Siku chache baada ya kuhusishwa na mpango wa kumsajili mshambuliaji raia wa Ivory Coast Wilfred Bony, mabingwa watetezi wa ligi kuu ya England Manchester City wametajwa kuongoza mbio za kumsajili kiungo wa Everton Ross Barkley na klabu hiyo imeandaa ofa ambayo ina uhakika kuwa haitakumbana na kikwazo chochote toka Everton na kwa mchezaji mwenyewe.
Manchester City wanadaiwa kuwa wameandaaa ofa ya paundi milioni 45 kwa ajili ya mchezaji huyo huku wakiwa tayari kumvutia kwa dau nono la mshahara wa paundi 130,000 kwa wiki kiasi ambacho kitakuwa kinauzidi mara mbili mshahara wake wa sasa.
Klabu ya Everton kwa upande wake iko tayari kumruhusu Barkley kuondoka ili mradi ihakikishiwe ada ya uhamisho ya paundi milioni 45 ambazo kwa upande wake itazitumia kuboresha kikosi cha kocha Roberto Martinez.
Hata hivyo Manchester City watakumbana na vita kali katika mbio za kumsajili Barkley kwani klabu kadhaa ikiwemo Liverpool zimekuwa zikimtolea macho.
Hata hivyo itakuwa vigumu kwa Barkley kujiunga na Liverpool kutokana na historia ya upinzani wa jadi uliopo baina ya Liverpool na Everton upinzani ambao mara nyingi hufanya iwe vigumu kwa timu hizo mbili kubadilishana wachezaji.
USISITE KUTUACHIA UJUMBE WAKO HAPO CHINI.
Post a Comment