MOTO mkubwa umeteketeza maduka 18 katika mtaa wa
Kwakivesa wilaya ya Handeni mkoani Tanga baada ya lori lililokuwa
limebeba mafuta kugonga nguzo ya umeme kupinduka na kisha kuanza kuwaka
moto uliosambaa hadi kwenye maduka hayo.
Taharuki hiyo imetokea leo majira ya saa 5:00
asubuhi baada ya lori hilo lililokuwa kwenye mwendo kasi kutaka kumkwepa
mwendesha bodaboda na kujikuta likiacha njia na kugonga nguzo ya umeme
na kusababisha hasara kubwa kwa wananchi huo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Frasser Kashai
amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kudai kuwa moto huo ulitokea
saa 5.asubuhi katika mtaa huo kufuatia roli la mafuta aina ya Fuso
kugonga nguzo ya umeme na kusababisha betri kutoa cheche zilizosababisha
moto kuanza kuwaka.
Kamanda Kashai amesema roli hilo lilikuwa
likiendeshwa na dereva Ali Makelele ambaye bado hajapatikana huku utingo
wake aliyemtaja kwa jina moja la Mfundo akiwa amekimbizwa hospitali ya
Wilaya ya Handeni kwa matibabu Zaidi baada ya kuungua vibaya.
“Moto ulianza kuliteketeza roli hilo la mafuta na
baadaye ukasambaa kwenye maduka jirani ,hali ilikuwa mbaya sana, hadi
sasa hatujajua hasara iliyopatikana, tutakapokuwa na taarifa kamili
tutawataarifu“, amesema kamanda Kashai.
Aidha mashuhuda wa tukio hilo wanaeleza kuwa moto
huo ulishika kasi kwa haraka kutokana na hali ya hewa kuwa ya upepo
mkali licha ya juhudi za wananchi kuuzima lakini uliwashinda nguvu.
Aidha jeshi la polisi limelaani mtindo unaoota
mizizi hivi sasa wa wananchi kujichukulia sheria mkononi kwani baada ya
tukio la moto kutokea kikosi cha zimamoto kutokea Korogwe kilifika
katika eneo la tukio lakini badala ya kuachwa kufanya kazi yake
kikashambuliwa.
Shambulio hilo la wananchi kwa zimamoto
limesababisha hasara ikiwa ni pamoja na kuvunjwa vioo vya gari, kupotea
kwa vitendea kazi pamoja na baadhi ya askari wa zimamoto kujeruhiwa.
USISITE KUTUACHIA UJUMBE WAKO HAPO CHINI.
Post a Comment