012/13 hadi Sh. trilioni 1.82 ikiwa ni ongezeko la Sh. bilioni 334, kwa mwaka 2013/14.
Kutokana na hali hiyo, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imesema hali hiyo inashangaza kwa kuwa kamati hiyo inapiga kelele misamaha hiyo kupungua, lakini inazidi kuongezeka jambo ambalo linaonekana ni wapiga porojo.
Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe alisema wakati kamati hiyo ikihojiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), juu ya hoja mbalimbali za kamati zilizotakiwa kutolewa maelezo katika kikao kilichopita.
Kamishna wa TRA, Richard Beda, alisema ongezeko hilo linatokana na miradi mikubwa ya barabara na madaraja pamoja na ujenzi wa bomba la gesi na miradi mbalimbali ya mafuta na gesi.
“Misamaha hii imejikita katika kodi ya ongezeko la thamani (VAT), (Special Relief) (misamaha maalum) kwa kampuni zinazohusika na ujenzi na utafutaji na ujenzi wa bomba la gesi, kwa daraja la Kigamboni pekee kuna msamaha wa Sh. bilioni 676, na mafuta na gesi ni Sh. bilioni 100…sheria mpya ya VAT ndiyo itapunguza misamaha hii, tunataka iharakishwe,” alibainisha.
Zitto alisema kampuni binafsi zinapata misamaha ya Sh. bilioni 340 huku msamaha wa VAT ikiwa ni Sh. bilioni 639 na kwamba lengo la kamati ni kuona misamaha hiyo inafikia chini ya asilimia moja ya pato la taifa.
NIPASHE
Mashine ya mionzi ya kutolea huduma ya matibabu ya saratani katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road jijini Dar es Salaam, inatarajia kuanza kufungwa wiki hii ikiwa ni sehemu ya ukarabati wake hivyo kuendelea kukabiliana na ukosefu mitambo hiyo katika hospitali nyingi nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid alisema mashine hiyo ni moja ya zilizoharibika na kwamba ufungaji wake unaanza ndani ya wiki hii baada ya wataalamu na vifaa vyake kutarajia kuwasili kutoka Canada.
Aliongeza kuwa serikali pia ipo katika mkakati wa kuleta mtambo mwingine mpya wa mionzi ambao utagharimu Dola za Marekani milioni moja.
Kwa mujibu wa Dk. Rashid, gharama hizo zitachangiwa na Serikali kwa asilimia 50 na asilimia 50 zitatolewa na Shirika la Kimataifa la Atomi ‘International Atomic Agency.’
Kuhusu hali ya saratani nchini, alisema, hali bado ni mbaya kwani hadi sasa idadi ya wagonjwa inaendelea kuongezeka na hadi sasa kuna wagonjwa 33, 834 ambao wanaugua ugonjwa huo nchini kote.
Kati ya idadi hiyo, 7, 304 wanasumbuliwa na saratani ya shingo ya kizazi na iliyobaki ni kwa aina nyingine ikiwamo ya ngozi na matiti na chanjo dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi imeanza kutolewa katika mkoa ya Kilimanjaro.
Kwa mujibu wa Waziri Rashid, walengwa wakubwa wa chanjo hiyo ni pamoja na wasichana kwani katika umri huo kuna uwezekano wa kupatwa na ugonjwa huo.
MTANZANIA
Wakati Watanzania wakisubiri kujua hatima ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, aliyewekwa kiporo na Rais Jakaya Kikwete baada ya kuhusishwa na kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow, Waziri huyo amesafiri kwenda Davos nchini Uswisi kuungana na rais katika Mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani maarufu kama World Economic Forum.
Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Muhongo ameondoka nchini jana.
“Profesa ameondoka leo (jana) kwenda Switzerland (Uswisi) ambako ataungana na rais kwenye mkutano huo utakaoanza Januari 21 hadi 24,” kilipasha chanzo hicho.
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Salva Rweyemamu, ili kuthibitisha taarifa hiyo, hakuweza kutoa jibu na badala yake kumporomoshea mwandishi matusi huku akimwambia aachane na habari hiyo.
“Acha habari zenu za kipumbavu hizo,” alisema Salva, na alipoulizwa habari za kipumbavu ni zipi na kwanini anatukana badala ya kutoa majibu alisema: “Nimekwambia acha upumbavu, kama unataka habari nipigie na kama hutaki usinipigie, siyo kila kitu mnachoandika tu lazima nizungumzie,” alisema na kukata simu.
Akizungumza na wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam Desemba 22 mwaka jana, Rais Kikwete alitangaza kumuweka kiporo Profesa Muhongo akisubiri kupata ufafanuzi kuhusu mambo kadha wa kadha ili kujiridhisha kabla kuujulisha umma juu ya hatua atakazochukua dhidi ya waziri huyo.
MTANZANIA
Vurugu zimetokea jana kwenye ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini baada ya makundi yanayopingana ndani ya Chama cha ACT-Tanzania kukutana ana kwa ana katika ofisi hiyo kwa ajili ya kikao cha usuluhishi.
Baada ya kukutana kwa makundi hayo, ghafla walitokea vijana wanaodaiwa kukodiwa na Mwenyekiti aliyesimamishwa, Kidawi Limbu na kumvamia Katibu Mkuu wa muda wa chama hicho, Samson Mwigamba.
Vurugu hizo zimetokea ikiwa ni siku chache baada ya Halmashauri Kuu ya chama hicho kumsimamisha uongozi Limbu na kumwondoa katika nafasi yake aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Leopold Mahona kwa makosa ya kinidhamu.
Mwigamba alidai vijana hao wamekodiwa na Limbu kwa lengo la kumfanyia vurugu baada ya kuona mikakati yake imekwama ndani ya chama.
“Limbu alikuja na kundi la vijana kama 12, kati yao wawili aliwasafirisha kwa ndege kutoka Arusha na mmoja anaitwa Gerald Emmanuel, pia alikuwamo Mwenyekiti wa Geita, Katibu Uenezi Ukonga, Katibu Uenezi Jimbo la Kinondoni pamoja na kina Mahona.
“Wakati tunatoka kikaoni nikawa pale nje nasubiri gari linichukue, akaja Gerald huku akishika shati langu akidai ananidai shilingi milioni moja na lazima nimlipe pale pale, nilishangaa sana na hapo ndiyo nikajua kuna kitu Limbu amefanya ili wale vijana wanivuruge na baadaye nikasirike na kuonekana nimepigana,” alisema Mwigamba.
MTANZANIA
Mtoto wa miaka 15 mkazi wa Manzese jijini Dar es salaam, anadaiwa kubakwa na kulawitiwa na mjomba wake aliyetajwa kwa jina la Hassan Maumba ambaye kwa sasa anashikiliwa na polisi katika kituo cha urafiki ambaye alikua akifanya kitendo hicho kwa muda wa miaka mitatu huku akitishia kuua.
Mbali na kulawitiwa mtoto huyo pia alidaiwa kulazimishwa na mjomba wake huyo kumyonya damu baada ya kujikata na wembe,huku akimtishia na kisu kama angekataa au kutoa taarifa hizo kwa mtu yoyote.
Mtoto huyo ambaye ni yatima alimaliza darasa la saba mwaka jana na alisema mjomba wake alianza kumfanyia hivyo wakati akienda bafuni kuoga.
“Siku ya kwanza nilipoingia bafuni, mjomba alikuja na kuanza kuniingiza vidole sehemu za siri huku akinitisha nisimwambie mtu,aliendelea hivyo na kufikia hatua ya kuniingilia kinyume na maumbile huku mke wake akiwa hajui na kunitishia kuniua kama ningesema“alisema mtoto huyo huku akibubujikwa machozi.
~millardayo.com
USISITE KUTUACHIA UJUMBE WAKO HAPO CHINI
Post a Comment